*Tangazo la wabunge Waislamu kukutana lavuruga

*Wakristo waandaa muswada wa Amri 10 za Mungu

NA MWANDISHI WETU

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekumbwa na mgawanyiko wa chini kwa chini wa udini.
  Hali hiyo ilitojitokeza Alhamisi iliyopita ambako Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, alitoa tangazo lenye kuashiria mgawanyiko wa kidini hasa wakati huu wa mjadala wa Mahakama ya Kadhi.


  Siku hiyo wakati anaahirisha kikao cha asubuhi, Zungu alitangaza kuwapo kwa mkutano wa wabunge wote wa dini ya Kiislamu uliopangwa kufanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa.
  Kutokana na tangazo hilo lililosomwa wakati wa matangazo ya shughuli za Bunge, wabunge walishtushwa na tangazo hilo, na baada ya kutoka katika ukumbi huo wa Bunge walikaa katika vikundi vidogo vidogo wakijadili tangazo hilo.


  JAMHURI lilishuhudia baadhi ya wabunge wakimshutumu Zungu kuruhusu kusomwa kwa tangazo hilo ambalo katika historia ya Bunge hilo hakujawahi kutokea jambo hilo.
  Akizungumzia tangazo hilo, Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mchungaji Luckson Mwanjale, anasema kuwa wengi wao walipatwa na mshtuko kuona uhamasishaji huo unafanywa na Kiti cha Spika, jambo ambalo ni hatari kwa nchi.
  Anasema kuwa kutolewa kwa tangazo hilo kunazidi kuhamasisha mgawanyiko wa kidini na kuongeza: “Mwenyekiti wa Bunge alipashwa kutafakari kabla ya kutangaza kutokana na hali halisi ya nchi.


  “Huu ni mwanzo wa mgawanyiko wa ndani na nje ya Bunge, nimepata meseji nyingi kutoka kwa watu mbalimbali. Ni vizuri Serikali iweze kuliangalia hilo mapema, ni vyema ikakutana na viongozi wote wa dini  ili kuweza kuweka mambo sawa, tunakoelekea si kuzuri kama nchi,” anasema.
  Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, anasema kuwa tangazo hilo limewachefua baadhi ya wabunge kwani baada ya kutolewa alisimama kuomba mwongozo wa Kiti apate ufafanuzi kuhusiana na kutolewa kwake ndani ya Bunge lakini alinyimwa fursa hiyo.
 Lusinde alieleza kuwa ni hatari kwa Bunge linalotegemewa kuanza kuonesha mgawanyiko wa waziwazi wakati huu ambao kuna mvutano kuhusiana na Mahakama ya Kadhi huku viongozi wa dini wakitoa matamko ya mara kwa mara.


  Moses Machali, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), anasema Serikali na Bunge ni lazima kuheshimu misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo inabainisha kutokuwa na dini.
 “Tatizo baadhi ya viongozi wa Serikali kwa sababu ya malengo yao binafsi wamekuwa wakitoa maelekezo yenye kuleta mgawanyiko,” anasema Machali.
 Anasema ipo changamoto iliyojitokeza na viongozi wanalo jukumu la kuiangalia kwa umakini Mahakama ya kadhi.
  Chama Cha Mapinduzi katika ilani yake ya mwaka 2005 kilitoa ahadi ya upatikanaji wa Mahakama ya Kadhi wakati huo wakijua fika kuwa Serikali haina dini.


  Mnamo mwaka 2007  waumini wa dini ya Kikristo  mkoani Tanga kutoka madhehebu ya Kilutheri waliwahi kuiambia Serikali ianzishe Mahakama ya Amri Kumi za Mungu, na mwaka 2011 Katoliki nao waliwahi kudai Mahakama ya Kikatoliki.
 Habari lililozipata Gazeti JAMHURI zinasema kundi la wanasheria Wakatoliki wakishirikiana na baadhi ya mapadre wamekutana mara nne jijini Dar es Salaam ndani ya mwezi huu kujadili hoja ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kanisa rasmi.


