*Mapato ya Sh milioni 300 yaingia mifukoni

*Safari hewa zagharimu shilingi bilioni 1.316

*Bia, soda, teksi vyagharimu Sh milioni 133

*Masurufu pekee yalamba shilingi milioni 100

Ufisadi wa kutisha umebainika kuwapo katika Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA), huku Serikali ikiwa kimya, JAMHURI inawathibitishia wasomaji.

Kuanzia toleo hili, JAMHURI itawaletea mfululizo wa RIPOTI HII MAALUM inayohusu ufisadi ndani ya Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, kiasi cha fedha kilichoibwa, na wahusika wakuu kwenye kashfa hii.

Malipo kwa wakandarasi kwa kiwango kinachozidi kile kilichoidhinishwa, safari hewa, kutumia usafiri wa ndege wa daraja la kwanza, mameneja kujilipa fedha kwa majina hewa ya watumishi, matumizi holela ya masurufu, watumishi kulipwa posho za safari zaidi ya idadi halisi ya siku walizosafiri na ununuzi holela wa tiketi za ndege, ni baadhi ya mambo yaliyobainika kufanywa na Menejimenti na Bodi ya NCAA.

Malipo mara mbili ya dola 78,890

Imebainika kuwa Mamlaka imefanya malipo ya fedha mara mbili ya dola 78,890 (Sh 118,335,000) kinyume cha kanuni za fedha. Malipo hayo yametolewa kwa watoa huduma wawili — Antelope Tours and Travel Services Ltd na Cosmos Travel Agents.

Pamoja na kubainika Cosmos Travel Agents amelipwa fedha hizo bila kutoa huduma, Mamlaka imekaa kimya; hali inayoashiria kwamba kusudio lao lilikuwa moja — kuzitafuna.

Septemba 9, 2010 Mamlaka ilifanya malipo mengine kwa watumishi wawili ya dola 12,000 za Marekani (Sh milioni 18) kwa kila mmoja zikiwa ni posho ya kujikimu kwa safari nje ya nchi. Malipo hayo yalifanywa kupitia hati ya malipo Na. 309/166 hundi Na. 2161 kwa kutumia kibali chenye kumbukumbu Na. NCAA/D/647/Vol.IV/F.38.

Imebainika kuwa kibali hicho hicho kilitumika kufanya malipo mengine ya dola 42,800 za Marekani (Sh milioni 62.2) kwa watumishi wanane kupitia hati ya malipo Na.309/165 na hundi Na. 2160 ikiwa ni posho kwa safari nje ya nchi. Kwa maana hiyo, imebainika kuwa malipo ya Sh milioni 18 ni batili.

Uchunguzi umebaini kuwa mbali na hizo, kuna hati za malipo ya dola 501,484.60 za Marekani (Sh milioni 752.226) ambazo hazionekani. Kati ya fedha hizo, dola 469,114.60 zililipwa kama fedha taslimu ambazo walengwa na makusudio ya malipo hayajajulikana.

Malipo kwa fedha taslimu

Kanuni namba 89(1) ya Kanuni za Fedha za NCAA za mwaka 2006 inataka malipo yote yafanyike kwa mlengwa kwa kutumia hundi au kwa kuhamisha fedha kwa njia ya benki.

Hata hivyo, imebainika kuwa kwa wastani, asilimia 54 ya miamala ya malipo ya Mamlaka imekuwa ikifanywa kwa fedha taslimu kinyume cha Kanuni za Mamlaka. Mathalani, mwaka 2011/2012 imebainika kuwa akaunti ya fedha za kigeni katika Benki ya NBC ilikuwa na miamala 464 ya malipo yenye thamani ya dola 2,174,497.35. Miamala 253 yenye thamani ya dola 4,034,679.43 ilifanyika kwa fedha taslimu. Mfumo huo wa fedha taslimu umetumiwa kwa sababu ni mwanya mkubwa wa ubadhirifu wa fedha ndani ya NCAA.

Pamoja na benki, imebainika kuwa malipo mengine mengi kwa wafanyabiashara yanafanywa kwa fedha taslimu; hali inayochangia ukwepaji kodi ambayo ingepaswa kulipwa serikalini.

Mfano halisi ni wa Advances Business Software Company Ltd ya Dar es Salaam ambayo imetoa huduma ya mfumo wa uhasibu. Kampuni hiyo imelipwa kwa fedha taslimu kupitia kwa Geofrey Kalinga. Imelipwa Sh 33,225,000 na hivyo kuikosesha Serikali kodi ya Sh 5,980,500.

