Hali si shwari katika Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kwani wakubwa wa chama hicho kwa sasa wanatazamwa kwa jicho la kutiliwa shaka katika uadilifu wao baada ya kutumia ukabila, udugu na upendeleo wa kila aina kuendesha chama hicho, JAMHURI limebaini.

 Tuhuma kadhaa zimeelekezwa kwa viongozi wa chama hicho, hasa Katibu Mkuu, Deus Seif. Miongoni mwa tuhuma hizo ni pamoja na kutoa ajira bila kuzingatia kanuni za utumishi na kuwashughulikia ‘waliompinga’ wakati wa uchaguzi uliomuingiza madarakani kwa kuwashusha vyeo.

 Mbali na tuhuma hizo, kigogo huyo na mwenzake wanadaiwa kutumia fedha za CWT kusafiri kwenda kutazama mechi kati ya Taifa Stars ya Tanzania na timu ya raifa ya Cape Verde wakati wa michuano ya AFCON iliyofanyika nchini Cape Verde, ambapo Tanzania ilifungwa 3-0. Walikaa huko nje ya nchi kwa siku tano, kuanzia Oktoba 8 hadi 12, mwaka jana kwa gharama za CWT.

Katika ajira za upendeleo, katibu mkuu huyo anadaiwa kumwajiri shemeji yake, yaani mdogo wa mkewe na kutoa ajira kwa dereva wa familia katika ofisi za CWT.

Kutazama AFCON

Katibu Mkuu Seif na mwenzake anayeitwa Abubakar Allawi walitumia fedha za CWT kusafiri nje ya nchi kwenda kutazama michuano ya AFCON, Oktoba 8-12 mwaka 2018.

 Katika hilo, katibu huyo amekiri kwenda kutazama michuano hiyo na mwenzake, lakini akisisitiza kuwa hakutumia fedha za CWT bali fedha binafsi.

 “Kwanza mimi ni Mjumbe wa TFF (Shirikisho la Chama cha Soka Tanzania). Ni Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita, mwenzangu Abubakar Allawi ni Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani. Mwaka jana TFF ilikodi ndege wakasema wanaoweza wachangie gharama kidogo, na sisi tulishiriki kama viongozi wa soka kwa gharama zetu wenyewe. Kwa kifupi kama TFF wasingekodi ndege nafikiri tusingeweza kwenda, hatua ile ilileta nafuu fulani, lakini tulitumia gharama zetu na siyo za chama,” amesema.

Hata hivyo, mmoja wa watumishi aliopata kuwashughulikia ni Prosper Lubuva ambaye katika mazungumzo na JAMHURI amesema yeye ndiye aliyepewa jukumu la kuratibu safari hiyo kati ya TFF na CWT kwa niaba ya viongozi wake hao.

“Fedha zilizotumika kwenda Cape Verde ni za CWT. Mimi ndiye niliyeambiwa nishughulikie suala hilo, lakini kwa sharti kwamba nisiseme kwa mtu yeyote na nikisema nitakiona cha mtema kuni. Awali sikujua hata ofisi za TFF ziko wapi, lakini nilizijua baada ya shughuli hiyo. Fedha ziliidhinishwa kabla ya kujua gharama halisi za safari. CWT ilipanga bajeti ya dola za Marekani 1,200 kwa kila mmoja wao, lakini baada ya kufuatilia TFF ilibainika gharama ni dola 1,500.

“Nilifanya kazi hii nikiwa na shughuli nyingine nyingi, sikuwa na muda wa kumwambia mtu. Sasa ile mechi ya Cape Verde na Taifa Stars ilionyeshwa ‘live’ kwenye televisheni, sisi (CWT) tunalo ‘group’ letu la mtandaoni, mjadala ukaanza kwamba wameonekana viongozi wetu wakiwa kwenye mechi. Rais wa chama chetu, ni mmoja wa aliowatumia ‘message’ kwamba tumewaona,” amesema Lubuva na kuongeza kuwa, viongozi hao waliporudi Tanzania waliamini yeye ndiye aliyevujisha siri hiyo ya wao kusafiri kwenda Cape Verde, lakini mwenyewe anasema kisa cha siri kujianika ni ‘mechi kuwa live’.

Anasema moja ya adhabu alizopata ni kushushwa cheo pamoja na wenzake kadhaa, lakini wameamua kupambana na uamuzi huo kupitia mkono wa Mahakama.

