Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimepata tuzo ya mshindi wa kwanza katika kipengele cha Taasisi za elimu ya juu katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.
Akizungumzia ushindi huo leo Julai
13,2024 jijini Dar es Salaam katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Shahada za awali UDOM, Dk.Victor Marealle amesema hiyo ni ishara ya kutambulika kwa kazi wanazozifanya Chuo hicho.
“Jambo hili kwetu ni la furaha sana, na tunamshukuru Mungu. Katika maonesho haya tulikuja na bunifu mbalimbali za kiteknolojia ambazo zimefanywa na wanafunzi wetu…hii yote ni matunda yanayotokana na ufundishaji wetu,” amesema.
Amefafanua kuwa wanapowafundisha wanafunzi hao wanatumia vitendo ambavyo vinazalisha bidhaa hizo na kwamba hilo ni chimbuko la tafiti ambazo zinafanywa na wanafunzi hao kwa kushirikiana na wahadhiri wao.
“Tuzo hii kwa kweli kwetu ni chachu kama Chuo kikuu cha Dodoma kuzidi kupambana zaidi, si tu kuboresha bidhaa ambazo tumezileta lakini kutatua matatizo kwa ujumla ambayo yanaizunguka nchi yetu na kuendeleza tafiti mbalimbali,” amesema.
Akizungumzia changamoto za vyuo vikuu vya elimu ya juu amesema kuwa vyuo hivyo vimekuwa vikipewa changamoto ambapo tafiti zake nyingi zinawekwa katika lugha ya kiingereza na kutumwa katika majarida ya nje na hazitumiki hapa nchini.
“Sisi tunakuja tofauti kidogo tunakuja na tafiti ambazo wanashirikiana na tasnia hii moja kwa moja, tunatafiti kwanza mahitaji ya ndani na nje halafu tunatengeneza programu ambazo zinakwenda kufiti tasnia inayotuzunguka,” amesema.
Ameongeza kuwa hata tafiti wanazozifanya zinaendana na matokeo ya moja kwa moja kwenye Sayansi, huku akisema katika maonesho hayo wamekuja na baadhi ya bunifu ambazo wamezigeuza na kuwa bidhaa zinazoingia sokoni.
Marealle ambaye pia alikuwa msimamizi wa banda katika maonesho hayo, amesema kuwa UDOM hawataki tafiti zao ziishie kwenye makaratasi bali zikasaidie matatizo halisi katika jamii.
Aidha amewakaribisha wanafunzi waliomaliza kidato cha sita ambao wanasifa stahiki za kujiunga na programu mbalimbali huku akisema UDOM wanashahada za awali hadi za uzamivu.