Matumizi bila idhini ya Bodi

Kanuni ya 4(1) ya Kanuni za Fedha za NCAA za mwaka 2006 hairuhusu kufanya matumizi yasiyoidhinishwa na Bodi. Tofauti na kanuni hiyo, NCAA ilitumia fedha zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 (Sh bilioni 2.441) na mwaka 2011/2012 (Sh bilioni 6.614). Kiwango kilicho kwenye mabano ni kile kilichotumika bila uamuzi wa Bodi.

Kwenye fedha hizo, kiasi kikubwa kilichotumika kimekuwa katika fedha za kigeni na kimetumika kwa ajili ya posho za safari nje ya nchi ambazo hazikuzingatia bajeti wala mipango ya NCAA. Imebainika kuwa mwaka 2010/2011 NCCA ilitumia dola 2,104,420 kwa ajili ya safari za nje kinyume cha dola 1,504,632 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

Mwaka 2011/2012 kiwango hicho kilipanda, kwani fedha zilizokuwa zimeidhinishwa ni dola 1,607,377.18 lakini kiwango kilichotumiwa bila idhini ya Bodi ni dola 3,226,140 za Marekani.

Imebainika kuwa safari nyingi za nje ni zile zilizohusu kwenda nchini Kenya. Baadhi ya malipo ya safari za nje hayaoneshi nchi ambazo watumishi husika walikwenda. Baadhi ya safari za Kenya hazikuwa na tija kwa Mamlaka, kwa mfano malengo ya baadhi ya safari hizo yalikuwa kwenda kufuata viza ambazo zingeweza kupatikana Dar es Salaam, matibabu, kusaka watengeneza bodi za mabasi, semina na mafunzo, kutafuta wazabuni na safari nyingi zisizokuwa na maana wala tija kwa NCAA na Taifa.

Mameneja kuidhinisha malipo hewa

Uchunguzi umebaini kuwapo kwa malipo ya safari ambazo hazikufanyika (safari hewa). Sh bilioni 1.316 zimeliwa kwa njia hiyo.

Malipo hayo yalihalalishwa kwa kughushi mihuri ya kutoka na kurudi nchini iliyopigwa kwenye hati za kusafiria na malipo mengine yaliishia mikononi mwa mameneja walioghushi saini za watumishi waliosingiziwa kuwa wamesafiri.

Baadhi ya majina ya baadhi ya wafanyakazi yametumika kuanzisha malipo ya safari hewa za nje ya nchi. Wakati baadhi ya mameneja hao wakikiri kuidhinisha malipo hayo, baadhi ya wafanyakazi wanakana kuomba kulipwa, na kupokea fedha za safari za nje ya nchi. Baadhi ya fedha za malipo ya safari hewa ambazo wafanyakazi wamekana kuzipokea na kusafiri, imebainika kuwa zilipokewa na kutafunwa na baadhi ya mameneja wa NCAA.

Mbinu zinazotumika kufanya malipo hewa ni watumishi kuanzisha malipo ya safari. Hao walioomba kibali cha safari, walijaza fomu za posho za safari na walipokea fedha wao wenyewe.

Watumishi wengine wanatumia majina ya watumishi wenzao kuomba kibali cha safari, kujaza fomu za posho za safari na kupokea fedha kwa niaba yao; na baadhi ya watumishi wanatumia majina, wanajaza fomu na kuchukua fedha kwa niaba yao.

Uchambuzi wa safari ambazo hazikufanyika unaonesha kuwa watumishi 44 walihusika kulipwa fedha kwa safari kati ya moja hadi 22 kwa mtumishi mmoja. Hati za malipo zinaonesha kuwa fedha hizo zimepokewa na watumishi 34. Kiasi cha fedha hizo kinahusu malipo kwa safari za wapokea fedha, na kiasi kingine walikipokea kwa niaba ya watumishi wenzao.

Wasimamizi au mameneja waliohusika kuidhinisha malipo hayo ya Sh bilioni 1.316 ni mameneja watano na maafisa wengine wanane.

Mameneja na maafisa walioidhinisha fomu za posho za safari hewa na kiwango cha miamala kwenye mabano ni Lilian Magoma (1), Fabian Chausi (2), Peter Makutian (4), Amiyo Amiyo (7), Regobertus Mackiros (8), Asantael Melita (10) Dk. Justine Muumba (26), Elinipendo Mbwambo (29) na Veronica Ufunguo aliyefunga kazi kwa kuidhinisha miamala 47. Fomu 23 hazikuwa na saini wala majina ya walioidhinisha. Miamala miwili haikuwa na saini.

