*Serikali yapiga marufuku mitihani Ijumaa, J’mosi

*Wizara yatoa waraka maalumu, ni ushauri wa AG

*Profes Bana, Joseph Selasini waonyesha hofu zao

 

 

Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imezuia uongozi wa vyuo vikuu nchini kuwalazimisha wanafunzi kuingia darasani au kufanya mitihani kwa siku zao za ibada.

Ingawa hazikutajwa, siku maalum za ibada zilizozoeleka kwa madhehebu mengi ni Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

Agizo la Serikali limetolewa na C.P. Mgimba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Barua hiyo ya Novemba 11, mwaka huu yenye kicha cha habari: “Wanafunzi kulazimishwa kuingia darasani au kufanya mitihani siku za ibada”, imepelekwa kwa Makamu Wakuu wa Vyuo, Wakuu wa Vyuo Vikuu Vishiriki; Wakuu wa Vyuo- Vyuo Vikuu na Vyuo Vishiriki vya Umma na Binafsi, Tanzania Bara.

Inasema: “Wizara imepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya viongozi wa dini na wanafunzi kuhusu kuingiliwa kwa uhuru wa kuabudu kwa kulazimisha wanafunzi kuhudhuria mihadhara au kufanya mitihani siku za kuabudu kinyume na imani zao za dini.

“Ikumbukwe kuwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania masuala ya haki ya imani za dini yamewekewa ulinzi katika Ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Kitendo cha wanafunzi kulazimishwa kuhudhuria mihadhara au kufanya mitihani siku za ibada kinyume na imani za dini zao ni kwenda kinyume na haki za msingi kama ilivyowekwa katika Ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

“Tukio kama hilo liliwahi kutokea kwenye chuo kimojawapo ambapo mwanafunzi alizuiliwa kufanya mitihani ya Wizara kutokana na kutofanya baadhi ya mitihani ya chuo kwa kuwa mitihani hiyo ilipangwa kufanyika siku ya Jumamosi kinyume na imani ya dini yake na hivyo kulazimishwa kuahirisha masomo yake.

“Kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusiana na suala hili, mnaelekezwa kuheshimu na kufuata misingi na haki ya kikatiba kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.”

Ibara ya 19 inayotajwa kwenye barua hiyo kifungu cha (1) inasema: Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.

(2): Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni uhuru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli na uendeshaji jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.

(3) Hifadhi ya haki zilizotajwa katika ibara hii itakuwa chini ya taratibu zilizowekwa na sheria ambazo ni muhimu katika jamii ya kidemokrasia kwa ajili ya usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii na umoja wa kitaifa.

(4) Kila palipotajwa neno “dini” katika Ibara hii ifahamike kwamba maana yake ni pamoja na madhehebu ya dini na maneno mengineyo yanayofanana au kuambatana na neno hilo nayo yatatafsiriwa kwa maana hiyo.

 

Maoni ya Profesa Bana, Joseph Selasini

 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana, amezungumza na Gazeti la JAMHURI na kupinga utaratibu wa Serikali kuingilia au kuamuru vyuo kutekeleza mpango huo.

Profesa Bana anasema: “Vyuo vina taratibu zake, kwa mfano wakati wa mitihani mwanafunzi anayekuja na hijab anaombwa aivue na aonyeshe kitambulisho ili kuhakikisha kuwa ni yeye kweli. Akimaliza hilo anavaa hijab na kuendelea na mitihani. Ndio utaratibu. Mimi wanafunzi wangu siku za Ijumaa na Jumamosi siwezi kuwakatalia kwenda kuabudu. Hili si suala la Serikali kutoa waraka – ni la mwafaka kati ya mwalimu na mwanafunzi.

“Wanafunzi wa vyuo vikuu ni watu wazima, pengine vyuo vikuu vimekuwa vingi – vyuo vya serikali, vyuo vya kidini, ndiyo maana Serikali imekuja na waraka huu. Mimi nashauri waache vyuo vyenyewe vijipange kwa sababu mambo yote vyuoni ni shirikishi.”

Mhadhiri huyo ambaye amekuwa mwalimu kwa miaka 38, anasema uamuzi wa Serikali kutoa waraka unaweza kuamsha makundi mengine kudai siku za mapumziko.

