Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MKUU wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Rose Mdami ametoa wito kwa wakulima nchini kutumia mbinu na teknolojia mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi walizozibuni kwa lengo la kuongeza tija na kukuza sekta ya kilimo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Amesema chuo hicho kimekuwa kikifanya tafiti na kubuni teknolojia mbalimbali ambazo ndio njia pekee ya kuwainua wakulima.

“Kila mwaka tumekuwa tukija na Teknolojia mbalimbali na miongoni mwa teknolojia zinazooneshwa na chuo hiki katika maonesho haya ya Nanenane ni kifaaa cha kulishia samaki kinachotoa taarifa kwa mfugaji kuhusu muda na kiasi cha chakula,” amesema.

Ameongeza kuwa wanahakikisha chuo kinakuwa na mchango katika kuhakikisha mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia yanayotokea duniani yanatumika kuendeleza na kukuza sekta ya kilimo.

Amesema bidhaa nyingi za kilimo wanazoonesha kwenye maonesho hayo zimetokana na tafiti ambazo chuo kinaendelea kufanya na kutolea mfano Mkoa wa Dodoma ambao hauna mvua nyingi kwa kubuni mazao ambayo yanastahimili ukame.

“Tunaamini tukiendelea kufanya hivyo tutazalisha wataalam ambao watakwenda kusaidia jamii ikajifunza kutoka chuo kikuu cha Dodoma tukaendelea kuongeza uzalishaji na wananchi kupenda na kujihusisha na kilimo,” amesema.

Katika maonesho hayo chuo hicho pia kinafanya udahili kwa wahitimu wa kidato cha sita na wale waliomaliza diploma na kuwataka wanaotaka kujiunga kuanzia ngazi ya stashahada, shahada za awali na shashada ya uzamivu kutembelea katika banda la Udom.