Walioidhinisha vibali vya safari nje ya NCAA na idadi ya miamala kwenye mabano ni Laban Maruo (2), Injinia Joshua Mwankunda (2), Fabian Chausi (2), Dk. Victor Runyoro (3), Amiyo Amiyo (3), Vicent Mbirika (3), Patrice Mattay (4), Rogobertus Mackiros (9), Peter Makutian (10), Elinipendo Mbwambo (13), Dk. Justine Muumba (18), Asantael Melita (28) na Veronica Ufunguo (38). Fomu 15 hazikuwa na saini na nyingine kwa idadi kama hiyo hazikuwa na majina wala saini zinazotambulika.

Maofisa wanavyolipwa kwa safari hewa

Yafuatayo ni majina ya maofisa ambao uchunguzi umebaini kuwa walipokea malipo kwa safari hewa. Hata hivyo, baadhi yao wamekana na wengine wakidai kwamba saini zao zilighushiwa. Wakati wakichukua fedha hizo, dola moja ya Marekani ilikuwa wastani wa Sh 1,500.

Maofisa hao na kiwango walichochukua kwa dola za Marekani kwenye mabano ni: Alais Saitoti (8,640), Amina Ponera (8,640), Amiyo Amiyo (8,400), Asantael Melita (109,760), Azimio Mawolle (28,560), Benard Margwe (6,750), Bernard Mulunya (3,200), Boniface Losuritian (5,600), Boniface Mtandika (38,640), Bosco Monah (9,600), Daniel Olemoti (45,000), Elinipendo Mbwambo (67,200), Fabian Chausi (10,080-fedha alipokea Asantael na Veronica), Florence Shoo (4,480 –fedha zilipokewa na Veronica Ufunguo), Hendry Sweddy (9,520), Heri Kejo (8,600), Hillary Mushi (5,600), Isra Missana  (11,200), Israel Naaman (2,400), John Shambamtwe (4,800), Joseph Mallya (5,600), Joshua Mwankunda (16,800), Justine Muumba (11,200), Laban Moruo (5,600), Lilian Magoma (15,680), Lohi Zakaria (3,920), Marcel Bituro (2,880) na Mohamed Msafiri (10,300).

Wengine ni Moinga Lesasi (9,300), Nickson Nyange (89,600), Orgoro Mauyai (3,360), Patrice Matay (5,040), Peter Makutian (70,000 –anadai hakupokea fedha hizo), Raphael Kundy (10,080), Said Msangi (14,800), Shaddy Kyambile (22,400), Stephen Lelo (11,200), Tulalora Mbande (6,160), Veneranda Baraza (90,360), Veronica Ufunguo (41,440), Vincent Mbirika (17,360), Walter Mairo (4,800), Yohana Shema (2,400) na Yusuph Machumu (11,200).

Posho za safari zaidi ya idadi halisi ya siku

Ufisadi mwingine umebainika kuwapo kwenye malipo ya safari za nje ya nchi ambako baadhi ya wajumbe wa Menejimenti wanalipwa posho za safari  zaidi ya idadi halisi ya siku wanazosafiri.

Siku za ziada ambazo watumishi hao wamelipwa kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011 na 2011/2012 ni dola 95,959.64 za Marekani ambazo kwa wakati huo zilikuwa sawa na Sh milioni 143.939. Licha ya kutakiwa waliochukua fedha hizo wazirejeshe katika Mamlaka, agizo hilo halijatekelezwa.

Dosari nyingine iliyobainika kufanywa na uongozi wa NCAA ni matumizi holela ya fedha za masurufu kinyume cha Kanuni za Utumishi za Mamlaka Na, 3.7.2(ii). Kanuni hiyo inaagiza kuwa gharama za teksi kutoka hotelini hadi eneo la kazi au semina hazitalipwa na Mamlaka.

Imebainika kuwa masurufu yanatumika kulipigia gharama ambazo zimejumuishwa kwenye posho ya kujikimu na kugharimia matumizi yasiyoruhusiwa.

Gharama za chai, bia na teksi zatisha

Baadhi ya watumishi wanaolipwa masurufu ya safari za kikazi wanatumia sehemu ya fedha hizo kununulia soda, bia, vyakula, maji, teksi na matumizi mengine yasiyoruhusiwa kwa mujibu wa Kanuni za NCAA.