“Kumewahi kufanyika majaribio kadhaa ya kunitaka niwasaliti wenzangu katika kupigania haki yetu ya kushushwa vyeo bila kuzingatia kanuni na taratibu. Niliwakatalia,” anasema.

Kudhoofisha CWT

Taarifa ambazo JAMHURI limezipata kutoka kwa ‘majeruhi’ wa uongozi wa sasa zinabainisha kuwa uongozi wa Katibu Mkuu wa CWT, Seif, umekuwa ukilalamikiwa kukidhoofisha chama hicho.

 Baada ya kuingia ofisini, Deus Seif, ameshusha baadhi ya wakuu wa idara vyeo kwa madai kuwa hawakumuunga mkono katika uchaguzi ambao alishinda na kuwa Katibu Mkuu.

Baadhi aliowashughulikia ni pamoja Mwandile Kiguhe aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Jinsia na Walimu Wanawake, ambaye ameshushwa kwenda kuwa Katibu wa CWT Wilaya ya Hanang.

Wengine ni Prosper Lubuva – Mkuu wa Idara ya Elimu na Mafunzo aliyepelekwa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kuwa Katibu wa Wilaya wa CWT, Simon Keha aliyekuwa Mkuu Msaidizi katika Idara ya Elimu na Mafunzo, amepelekwa kuwa Katibu wa CWT Wilaya ya Serengeti; Dagobati Deogratius aliyekuwa Mkuu Msaidizi katika Idara ya Utetezi amepelekwa kuwa Katibu wa CWT Wilaya ya Mkalama.

 Katika hilo, Seif amesema: “…chama (CWT) kina vikao ngazi ya chini (ya shule), ngazi ya wilaya, ngazi ya mkoa na ngazi ya taifa. Masuala ya kiutumishi kuna chombo cha Kamati ya Utendaji ya Taifa, kinatambuliwa na Katiba ya Chama.

“Wakisema Katibu Mkuu amefanya hivyo wanakosea. Mimi ni Katibu wa vikao vya kitaifa, uamuzi ukishafanyika anaachiwa Katibu Mkuu atekeleze.

“Kwa hiyo mwisho wa siku ikionekana kuwa Katibu Mkuu kasaini, inaonyesha mimi ndiye niliyeamua. Hilo suala lilianzia kwenye menejimenti ambayo wajumbe wake ni Rais, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu na Mweka Hazina (wote wa CWT), na kikao hicho kilifanyika Oktoba 24, 2018 na Mwenyekiti wa kikao hicho ni Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania, baada ya hapo tukalipeleka suala hili kwenye Kamati ya Utendaji wa Taifa Oktoba 31, 2018, na Mwenyekiti wake ni huyo huyo Rais wa CWT.

“Na wajumbe wa kamati hiyo ni mwakilishi mmoja kutoka kila mkoa ambao ni makatibu wa mikoa 26 pamoja na sisi wajumbe wanne wa menejimenti inakuwa na jumla ya wajumbe 30. Hatukulimaliza hilo suala, tumekuja kulimaliza tarehe 2/11/2018 chini ya Mwenyekiti Rais wa CWT, baada ya hapo ndipo ikafuata hatua ya utekelezaji.

“Sasa wakisema mimi nahusika wanakosea kwa sababu kwa mujibu wa Katiba ya Chama Ibara ya 23.3 kipengele C (i) [CWT] imepewa mamlaka ya kuajiri ikiwa na maana pia ya kuondoa (kufukuza) kazini.”

 Pamoja na majibu hayo, baadhi ya ‘majeruhi’ wamedai suala lao halikuchukua mkono stahili, kwa hiyo wamefungua mashtaka kortini.

 Kukiuka kanuni za ajira

Tuhuma nyingine zilizoelekezwa kwa Katibu huyo wa CWT ni pamoja na kutoa ajira za watumishi kwa kukiuka kanuni za chama hicho, akiajiri kwa upendeleo baadhi ya watu wakiwamo wenye uhusiano wa kindugu bila hata usaili.

Kati ya hao ni dereva wake wa familia, Faraji Kanyama na mwingine ambaye ni msaidizi ndani ya ofisi yake, Katibu Muhtasi, Ansila Masawe, ambaye ni shemeji yake – mdogo wa mkewe.

