Miaka kadhaa iliyopita, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam hawakuwa na uhakika wa kusafiri salama kutoka eneo moja kwenda jingine.

Hali hiyo ilichochewa na uhaba wa huduma za usafiri wa umma na za kiwango cha chini tofauti na majiji mengine kwenye mataifa mbalimbali barani Afrika, Ulaya na Marekani.

Zilifanyika juhudi nyingi za wadau mbalimbali kuanzia Serikali na watu binafsi katika kile kilichoonekana kutaka kukomesha kabisa tatizo la usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam hususan wanafunzi.

Hata hivyo, juhudi hizo ziligonga mwamba kama siyo kushindwa. Miongoni mwa watu walioathiriwa zaidi na tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam ni wanafunzi.Tatizo  hilo liliathiri sana hata uwezo wao kitaaluma.

Itakumbukwa visa lukuki vya makondakta kunyanyasa na kuwanyanyapaa wanafunzi ambao baadhi yao waliathirika kisaikolojia na hata kujeruhiwa au kufa kwa kusukumwa chini na makondakta, ambao hawakutaka wanafunzi wapande magari yao.

Wakati huo vyombo mbalimbali vya habari nchini viliripoti matukio mbalimbali ya wanafunzi kukumbana na unyanyasaji huo uliowafanya baadhi yao kuchukia shule, na wengine kujiingiza kwenye mahusiano ya kingono na makondakta kwa lengo la kupata upendeleo wa usafiri wa kwenda na kurudi shuleni.

Itakumbukwa wakati huo kabla ya ujio mpya wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa mara ya pili chini ya kampuni ya Simon Group, wanafunzi walifika shuleni kwa kuchelewa kwa sababu ya adha ya usafiri na kurudi nyumbani majira ya kuanzia saa 3 usiku ilikuwa jambo la kawaida.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Bwire Manyama, mzazi wa mwanafunzi Nyakwesi Bwire, anasema kuwa ujio wa UDA umebadili hali ya mambo na kuleta mapinduzi ya kweli ya sekta ya elimu kwa wanafunzi  wa Dar es Salaam, kwa kuwawezesha kupata usafiri wa kwenda shuleni na kurudi majumbani kwao salama bila kubughudhiwa wala kubaguliwa kama ilivyokuwa zamani.

Anasema hivi sasa mtoto wake  ana uhakika wa kuwahi vipindi vyake shuleni na kurudi nyumbani  salama na mapema, tofauti na ilivyokuwa  awali kabla ya ujio wa UDA chini ya mwekezaji mzalendo Kampuni ya Simon Group.

“Zamani mtoto wangu  alikuwa akinyanyaswa sana na makondakta, lakini sasa ana uhakika wa kufika shuleni na kuwahi masomo yake kwa kupanda mabasi ya UDA ambayo mimi mwenyewe nimeshuhudia wanafunzi wakibembelezwa kupanda kwa lengo la kuwahi shuleni na hata kurudi nyumbani,” anasema Manyama.

Athumani Haruna, ambaye mtoto wake anasoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Kinondoni, anasema Shirika la UDA limejizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa wakazi wa jiji kutokana na sababu kadha wa kadha zikiwamo za kutonyanyasa wanafunzi ambao Taifa linaamini kuwa ni viongozi wa kesho wa nchi hii.

Haruna anasema “Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni,  UDA wameleta mapinduzi ya usafiri wa umma katika jiji la Dar es Salaam, ikiwamo kutambua umuhimu wa wanafunzi kwa maendeleo ya nchi yetu kwa kuwachukua vituoni bila manyanyaso ya aina yoyote,” anasema na kuongeza:

“Pia UDA imekuwa kimbilio la wanafunzi kwani wawapo ndani ya magari hayo wanafunzi hawanyanyaswi kama kwenye magari mengine, wana uhakika wa kufika shuleni mapema na kuwahi vipindi, hii si tu inaleta faraja lakini pia wanafunzi wana uhakika wa kuwahi masomo shuleni, kusoma kwa furaha na kufaulu vuzuri mitihani yao.”

“Aidha mimi mtoto wangu hivi sasa anawahi kufika nyumbani na sisikii tena suala la yeye kulalamika kuwa amegombana na kondakta katika suala la usafiri, mwalimu wake anayemsimamia kitaaluma na kinidhamu ananiambia hivi sasa anawahi kufika shule na anaamka saa 12 asubuhi, tofauti na awali alikuwa akiamka saa 10 alfajiri na bado anachelewa kufika shule, kwani wakati mwingine anakaa kituoni hadi saa 2:30 hadi saa 3 asubuhi,” anasema Haruna.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, mwanafunzi Yasinta Paul anayesoma kidato cha tano, anasema kuwa hapo awali wanafunzi wengi  walikuwa hawana uhakika wa kufika majumbani kwao mapema  nyakati za jioni na hata mashuleni, lakini hali hiyo sasa imebadilika na wanafunzi wanawahi shuleni na hata majumbani.

“Mimi nilishuhudia dada na kaka zangu wakati wanasoma walikuwa wakifika nyumbani usiku mnene kutoka shuleni na kubwa walilokuwa wakilizungumza ni adha ya usafiri kwao wa kwenda na kurudi shuleni, lakini hivi sasa hali ni tofauti, tunapenda kuwaomba UDA waendelee na moyo huo na isiwe nguvu ya soda,” anasema Yasinta.

Naye Mwalimu wa Shule ya Mbagala Maji Matitu, Jacob Edward, anasema hivi sasa mahudhurio ya wanafunzi kuwahi yanaridhisha tofauti na awali, na hata mwenendo wao kitaaluma ni mzuri na kwamba zile kesi za wanafunzi kuwa na mahusiano ya kingono na makondakta na madereva wa daladala hazisikiki tena kutokana na UDA kuthamini wanafunzi kuwa ni taifa la kesho.

“Ukweli lazima uzungumzwe, UDA imepunguza kama siyo kumaliza kabisa kesi mbalimbali tulizokuwa tunasumbuka nazo kuzitatua kila kukicha, za makondakta na madereva kuwa na uhusiano wa kingono na wanafunzi, hivi sasa hatusikii mwanafunzi akisema kachelewa kwa sababu ya kunyanyaswa katika usafiri, kwanza wengi wao vituoni husubiri UDA kwa madai kuwa ndiyo usafiri wao wa sasa unaowathamini,” anasema Edward.