“Haya mambo yanaweza kuibua hisia za makundi kama ya Waislamu wenye msimamo mikali kuibuka na kudai Ijumaa isiwe siku ya kazi. Watataka wapumzike kama wenzao wanaopumzika Jumapili, ndio maana nasema hili jambo halipaswi kuingiliwa na Serikali, liachwe walimu na wanafunzi wenyewe waone namna ya kulitekeleza.”

Ameongeza: “Mambo kama haya yapo Zanzibar ambako Ijumaa muda wa ibada ukifika ukiwa darasani utabaki peke yako. Wote wanakwenda kuswali. Hakuna waraka, lakini ni utaratibu uliopo. Hapa naona Serikali inachokoza jambo ambalo tayari lina utamaduni wake. Unapotoa mwongozo maana yake nao wengine wadai. Kinachotakiwa ni kutoa waraka unaozingatia sheria za nchi halafu hayo mengine unayaacha kama yalivyo yashughulikiwe na pande husika.”

Profesa Bana anasema Serikali makini hutoa mwongozo wa jumla kwa kuzingatia katiba na sheria.

“Mbona miaka 10 iliyopita haya mambo hayakuwapo? Sina kumbukumbu za Waislamu kudai jambo hili. Ukichokonoa wengine nao watadai, uki-base kwenye sheria ukakosa… utapata shida. Serikali ifanye mambo ya jumla. Iseme ‘heshimuni sheria, katiba, imani za watu; basi’. Ningekuwa mimi ningetoa mwongozo wenye sentesi mbili tu.

“Watanzania tunaishi kwa undugu, mshikamano kwa hiyo kufanya uamuzi kunapaswa kuzingatia sheria na Katiba. Kinachofanywa sasa ni kutoa jini kwenye chupa,” anasema.

Profesa Bana anasema tukio moja haliwezi kuwa la Tanzania nzima. “Nimefundisha kwa miaka mingi, kule Bukoba siku senene wanatoka wanafunzi wote concentration darasani hakuna. Mwalimu unachofanya unawaacha, unatafuta muda au siku nzuri ya kufidia masomo. Au kukiwa na msiba ukisema uwafundishe utakuwa unajidanganya. Sasa haya unayafanya si kwa sababu ya waraka, bali ni kwa mwalimu kupanga na wanafunzi. Unachoweza kufanya ni kuomba kibali cha Mkuu wa Idara ili uweze ku-cover kwa muda uliopangwa.”

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), anaunga mkono uamuzi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kusema kwa mujibu wa Katiba, nchi yetu haina dini.

“Huwezi kulazimisha au kupanga mitihani au shughuli ya jumla ambayo unajua huwezi kupata watu wote,” anasema.

Mbunge huyo ambaye ni mmoja wa viongozi wa utume katika Kanisa Katoliki, anasema haki ya kuabudu ni ya kila Mtanzania, na kwamba hata siku ya Jumapili inapendekezwa isiwe siku ya uchaguzi (Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu).

“Jumapili kuwa siku ya Uchaguzi kumesababisha wapigakura wapungue kwa sababu wengi wanakwenda kuabudu siku hiyo. Ijumaa na Jumamosi ni siku za kuabudu. Ukiwazuia hao kuzitumia siku hizo na wao wanaweza kusema Jumapili iwe siku ya kawaida ya kazi.

“Jamii imeharibika kwa ukosefu wa maadili, sehemu pekee inayoweza kusaidia kurejesha maadili ni dini. Kuwafanya vijana wasishiriki siku za ibada tutakuwa tunakosea,” anasema.

Alipoulizwa kama waumini wanaoabudu Ijumaa wanaweza kudai siku hiyo iwe ya mapumziko kama ilivyo Jumapili, Selasini anasema: “Mimi nimesoma Kuran. Wakifanya hivyo watakuwa wamekosea kwa sababu Mtume aliamuru Waislamu siku ya ibada washiriki ibada kisha watafute riziki. Kutafuta riziki ni kufanya kazi. Wakiamua Ijumaa wasiende kazini huo utakuwa ukorofi ambao naamini Waislamu hawana kabisa.”

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama, alipotafutwa kwa simu, alipokea lakini akasema yuko katika kikao.

Baadaye, kupitia kwa msaidizi wake, akatoa maelezo kwa Gazeti la Jamhuri kuwasiliana na Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa. Hadi tunakwenda mitamboni hatukufanikiwa kuzungumza naye.