Septemba 18, mwaka huu wa 2014 historia ilijirudia katika nchi yetu hii. Nasema hivi kwa sababu Kiongozi Mkuu wa Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini (CHADEMA), Mheshimiwa Freeman Mbowe alitiwa msukosuko wa kihistoria.

Hii mimi ilinikumbusha tukio la mwaka 1958 pale Mwenyekiti wa TANU – chama cha upinzani kwa Serikali ya mkoloni aliposhtakiwa eti kwa ‘uchochezi’ baada ya kuanika uovu wa ma-DC wawili- yule wa Musoma (Mr. Weeks) na wa Songea (Mr. Scot) walioshabikia uchaguzi wa mseto na kuwakandamiza wana TANU waliopinga utaratibu ule wa kura za mseto.

Tofauti kati ya tukio la mwaka 1958 na hili la mwaka 2014 ni njia tu zilizotumika. Wakati Baba wa Taifa aliposhitakiwa – hakwenda na kundi la wapambe (mashabiki) kumsindikiza, bali alifuatana na mawakili wake watatu tu -nao walikuwa Bwana Pritt QC, Bwana M. Ratansey na Bwana Jhaveri.

Kumbe kiongozi wa upinzani mwaka huu 2014 alipokwenda Makao Makuu ya Polisi kuitika mwito wa polisi, alisindikizwa na washabiki, waandishi wa habari na wanasheria wake. Msemaji wa kisheria wa CHADEMA alisema wazi kuwa Mwenyekiti wao atapata ushauri wa kisheria wakati atakapokuwa anahojiwa Polisi. Tamko hili la busara lilikuwa sahihi kabisa na lilitosha sana kumlinda Mwenyekiti wakati wa mahojiano yake pale Polisi.

Kilichotokea ni wale mashabiki, wapambe na waandishi kutoka vyombo vya habari kuzonga Makao Makuu ya Polisi kulisababisha kutokuelewana; na ndipo lilitokea sokomoko la kihistoria. Wapambe na waandishi wa habari kusukumwa, kupigwa na kutishiwa kwa mbwa!

Kwanini haikutumika busara katika tukio hili? Mwaka 1958 Mwalimu alionya wafuasi wake wa upinzani kwa Serikali (wanaTANU) kwa maneno haya ya tahadhari. Nanukuu: “Ndugu wananchi, jihadharini. Adui anashindwa, anahangaika kwa sababu hana njia ya kupinga kilio chetu. Njia yake ni moja tu nayo ni kutaka ghasia ili atumie bunduki. Tusimpe nafasi hii. Msichochewe mkafanya ghasia na matata. Kaeni kimya na wachangamfu kama kawaida yetu. Adui atateketea bila shaka” (SAUTI YA TANU Na. 29 tarehe 27 Mei 1958 ibara ya 4).

Kumbe mwaka huu uongozi wa upinzani haukutoa tahadhari namna ile, bali ulitoa maelekezo katika Mkutano Mkuu wa Chama kuwa, nanukuu: “Hatuwezi kukaa kimya huku maoni ya Watanzania yakiwa yanachakachuliwa. Hivyo basi, tutashirikiana na taasisi mbalimbali, UKAWA kufanya migomo na maanamano nchi nzima bila kikomo… aidha kuwe na kibali cha Polisi au laa, na kwamba kuna watu watakaokuwa mstari wa mbele watajeruhiwa, lakini lengo likiwa kufikisha ujumbe wenye sura ya wananchi” (Tanzania Daima Toleo Na. 3573 la Jumatatu tarehe 15 Sept. 2014 uk. 3 ibara ya 8).

Neno “watajeruhiwa” linahatarisha usalama wa watu. Ni nia iliyodhamiriwa (in anticipation) tangu mwanzo.

Hapa pana tofauti kubwa ya miongozo katika vyama vya upinzani kati ya upinzani ule wa miaka ya 1958 kupinga ukoloni na ubeberu wa Wazungu kwa kudai wananchi wapate haki yao ya kujitawala; na upinzani wa leo mwaka 2014 kati ya Serikali ya CCM ya wananchi wenyewe kwa wenyewe juu ya uchakachuaji wa Rasimu ya Katiba yenye kubeba mawazo ya wananchi.

Nikifikiria hila zile za mkoloni kuhadaa wananchi kwa kuleta uchaguzi wa mseto eti ndiyo njia ya kuelekea kwenye Uhuru wa Tanganyika, na kulinganisha na hali ya sasa Serikali ilipoleta Rasimu ya Katiba mpya naona kama kuna mfanano wa mazingira kuwapatia wananchi KATIBA yao wenyewe kwa namna ya mizengwe au hadaa katika Bunge Maalum la Katiba (BMK).

