Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imesema nia ya  kuendeleza Mji Mpya wa Kigamboni, ipo palepale.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amesema Wizara imeunda Wakala wa Kusimamia Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni, yaani Kigamboni Development Agency (KDA).

 

KDA ni Mamlaka ya Upangaji (Planning Authority) wa eneo la Mji Mpya Kigamboni lenye kata tisa za Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Mjimwema, Kibada, Somangila, Kisarawe II, Kimbiji na Pemba Mnazi.

 

Waziri Tibaijuka ametoa msimamo huo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2013/2014 bungeni mjini Dodoma, juzi.

 

“Kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kuandaa michoro ya kina inayoonesha miundombinu inayotakiwa kwa ajili ya makazi mbadala katika kata ya Kibada. Kazi ya kupima na kuthamini mali katika maeneo hayo inaendelea kwa kushirikiana na wananchi katika ngazi za Mitaa. Kamati za Mitaa za Wadau zimeundwa na wananchi wenyewe na madiwani wao katika mitaa yote na Baraza la Ushauri la KDA litaanza kazi yake.

 

“Pia, Wizara itaanzisha Mfuko ambao utawezesha wananchi wa Kigamboni kushiriki kama wanahisa katika uendelezaji wa Mji wa Kigamboni. Vilevile, Wizara imeingia makubaliano ya awali (MoU) na kampuni mbili za nje kwa ajili ya kujenga nyumba za makazi mbadala. Kampuni ya Mi World kutoka Dubai – Falme za Kiarabu inatarajiwa kujenga nyumba 5,000 na kampuni ya China Hope Limited kutoka China inatarajia kujenga nyumba 10,000,“ amesema.

 

Ameongeza kuwa wananchi wa Kigamboni watakaolipwa fidia watapewa fursa ya kwanza kununua nyumba hizo  kwa kutumia fidia hiyo moja kwa moja.

 

“Utaratibu huu wa kulipia nyumba mpya kutumia fidia ndiyo unaotambuliwa na Umoja wa Mataifa kama mfano bora wa kuhamisha wananchi. Kumlundikia mtu malipo na kumtegemea ajenge nyumba mpya mwenyewe una upungufu kwa sababu inamaanisha atafute eneo jipya na ajenge. Mchakato huu  hupoteza muda na kusababisha fidia yake kupunguka thamani. Ninachukua fursa hii kuwahimiza wananchi kutoa ushirikiano katika mbinu hizi za kisasa kujiletea maendeleo endelevu,” amesema Profesa Tibaijuka.

 

Waziri huyo amewashukuru wananchi wa Kigamboni kwa ushirikiano wanaoipa Wizara hiyo na kuwahamkikishia kuwa Wizara itaendelea kuwashirikisha katika hatua zote za utekelezaji wa Mpango huo.

 

“Pia ninatambua mchango mkubwa na ushirikiano tuliopata kutoka kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, madiwani na wabunge wanaofuatilia mradi huu wa kihistoria,” amesema.