Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimesema kuwa kimejielekeza kufanya tafiti zinazotoa majibu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ili kuhakikisha kunakuwa na ustawi kwa Watanzania.
Akizungumza kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson, amesema tafiti hizo zinafanywa na wanafunzi pamoja na wanataaluma.
Amesema mwaka huu katika maonesho hayo wamekuja na bidhaa mpya ya kuwaonesha Watanzania kwa sababu ambazo ni tofauti na za mwaka jana.
“Mwaka huu tumeamua kuja kivingine kuanzia aina za mashine ambazo zinasaidia katika sekta ya samaki. Lakini wanafunzi wetu wameingia katika uwanja wa kutengeneza ‘rockets’ na kwenye maeneo ya vyakula ili kutibu maradhi mbalimbali kwa kutumia lishe asili.
“Udom inajipambanua kwa kuangalia matatizo ya jamii ya Watanzania na kutumia akili za wanafunzi na wafanyakazi wake kuangalia namna ya kuzitatua hasa katika eneo la afya, teknolojia na ukija Sabasaba utaziona,” amesema Profesa Wineaster.
Amesema bidhaa hizo ambazo zimetengenezwa na wanafunzi mbalimbali wa chuo hicho zinatokana na tafiti walizofanya pamoja na wanataaluma na kusisitiza ndizo zinazowezesha kuwepo kwa teknolojia mpya.
“Bila tafiti huwezi kuja na tekolojia mpya, huwezi kuja na ubunifu wowote kwahiyo tumejipambanua katika eneo hilo, licha ya kuwepo kwa changamoto ya rasilimali fedha kweye tafiti lakini tunaendelea kujitahidi katika eneo hilo…kikubwa tafiti zetu zimejikita katika jamii ya Watanzania na kutatua matatizo yaliyoko katika jamii yetu Tanzania,” amesema.
Profesa Wineaster amesema hivi sasa wanajielekeza kutoa mafunzo ya amali ambayo mwanafunzi yeyote katika chuo hicho anafunzwa kwa vitendo na darasani ili akimaliza masomo akatengeneze ajira badala ya kutafuta ajira.
Aidha amesema wanatarajia kufungua kampasi mpya mkoani Njombe itakayoanza kutoa mafunzo Septemba 2026 ambayo itajikita katika sekta zilizoko mkoani humo kama misitu, madini, uvuvi na nyingine.
Kwa mujibu wa Profesa Wineaster, ujenzi wa kampasi hiyo utatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na kwamba hivi sasa wako katika hatua za manunuzi.