TANU siku zile ilipinga sana kulazimisha wananchi wake wapige kura za mseto eti wachague Mzungu, Mhindi na Mwafrika katika kupata Uhuru wetu. Hivi sasa upinzani wanapinga sana namna mijadala inavyoendeshwa ndani ya BMK hasa kwa kukosekana ile dhana ya maridhiano.

TANU waliitisha Mkutano Mkuu wa mwaka pale Tabora katika ukumbi wa Kanisa Katoliki. Moja ya madhumuni ya mkutano yalikuwa kuongelea ule utaratibu wa KURA TATU (tripartite vote). Masharti yaliyotolewa na mkoloni katika uchaguzi ule yalikuwa magumu kwa Mwafrika (mwananchi), na hivyo wakoloni wangejipatia ushindi wa chee.

Mwalimu Nyerere alijua kuchezea turufu za karata zake na akatumia methali ya Kiswahili isemayo ‘SAMAKI MKAANGE KWA MAFUTA YAKE’, yaani uamuzi ule wa hatari na wa kibaguzi, basi huo huo utumike kumponda mkoloni mwenyewe. Waswahili wengi hilo hawakulielewa.

Basi, katika ule mkutano wa Tabora wanachama karibu wote wa TANU walikwenda na nia moja tu kupinga kwa nguvu zote huo uchaguzi wa KURA TATU – Uchaguzi wa MSETO (Tripatite voting) na kwa namna ile TANU ingeususia uchaguzi ule wa mwaka 1959/1960.

Vigogo kama akina Bhoke Munanka, Sheikh Suleiman Takadiri, Bwana Zuberi Mtemvu aliyekuwa TANU Organising Secretary na wengine walijipanga kwa hilo. Hawa walisema yafaa kura isipigwe ilaISUSIWE kabisa.

Busara za Mwalimu zilisema hivi: “Madhali (TANU) hawatapiga kura, vyama vingine vitapata nafasi ya kuingia katika LeGCO (Baraza la Kutunga Sheria) na hapo ‘lengo’ letu (TANU – upinzani) halitapata wasaa wa kuingia katika Serikali na kuongoza nchi”.

Baada ya mabishano makali na ya muda mrefu, hatimaye wazo la Mwalimu Nyerere lilikubalika. TANU ikashiriki katika ule uchaguzi wa kura tatu uliotakiwa na Serikali. Matokeo yake baadhi ya viongozi mashuhuri wa TANU walikihama chama na kuunda chama kingine kilichoitwa African National Congress (ANC). Tokeo jingine TANU ilishinda kwa kishindo uchaguzi ule wa mseto na hivyo mkoloni akafyata mkia na kuharakisha kutoa Uhuru wa Tanganyika.

Kama si hivyo jamani TANU isingetufikisha hapa tulipo leo, yaani tusingepata Uhuru mapema namna ile na bila kumwaga damu. (Taz. MWITO wa UHURU by Saadam Abdu Kandoro uk. 105 na Abdulwahid Sykes by Mohamed Said uk. 243).

Safari hii mwaka 2014 chama kikuu cha upinzani kiliitisha kikao chake pale Mlimani City, Dar es Salaam na katika mkutano ule CHADEMA walitoa azimio la kupinga  vikao vya BMK na kudhamiria kushinikiza hilo basi wafanye mgomo na maandamano nchi nzima.

Nimeelezea historia hii kuonesha namna busara za kutowapa nafasi watawala wenye nguvu za dola kama Jeshi la Polisi kutumia mabavu kuvunja maandamano ya wananchi wasio na silaha. Mwalimu alisema “tusiwape nafasi ya kuchochea ghasia na matata wasitumie bunduki”.

Katika maeneo mengine ma-DC wakoloni walitafuta mbinu za kufanya amani ivunjike ili watumie dola, mabavu na bunduki kuchachafya wananchi. Lakini TANU ilijengeka kisaikolojia kutokuanzisha mapambano (not to be provoked). Lakini wakichokozwa watatumia sheria zile zile zao (Serikali) kuwachachafya.

Nitoe mfano halisi. Mwaka 1959 kule Masasi alikuwapo DC matatizo akiitwa bwana Thatle. Huyu alidhamiria kuendesha kura za mseto wilayani.  Vijana wa TYL (Umoja wa Vijana wa TANU) pale Masasi kwa kufuata sheria, Jumamosi fulani waliomba kibali cha kucheza ngoma ya kienyeji (inaitwa Lijole) usiku pale Mkuti. Serikali ikatoa kibali. Ngoma (Lijole) ikapigwa kuanzia saa 3 za usiku hivi. Majira ya saa 6 za usiku Bwana DC akaja Mkuti eti kunyamazisha Waafrika wasipige kelele watu wanalala saa zile.

