Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Lughano Kusiluka, ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana na chuo hicho ili kuweza kutengeneza tiba lishe zitakazosaidia kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Aidha Profesa Kusiluka amewakaribisha Watanzania kwenda kusoma katika chuo hicho kwasababu kila program katika vyuo vingine na UDOM inapatikana.

“Chuo hiki ndicho kilikuwa cha kwanza kutoa Shahada katika lishe tiba na chakula hivyo uzoefu huo umesaidia wataalam kutengeneza vyakula mbalimbali. Hatua tunayofuata ni kutafuta wadau na wabia ili tuweze kutengeneza lishe ambayo ni tiba ili watu waweze kuipata sehemu mbalimbali.

“Tuwakaribishe wajasiriamali au wanyabiashara waje, sisi tunazo formula waje waunganishe nguvu tutengeneze tiba lishe ili magonjwa ya kuambukiza yapungue tunataka kutengeneza Tanzania yenye afya,” amesema.

Ameongeza kuwa UDOM wana uzoefu wa kutosha kwani wamekuwa na wataalamu wanaotengeneza vyakula vya aina mbalimbali.

“Lakini pale chuo tunafundisha ufugaji wa samaki, pia masuala ya Tehama na akili mnemba hivyo tumeamua kuunganisha wataalamu katika maeneo hayo ili uweze kusaidia katika ufugaji wa kisasa zaidi wa samaki. Na yeyote anayekuja kwenye Banda aje ajionee, ushiriki wetu umekuwa mzuri watu wengi wamekuja kujifunza,” amesema.

Kwa mujibu wa Profesa Kusiluka, mafunzo mengine yanayotolewa katika chuo hicho ni ya madaktari, wauguzi, wataalam wa lishe tiba, afya ya jamii nk.

Aidha amesema Tanzania imejitangaza vizuri na ni nchi inayovutia kwa wawekezaji kutokana na juhudi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba wanaunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kuandaa wataalam katika sekta mbalimbali.

“Tunafundisha wataalam katika maeneo mbalimbali kama vile biashara, uchumi, ujasiriamali, masoko na mambo yote yanayohusiana na biashara, lakini biashara katika miaka ya siku hizi ni lazima uwe unajua kuifanya kisomi,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share