Bandari ya Dar es Salaam ni mashuhuri katika nchi za Afrika Mashariki na Kati. Bandari hii, kwa muda mrefu, imekuwa kitovu cha biashara kati ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Kati zisizokuwa na bandari (land locked).

Pia Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikitumika kama daraja au kituo maalumu kwa kusafirisha na kupokea bidhaa mbalimbali za nchi za jirani, ama kutoka kwenye nchi hizo kwenda nchi za jirani, au kutoka nchi tofauti duniani kwenda nchi hizi za jirani.

 

Serikali imekuwa ikijipatia mapato makubwa kutokana na ushuru unaotokana na matumizi ya Bandari yetu ya Dar es Salaam, na imeweza kutengeneza ajira nyingi za moja kwa moja, au zile zinazohusiana na shughuli zote za bandari.


Pamoja na umuhimu wa bandari hii kwa Tanzania na nchi zote zinazoitumia, lakini imeingiwa na dosari ya vitendo vya udokozi wa vifaa mbalimbali vinavyopitia hapa nchini.


Tatizo hili linazidi kutuongezea umaskini kwa vile baadhi ya wateja waliokuwa wanaitumia bandari hii, wameanza kuihama na kuanza kupitishia mizigo yao ama Mombasa, Kenya, au Durban, Afrika Kusini, jambo linalotunyang’anya mapato, kazi zetu, uzoefu na heshima mbele ya majirani zetu! Na udokozi huu si wa vitu vikubwa sana, hapana, bali ni wa vitu vidogovidogo.

 

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amefanya kazi kubwa ya kuirudisha Bandari ya Dar es Salaam katika taratibu zinazokubalika kimataifa, lakini bado kuna watu wanaompiga vita chini kwa chini asifanikiwe kuiweka bandari yetu katika mazingira yanayokubalika.


Dk. Mwakyembe ni kiongozi wa pekee tangu nchi hii ipate Uhuru ambaye ameweza kuweka nidhamu ya hali ya juu katika bandari yetu; pamoja na juhudi zake zote hizo lakini kuna kikundi cha watu ambao bado wanaendeleza tabia za udokozi chini kwa chini, na vitendo hivi vinaendelea kuiweka bandari yetu katika orodha ya bandari hatari duniani!


Naiomba Serikali imsaidie Dk. Mwakyembe kwa hali na mali aweze kupambana na wahalifu hao wanaolinyima Taifa letu mapato, na pia kuwanyang’anya Watanzania nafasi za kazi. Serikali ikifanya hivyo itarudisha imani kwa wafanyabiashara mbalimbali wa nchi za jirani ambao wameshaanza kuzitumia bandari za Durban na Mombasa badala ya Dar es Salaam.

0782 000 131