Katika sehemu hii ya tano na ya mwisho, Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna, anahitimisha makala yake ya awali kuhusu udini na athari zake nchini Tanzania. Maudhui kwenye makala haya ni kuwasihi Watanzania wote, bila kujali jinsi, hali, rangi na tofauti zozote zile, kuungana katika kukabiliana na hatari ya udini inayolinyemelea Taifa letu kwa kasi.
Amejitahidi kueleza namna Watanzania wa imani zote walivyoshirikiana kwenye masuala mbalimbali ya kijamii na kitaifa bila kujali imani zao. Brigedia Jenerali mstaafu Mbenna anasisitiza katika umoja wa Watanzania na binadamu wote, na umuhimu wa kuvumiliana. Endelea…
Jumapili ya Februari 17, 2013 majira ya asubuhi kule Zanzibar lilitokea jambo la kutisha na kustaajabisha sana. Vyombo vyote vya habari — radio, runinga na magazeti hata SMS (ujumbe mfupi wa maandishi) katika simu zetu za mikono — ilitangazwa kuwa Padri Evarist Mushi, Paroko wa Kanisa la Minara miwili, mjini Zanzibari, Kathedrali la Askofu, amepigwa risasi tatu kichwani na kufariki dunia.
Huyu Padri alikuwa anajiandaa kwenda kutoa sadaka ya misa katika Kigango cha Mt. Theresia Mtoni, Jumapili ya kwanza ya Kwaresima.
Tukio la namna hii linatokeaje Jumapili, siku ya ibada kwa Wakristu? Serikali ya Tanzania imejigamba ni nchi isiyokuwa na dini lakini wananchi wake wana imani za dini tofauti tofauti — Ukristo, Uislamu na imani kiasili (upagani). Padri anakwenda kuendesha ibada ya imani yake kwa waamini wake wa Katoliki ghafla tu maisha yake yanaondolewa. Hao waliotenda unyama huo ni kina nani na wa imani gani? Nchi kama Pakistan au Iran zinajulikana waumini wa Shia na Sunni wanapambana hata kuuana. Lakini hapa Tanzania nchi yenye Serikali isiyofungamana na dini yoyote, tukio namna hii linatisha na linashangaza.
Kule Visiwani, viliwahi kutolewa vipeperushi na wafuasi wa dini moja kutishia amani Wakristo. Vipi Serikali haikuweza kujiandaa kwa tukio namna hii (not prepared or aware of such an eventuality?)
Vipeperushi vile viliashiria mvunjiko wa amani na pia viliashiria kuwapo kwa kundi la wahalifu katika nchi. Utayari wa Serikali hasa vyombo vya ulinzi na usalama ukoje Visiwani kukabiliana na uhalifu huo wa kutisha kwa viongozi wa dini?
Kuna shehe alimwagiwa tindikali, kuna Padri Mkatoliki alipigwa risasi siku zilizopita. Hao hawakufariki dunia! Kuna makanisa yalichomwa moto. Leo hii Padri, kiongozi wa dini kapigwa risasi na kufa.
Matukio ya aina hii yanaashiria hali hatarishi sana Visiwani na nchini Tanzania. Ulinzi shirikishi wa polisi uko wapi hapo? Nani alaumiwe? Wasiwasi namna hii unaota mizizi katika Taifa hili hata raia hawawezi kuishi kwa amani. Wakristu hawana moyo au tabia ya kisasi hata kidogo. Katika Biblia tunasoma juu ya upendo kwa adui maneno haya:-
“Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia, wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wanawachukia ninyi, wabarikini wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wanawaonea ninyi….” (Lk 6:27 – 28).
Basi, tunaombea AMANI katika nchi yetu ili tuishi kwa upendo na tulijenge Taifa letu. Serikali itakuja na tamko rasmi juu ya yote haya. Mungu ibariki Tanzania.