  “Ni kweli wamekutana, ingawa Biblia inasema ukipigwa shavu la kulia geuza la kushoto, hapa tunatafuta ufumbuzi wa kisayansi usio wa kupigana. Kama wanaona inawafaa Mahakama ya Kadhi, basi tunaanzisha Mahakama ya Kanisa na sisi, hiyo ya Serikali iende likizo,” amesema mtoa habari wetu.
 “Nchi hii tunaipeleka wapi? Misingi ya Katiba inavunjwa, suala la Mahakama ya Kadhi limetibua Wakristo, busara ya kawaida ni lazima kutumika ili hayo yasiendelee, Serikali ni lazima iachane na suala la Mahakama ya Kadhi kuingizwa katika mchakato wa kiserikali.    Ikumbukwe Rais Jakaya Kikwete aliwahi kueleza ukweli kuwa suala hili liendeshwe kwa misingi ya kidini si vinginevyo,” anasema Lusinde.
  “Nafikiri Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati wa Bunge la Katiba alipoahidi Mahakama ya Kadhi  alikuwa na dhamira yake binafsi, maana anajua kuwa haitekelezeki lakini alisema kitu wanachotaka kukisikia. Kuheshimiana kumeanza kutoweka maana kuna viongozi wanakosa busara,” anasema.
  Mnidhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, kwa upande wake anasema hadhani kama ni sahihi kwa tangazo hilo kusomwa bungeni ila Spika wa Bunge, Anne Makinda, amekuwa akitangaza mara kwa mara ibada za  Wakatoliki, jambo ambalo si sahihi pia.


  “Haiwezekani ikawa mbaya Waislamu wakitangaziana wakutane, ni makosa kweli, ila Spika amekuwa akifanya matangazo kwa kutumia kiti chake. Hili Bunge si la kidini, haliwezi kutumika kualikana katika mazungumzo ya kidini. Kwa sababu yoyote ile ukishaanza kufanya mambo yasiyokuwa sawa sawa, hizi dalili si nzuri kwa nchi maana wameanza kuleta ugomvi wa kidini nchini,” anasema Lissu.  
  Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo, alisema kuwa hali ni mbaya Taifa linagawanywa vipande vipande maana baada ya tangazo hilo baadhi ya wabunge walitaka kuitisha mkutano wa Wakristo huku wengine wakitaka kuitisha mkutano wa wapagani, jambo ambalo ni hatari kwa nchi katika kipindi hiki.
  “Nchi yetu inakumbwa na hali ya hatari, Taifa linapoelekea ni kubaya sana, tunaligawa Taifa vipande vipande,” anasema.
  Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, anasema kuwa alishtushwa na tangazo hilo kutolewa katika kikao cha Bunge, akidai jambo si sahihi maana wabunge wamekuwa wakikutana katika Kamati za Bunge, semina mbalimbali lakini si mkutano wa wabunge wote wa dini fulani.
“Nchi ni kama haina mwenyewe, hali sasa inaanza kuwa mbaya,” anasema Mdee.


  Hata hivyo, mmoja wa wabunge aliyetaka kutangaza kikao cha Wakristo bungeni, ameiambia JAMHURI kuwa tangu kusomwa kwa tangazo hilo bungeni kumekuwa na minong’ono mingi miongoni mwa wabunge huku baadhi yao wakimuomba kuitisha kikao cha wabunge Wakristo.
 Anaeleza kuwa si jambo sahihi kutolewa matangazo ya namna hiyo katika Ukumbi wa Bunge ingawa wamekuwa wakiitana na kukutana katika ibada, mambo ambayo yanaeleweka kwa wabunge wote.
  “Kuitishwa kwa mkutano au kikao cha wabunge wote Waislamu si sahihi, na tetesi zilizopo ni ajenda ya Mahakama ya Kadhi na kuweka msimamo jambo ambalo si sahihi.


  “Huu siyo utamaduni mzuri tunaouanzisha. Tukiamua kuruhusu mikutano ya kidini katika Bunge kutakuwa hakuna tena Bunge, ndiyo maana nilipoombwa kufanya hivyo nilikataa maana niliwauliza ajenda yao ni nini hasa?” Anahoji.
  “Kutokana na msukumo huo inaonekana kilichotokea baadhi ya wabunge wamechukizwa, maana ni jambo ambalo halijawahi kutokea katika uhai wa Bunge hili,” anasema.
  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mkuchika, anasema suala hilo si jambo la ajabu na hakuna sheria inayozuia kuwapo kwa matangazo ya aina hiyo bungeni.


  Baadhi ya wabunge ambao hawakuwa tayari kutajwa majina walisema si busara kwa kiongozi yeyote kutoa tangazo la namna hiyo katika Bunge la Jamhuri kutokana na kwamba si Watanzania wote walio na dini, kwani wapo pia wapagani.
  Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage, anasema kuwa mkutano huo haukufanyika Alhamisi iliyopita kama ilivyopangwa kutokana na kutopata nafasi katika Ukumbi wa Msekwa na ukafanyika Ijumaa iliyopita.
  Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Msekwa kama ulivyoitishwa, ila katika hali isiyokuwa ya kawaida hakuna mbunge hata mmoja aliyekuwa tayari kuzungumza yaliyojiri katika mkutano huo.