RAIS wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema atajadiliana na viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya juu ya kuruhusu kutumiwa silaha zake za Nyuklia kuisadia Ukraine.
Katika hotuba yake jana kwa taifa kiongozi Macron pia alizungumzia uwezekano wa kupelekwa wanajeshi wa mataifa hayo nchini Ukraine ili kusimamia makubaliano ya amani.
Alisema “Tunapaswa kuendelea kuwasaidia Waukraine mpaka watakapopata amani thabiti, Urusi ikiwa peke yao na sisi tukiwa pamoja. Hiyo ndiyo sababu njia ya kuelekea amani haipaswi kuhusisha suala la kuiacha peke yake Ukraine. Ni kinyume chake. Amani haiwezi kuhusisha Ukraine kusalimu amri. Haiwezi kuachwa kuporomoka. Na wala haiwezi kumaanisha kufikiwa makubaliano dhaifu ya kusitisha vita.”
Macron amesema Wafaransa wana wasiwasi kuhusu kuanzishwa kwa enzi mpya kufuatia kuingia madarakani kwa Trump nchini Marekani, kutokana na hatua yake ya kubadili sera ya taifa hilo kuelekea Ukraine na kutishia kusababisha mtengano na Ulaya.
Rais Macron amesisitiza kwamba Ulaya haipaswi kukubali kufanyiwa maamuzi na Washington au Moscow, huku pia akimuonya Rais Trump kwamba hakuwezi kuweko makubaliano ya kusitisha vita ambayo ni dhaifu.