Katika orodha hii ya ajira za upendeleo yumo pia Afisa Habari aliyechukuliwa kutoka Geita bila kufanyiwa usaili, Batholomeo Chirwa, huyu akidaiwa kupenyezwa kwa shinikizo kutoka kwa waziri mmoja ambaye aliwahi kuwa Afisa Taaluma Manispaa ya Geita kabla ya kuingia katika siasa, akianzia ubunge.

 Seif amejibu tuhuma hizi kwa kusema: “Taratibu zilifuatwa, nafasi za kazi zilitangazwa wazi kupitia vyombo mbalimbali vya habari, hivyo Idara ya Utumishi ikachagua.

“Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa Taifa mmoja kila mkoa wote walikuwepo, tukisema kuna kundi la Katibu watakuwa wanakosea. Sina uhusiano wowote na hao waliotajwa. Na siyo hao tu, hata ndani ya CWT sina ndugu yeyote.”

 

Kashfa ya vyeti feki

Katika uongozi wake CWT, katibu mkuu huyo amemlinda mmoja wa watumishi waliokumbwa na kashfa ya vyeti feki katika operesheni iliyoendeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais Dk. John Magufuli.

“Kuna mtumishi alikumbwa na kashfa ya vyeti feki baada ya zoezi la Magufuli, akaondolewa kwenye ajira CWT, lakini yeye akampeleka kuwa katibu wa CWT Mpanda (jina linahifadhiwa),” kimeeleza chanzo chetu cha habari. Jina limehifadhiwa kwa kuwa mtuhumiwa hajapatikana ingawa bosi wake amethibitisha kuwa zilikuwapo tuhuma.

Seif amejibu tuhuma hizo kwa kusema: “Vyama vyote vya wafanyakazi kikiwemo CWT viliandikiwa barua na Serikali kwa ajili uhakiki wa vyeti (kipindi hicho sijawa Katibu). Mwaka jana nilivyofika hapa nilienda kupokea majina hayo, na kuyapeleka kwenye chombo kinachohusika ambacho ni Kamati ya Utendaji ya Taifa.

“Kuhusu… (jina linahifadhiwa) kwanza hakuwa mtumishi wa chama (ingawa sikuwepo), alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa, baadaye akaomba nafasi ya Katibu wa CWT wa wilaya akapata, akapewa barua na katibu aliyekuwepo, akaenda kuomba barua ‘secondment’ kwa mwajiri wake, alivyopata hicho kibali ndiyo majibu ya uhakiki yakatoka na kuonekana ana matatizo ya vyeti.

 “Kwa hiyo alikuwa hajaanza ukatibu wala kupangiwa kituo cha kazi licha ya kuwa tayari alishapata barua ya ‘secondment’.

“Baada ya mimi kuingia mwaka jana akaniletea barua kwamba mimi nimerudishwa kazini na kwa kuwa nilikuwa nina kibali cha kufanya kazi CWT ninaomba nirudi kwako unipangie kituo cha kazi, ikabidi nimuite Afisa Utumishi anipe taarifa zaidi.

“Baadaye tukapeleka shauri hilo kwenye chombo cha ajira cha chama, wao wakaniambia niandike barua ya siri kwa mwajiri wake yeye ndiye akwambie na siyo Sabato akwambie.

“Nikafanya hivyo, ndipo nikajibiwa kwa barua ya tarehe 24/12/2018 kutoka kwa mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bunda,” amesema Seif. JAMHURI limeiona barua hiyo, lakini halikuruhusiwa kuinakili popote.

“Baada ya kupata barua hiyo, nami nikaielekeza kwa Afisa Utumishi, kwa hiyo tukamrudisha kazini,” ameeleza katibu huyo.

Uhakiki wa hesabu

Inadaiwa kuwa Katibu Mkuu huyo aliendeleza mpango wake wa ‘kuwashughulikia’ wasiomuunga mkono, na moja ya mbinu aliyotumia ni kuitisha ukaguzi wa hesabu kwenye ofisi za makatibu aliowalenga, na kabla ya mchakato wa ukaguzi haujakamilika, akawaondoa kazini.