Imebainika kuwa katika kipindi cha mwaka 2010/2011 na mwaka 2011/2012 Sh milioni 138.136 zilitumika kwa matumizi yasiyokubalika kikanuni.

Baadhi ya watumishi waliolipwa fedha za masurufu wanatumia fedha pungufu ya zile walizolipwa, hivyo Mhasibu Mkuu ameelekeza  zikatwe katika mishahara ya watumishi husika. Hata hivyo, wahasibu walioagizwa kutekeleza amri hiyo wamepuuza. Hatua hiyo imeifanya NCCA ipate hasara ya Sh milioni 101.158 kutokana na kutokatwa fedha hizo.

Ujanja mwingine uliobainika ni kwamba masurufu yanatolewa kwa kiwango kikubwa bila kuzingatia mahitaji. Baadhi ya watumishi wanachukua masurufu ambayo wanatumia na kurejesha kati ya asilimia 10 na asilimia 67 ya kiasi walichochukua.

Aidha, imebainika kuwa masurufu ya dola 22,000 za Marekani yamelipwa kwa watumishi kadhaa bila kuingizwa kwenye rejista. Kutoingizwa kwenye rejista ni kinyume cha Kanuni za Fedha na hutoa mwanya wa kutumiwa kwa fedha za umma bila kutolea hesabu.

Sh milioni 87 zatafunwa kwa kazi zisizo na tija

Dola 58,180 ambazo ni sawa na Sh milioni 87.27 zimelipwa kwa maofisa mbalimbali wa NCCA kwa safari za kwenda Kenya kufanya ununuzi; kazi ambazo zingeweza kufanywa kwa njia ya matangazo ya kutafuta mzabuni.

Licha ya fedha hizo kutumiwa, hakuna mahali popote katika NCAA ambako kunaoneshwa thamani au faida iliyopatikana kutokana na safari hizo.

Mchanganuo wa ulaji huo ulikuwa kama ifuatavyo: Dola 12,600 zimetumika kumpeleka ofisa nchini Kenya kutafuta mtaalamu wa kutengeneza bodi ya basi la shule. Dola 6,240 kimetumika kufuatilia muuza vifaa vya kufuatilia magari kwa ajili ya NCAA. Dola 3,920 zimetumika kumsafirisha mtumishi kwenda Kenya kwa kile  kilichoelezwa kuwa ni vyanzo vya utafiti. Dola nyingine 9,600 zimetumika kumlipa mtumishi kwenda Kenya kufuatilia masuala ya ununuzi; dola 3,360 zimelipwa kwa mtumishi ili aende nchini humo kuonana tu na mtengeneza bodi za magari; dola 8,960 zimetolewa na NCAA kwa ajili ya muuzaji basi kubwa la utalii!; na mwisho zimetumika dola 13,440 kwa ajili ya kumtuma mtumishi nchini Kenya kufuatilia matengenezo ya basi!

Mitambo ya Sh milioni 140 yatelekezwa

Mwaka 2005 NCAA ilinunua mtambo wa kukagua mizigo (Cargo Scanner) wenye thamani ya Sh milioni 131.76. Mwaka 2009 NCAA ikanunua tena mtambo wa kupimia uzito wa magari yanayopita ndani ya Hifadhi kwa thamani ya Sh milioni 6.367. Uchunguzi umebaini pasi na shaka kuwa hadi mwaka jana mwishoni, mitambo hiyo haikuwahi kutumika.

Tiketi za ndege zanununuliwa kiholela

Ufisadi mwingine mkubwa umebainika kwenye eneo la ununuzi wa tiketi za ndege kwa safari za ndani na nje ya nchi. Hatua hiyo inatokana na udhaifu wa NCAA wa kutoweka taratibu. Kwa mwanya huo, kila mtumishi anayetaka kusafiri hutafuta ankara kutoka kwa wakala atakayempendekeza yeye. Bei za tiketi pia hazina udhibiti kwa kuwa zinatofautiana mno kwa safari moja kati ya wakala mmoja na wakala mwingine au mtumishi aliyeomba Ankara.

Safari za Wajumbe wa Bodi na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya NCAA zimekuwa za daraja la kwanza badala ya daraja la kati; ambalo ambalo ni kinyume cha Kanuni namba 3.7.4 ya Kanuni ya Utumishi za NCAA. Mfano hai kwa jambo hili ni hati ya malipo namba 310/379, hundi namba 2842 ambayo ililipia usafiri wa ndege wa daraja la kwanza badala ya daraja la kati.