Vijana wa TYL kwa vile walikuwa na kibali halali cha ngoma usiku kucha walichofanya ni kumkamata Mzungu yule, wakamfunga kamba mikono na miguu na kumweka nyuma katika Land Rover ya TANU wakampeleka Bomani Masasi kumkabidhi kwa Polisi, chombo cha usalama.

Polisi walistuka sana kumuona bwana mkubwa wao DC kaletwa kama mhalifu. TYL wakaonesha kibali chao cha ngoma kina mhuri wa wilaya. Polisi hapo hawakuweza kuwafanya chochote vijana wale wa TYL ambao walirudi Mkuti wakaendelea na Lijole lao usiku kucha.

Nini kilitokea? Polisi Wilaya (kama bado nakumbuka vizuri (OCD akiitwa Ndamgoba) waliwasiliana na Kamanda wa Polisi (RPC) Mtwara na habari zikamfikia PC wa Mtwara akiitwa Bwana Pike. Wote wakaja kuangalia hali ya vurugu za Masasi. Ikathibitika DC aliwachokoza wanaTANU.

Jamani, yule mzungu alihamishwa mkuku mkuku toka Masasi na akaletwa DC mpya akiitwa Bwana Neath. Hapo Serikali ilikamatwa pabaya na chama cha upinzani (was caught wrong footedly). Mimi nilikuwa Mwalimu kule Masasi enzi hizo na huyo DC Neath ndiye aliyeniapisha pale wilayani wakati naomba pasipoti kwenda masomoni Uingereza miaka ile.

Nimetoa mifano hiyo miwili kwa kulinganisha na haya yaliyotokea Septemba 18, mwaka huu pale Makao Makuu ya Polisi. Kule miaka ya 1958 – 1959 Serikali kandamizi ya mkoloni ilipambana na upinzani wa TANU. Leo hii Serikali ya CCM imetoa Rasimu ya Katiba yenye kusheheni mawazo ya wananchi. Inaonekana Bunge la Katiba linayachakachua maoni haya ya wananchi. Upinzani wana hoja ya kilio cha wananchi kisikike. Hapo pana utofauti wa njia za kuibana Serikali iwe sikivu kwa matakwa ya wananchi.

Enzi za TANU Mwalimu alitumia ‘passive ressistance approach’ leo upinzani wanaona njia namna ile imepitwa na wakati. Wanataka njia ya mkato, njia endelevu ya jino kwa jino na jicho kwa jicho. Hii inaitwa njia ya ‘confrontations’ -mapambano! Mwaka ule wa 2005 chama cha upinzani cha CUF kilijaribu kutumia njia namna hiyo, wao waliita ‘NGANGARI’ kumbe Serikali ikatumia dola kwa njia ya ‘NGUNGURI’. Tunakumbuka hayo?

Sijui wangapi tungali tunakumbuka kilichotokea ndani ya CHADEMA baada ya kutolewa waraka ulioitwa Movement for Change (M4C) mwaka 2012. Waraka ule ulitamka wazi wazi hivi, nanukuu:“Uongozi wa sasa na wa taasisi yetu (CHADEMA) umefanya tuonekane kwamba taasisi yetu ipo kwa ajili ya kuvuruga amani ya nch. Yote hii ni kwa sababu tumekuwa hatuna mbinu mpya za mapambano zilizobadilika zaidi ya maandamano ya kila mara….” Waraka ule ulileta tafrani kubwa ndani ya CHADEMA. Si mnajua matokeo yake?

Hapo ndipo mimi nasema sheria zinatungwa na Bunge, zinasimamiwa na chombo cha usalama- ndio Polisi. Sasa kutunishiana misuli kutaleta kweli Katiba mpya na amani katika Taifa letu?  Sidhani!

Bunge la Katiba lilipoanza, waheshimiwa wabunge wa vyama vyote wakashirikiana kutunga kanuni zao za namna ya kuliendesha Bunge lile. Taifa lilipata matumaini kuona vyama vyote vya siasa vinashiriki. Pole pole hali ya hewa ikatibuka na kukatokea mtafaruku wa kimtazamo (approach). Ule moyo wa uzalendo na wa waridhiano ulitoweka ghafla. Ukatokea huu mpasuko wa mawazo usiozibika mpaka sasa.

ITAENDELEA