“Alifanya hivyo kwa lengo la kuwakomoa kwa kuwa hawakumuunga mkono katika uchaguzi uliopita,” ameeleza mmoja wa viongozi mwenye malalamiko dhidi ya katibu huyo ambaye pamoja na wenzake, ambao wameomba malalamiko yao hayo yafikishwe kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania kuinusuru CWT na kile walichokieleza kuwa “chama hicho kinaangamia.”

 Katika ufafanuzi wake, Katibu wa CWT amelieleza JAMHURI: “Kwanza kuna ukaguzi wa aina mbili. Ukaguzi wa kushtukiza na ukaguzi wa kawaida, ama maalumu.

 “Na mimi ndiye Afisa Masuhuli wa chama, napaswa kuhakikisha fedha ya chama inatumika kulingana na utaratibu wa chama chetu.

 “Ukaguzi maalumu kwa mujibu wa Katiba ni ukaguzi wa Katibu Mkuu, yaani anaamua yeye, na zoezi lile lilifanyika kweli, baadaye tukapeleka kwenye kamati husika, ambayo ni Kamati Ndogo ya Hesabu za Chama, ambapo yalionekana makosa makubwa sana.

“Baadaye tukapeleka kwenye Kamati ya Ajira ya Taifa, wao kama chombo cha uamuzi, waliwasimamisha kazi na siyo Katibu Mkuu.

 “Wamesimamishwa tu siyo kwamba wamefukuzwa, na wiki ijayo wataitwa kusikilizwa ili na wao wajibu hoja zilizoibuliwa na kamati. Waliofanyiwa ukaguzi ni watano, lakini waliosimamishwa ni watatu. Naogopa kusema wamesimamishwa kwa sababu gani kwa kuwa suala hilo halijafika mwisho. Likifika mwisho tutasema.”

Mipango uchaguzi 2020

Fukuto zaidi ndani ya CWT linaainisha kuwapo kwa mipango ya chini kwa chini kuelekea kampeni za uchaguzi wa viongozi ndani ya chama hicho hapo mwakani, na kwamba, katibu huyo ni kati ya wanaopanga safu kuelekea uchaguzi huo, akidaiwa kutumia nafasi yake kujiimarisha.

Akizungumzia madai hayo amesema: “Sijui kujiimarisha wanamaanisha nini, kwa sababu ni lazima nifanye kazi nzuri ili kila mwanachama aone kuna Katibu Mkuu. Sasa kama huko ndiko kujiimarisha itafsiriwe tu hivyo. Siwezi kukaa tu ofisini niache kutembelea chama kujua changamoto na kuzifanyia kazi.

“Nimefanikiwa kusimamia nidhamu ya chama, kuvunja mikataba ya ajabu (ambayo haifai kuisema hadharani). Sasa kama huko ndiko kujiimarisha, acha nieleweke hivyo.”

Majibu ya Rais CWT

Awali, alipoulizwa kuhusu masuala hayo tata katika CWT Jumamosi iliyopita, Makamu wa Rais wa chama hicho, Christopher Banda, aliliambia JAMHURI kwamba yeye si msemaji wa chama hicho na kwamba angeweza kuzungumzia masuala hayo endapo angepewa idhini hiyo na Rais wa CWT, Leah Ulaya.

“Kwa mujibu wa itifaki, siwezi kuzungumzia masuala ya chama kama Rais wetu wa CWT yupo. Ningeweza kufanya hivyo kama ama hayupo au ameniagiza kuzungumza, nakushauri umtafute Rais – Mama Leah Ulaya,” amesema Banda.

JAMHURI lilipomtafuta Leah Ulaya awali hakupokea simu yake ya mkononi na baada ya dakika chache alitaka atumiwe ujumbe mfupi wa simu. Ujumbe huo ulitumwa kwake, na baada ya kuupokea alijibu kuwa yuko katika kikao atafutwe baadaye.

Ilipofika jioni ya Jumamosi, alipigiwa simu tena kama alivyoelekeza na majibu yake yalikuwa hivi: “Hayo masuala ni magumu, ili kuyazungumzia hayo nahitaji utulivu. Siwezi kuyazungumza kwa sasa.”

Alipotakiwa kutoa majibu kwa ufupi endapo anakanusha kuwapo kwa kasoro hizo CWT ama la, alijibu: “Siwezi kutoa jibu lolote kwa sasa.”

Chama cha Walimu nchini kina jukumu la kutetea masilahi ya walimu na tangu kimesajiliwa hadi sasa kina miaka 25.