Uchunguzi umebaini kuwa kuna vitendo vingi vya kughushi nyaraka za hati za madai zilizotolewa kwa huduma za tiketi za ndege. Hatua hiyo imechangiwa na mazoea ya kufanya malipo kwa kutumia nakala ya Ankara zinazowasilishwa kwa njia ya kiektroniki badala ya hati halisi.

Mfano halisi wa ufisadi kupitia mbinu hii ni safari ya watumishi wanne wa NCAA ya kwenda Istanbul, Uturuki iliyowasilishwa kwa ankara Na. 28151 ya Januari 14, 2011 kutoka kampuni ya Interlink Travel. Ankara hiyo ilighushiwa ili isomeke dola 25,164 za Marekani badala ya dola 18,878 za Marekani iliyokuwa imeandikwa kwa maneno.

Kughushi huko kunatokana na kubadilisha tarakimu za nauli halisi kutoka dola 4,718.25 kuwa dola 6,291 kwa mtu mmoja na hivyo kuifanya ankara ya Interlink Travel isomeke kuwa ni 25,164 za Marekani dhidi ya wakala mwenzake Sedec Travel & Tours ambayo ilikuwa dola 23,796. Malipo hayo yameandaliwa na Idara ya Utalii na yalifanyika kwa Sedec Travel & Tours kwa hundi Na. 013434 yenye thamani ya dola 23,796.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa kuna matumizi mengi ya malipo makubwa mno kwa safari za nje ya nchi za watumishi ikilinganishwa na vipaumbele vya matumizi mengine ya Mamlaka ya NCAA.

Kughushi mihuri kwenye hati za kusafiria

Kwenye vivuli vya hati za kusafiria, vikilinganishwa na kumbukumbu za safari kutoka Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kumethibitika pasi na shaka kuwa kuna matukio mengi ya kughushi. Baadhi ya mihuri katika hati za kusafiria imekuwa hainonekani katika kumbukumbu zilizowasilishwa Idara ya Uhamiaji.

Mmoja wa watumishi anayedai kupotelewa hati ya kusafiria, ameshindwa kuthibitisha madai yake. Kumbukumbu za Uhamiaji zinaonesha kuwa hati hiyo hiyo aliitumia kusafiri katika kipindi alichodai kwamba imepotea.

Kutokana na hali hiyo, kuna ukweli usiotiliwa shaka kwamba hati za kusafiria za baadhi ya watumishi zimegongwa mihuri bandia kuhalalisha malipo kwa safari hewa.

Uchunguzi umebaini kuwa hati za watumishi wafuatao zinatia shaka, na kuna kila dalili kuwa mihuri imeghushiwa ili kuhalalisha malipo hewa. Watumishi hao ni Veneranda Baraza (AB167047), Elinipendo Mwambo (AB443307), Elinipendo Mbwambo (AB124133), Veronica Ufunguo (AB441452), Joseph Mallya (AB486491), Nickson Nyange (AB16385), Daniel Olemoti (AB280289) na Vincent Mbilika (AB462075).

Hati ya Baraza ilikuwa na mihuri 52, lakini ni mihuri miwili pekee iliyokuwa halali. Mbwambo, hati yake ina mihuri 23; kati ya hiyo mihuri batili imebainika kuwa ni 20. Ufunguo hati yake ina mihuri 28, lakini 15 kati ya hiyo ni batili. Mallya hati yake ina mihuri 26; lakini 10 kati yake ni batili. Nyange ana taarifa zinazotia shaka akidai kwamba mara ya mwisho kuitumia hati yake kusafiria ilikuwa Februari/Machi, 2013 na kwamba ilipotea mwanzoni mwa Mei, 2013. Hata hivyo, uchunguzi umeonesha kuwa alisafiri kwa kutumia hati hiyo hiyo Mei 25, 2013 kurudi nchini kupitia mpaka wa Namanga mkoani Arusha.

Olemot kwenye hati yake ana mihuri 26, lakini uchunguzi umebaini kuwa mihuri 20 imeghushiwa; kadhalika Mbilika naye hati yake ina mihuri 15, lakini mihuri sita kati ya hiyo ni batili.

Sehemu ya pili ya ripoti hii maalum itaendelea toleo lijalo. Usikose kujua kiwango cha fedha kilichochotwa na wakuu wote wa Menejimenti na Bodi, upendeleo wa ajira kwa ndugu, mtumishi mdogo wa kike aliyejenga maghorofa Manzese kwa fedha za Ngorongoro; na mengine mengi. USIKOSE JAMHURI.