Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema katika maoni yaliyochapishwa Jumapili kwamba Ulaya haina nia ya kuchochea mzozo wa Taiwan na inapaswa kuendelea na mkakati huru mbali na Washington na Beijing.

Macron alirejea hivi karibuni akitokea China baada ya ziara ya kiserikali ya siku tatu ambako alipokelewa kwa shangwe na Rais Xi Jinping.

China Jumamosi ilianza mazoezi karibu na Taiwan kwa kukasirishwa na mkutano kati ya Rais wa Taiwan Tsai Ing-Wen na Spika wa Baraza la wawakilishi la Marekani Kevin McCarthy siku ya Jumatano.

China inaiona Taiwan inayojitawala kidemokrasia kama himaya yake na haijawahi kuachana na msimamo wa kutumuia nguvu ili kukifanya kisiwa hicho kuwa chini ya udhibiti wake.

Serikali ya Taiwan inapinga vikali madai ya China.

Macron amesema Ulaya haipaswi kuongeza kasi ya mzozo lakini kuchukua muda ili kuwa na msimamo thabiti kama nguzo ya tatu kati ya China na Marekani, katika maoni aliyotoa kwenye gazeti la Ufaransa Les Echos na Politico wakati wa ziara yake nchini China.

Politico ilimnuku akisema “Jambo baya zaidi ni kufikiria kuwa sisi watu wa Ulaya lazima tuwe wafuasi wa suala hili na tukubaliane na mwenendo wa Marekani na msimamo mkali wa China.”