Serikali imeanza taratibu za kufufua kesi ya ufisadi wa uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) ambalo ni mali ya umma.
Vyanzo vya habari vya uhakika vimelithibitishia JAMHURI kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tayari imeshaanza kufuatilia Shirika hilo ambalo uuzwaji wake unatajwa kugubikwa na rushwa ya hali ya juu.
Duru za uchunguzi zinaonyesha kuwa hata kufutwa kwa kesi iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Iddi Simba na wenzake; waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, nako kumeanza kufuatiliwa.
Chanzo chetu kimesema: “Haitashangaza kusikia muda wowote Simba na wenzake wakifunguliwa mashitaka upya.”
Simba aliwekewa Sh milioni 320 kwenye akaunti yake binafsi kutoka kwa mnunuzi wa UDA ambaye ni kampuni ya Simon Group. Kampuni hiyo imekuwa ikitajwa kuwa karibu mno na familia ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, lakini mara zote familia hiyo na mmiliki wa Simon Group wamekanusha tuhuma hizo.
Mwaka 2011 Waziri Mkuu alimuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalum juu ya taratibu zilizotumika wakati wa uuzwaji wa hisa za UDA kwa mnunuzi wa hisa hizo na pia kufanya ukaguzi maalumu wa Menejimenti ya UDA.
Ukaguzi ulifanyika kutokana na maswali yaliyoibuka kwenye kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julai, 2011 kuhusiana na uuzwaji wa hisa za Serikali zilizokuwa katika UDA na uuzwaji wa hisa ambazo zilikuwa bado hazijatengwa kwa mwekezaji.
Uuzwaji wa Hisa za UDA:
UDA ni Shirika ambalo lilitengwa kwa ajili ya ubinafsishaji (specified) chini ya usimamizi wa Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC) ambalo lina jukumu la kuyaunda upya mashirika ya aina hiyo.
Kwa mantiki hiyo, CHC ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kuidhinisha uuzaji wa hisa za UDA na siyo Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kama ilivyofanyika.
Julai, 2010 CHC iliishauri Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kupata idhini ya Serikali kabla ya kuendelea na uuzaji wa hisa za UDA.
Imethibitika kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa UDA iliendelea na uuzaji wa hiza hizo bila kupata kibali cha Serikali. Shirika Hodhi la Mali za Serikali lilitoa ushauri kwa Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kuwa njia ya wazi itumike kulingana na Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kumpata mwekezaji bora katika Shirika la UDA.
Habari kutoka serikalini zinasema Bodi ya Wakurugenzi wa UDA ilipuuza ushauri huo na kuendelea na uuzaji huo wa hisa za UDA kwa anayedaiwa kuwa mmiliki wa UDA bila kufuata taratibu za ushindani wa zabuni kama Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.21 ya mwaka 2004 inavyotaka.
Hisa za Shirika la UDA zilithaminishwa na kuwa Sh 744.79 kwa kila hisa Oktoba, 2009. Novemba, 2010 thamani ya kila hisa ikawa Sh 656.15.
Hata hivyo, katika uuzaji huo, Bodi ya Wakurugenzi ya UDA ilitoa punguzo la asilimia 60 kwa kila hisa kwa mwekezaji huyo (kwa tathimini ya bei ya hisa ya Oktoba, 2009), bila kuwapo sababu za kufanya hivyo.
Kwa hiyo kila hisa ilitakiwa kuuzwa kwa Sh 298 kutoka Sh 744.79 kwa hisa moja ambayo ilithaminishwa Oktoba 2009. Hatua hiyo iliifanya UDA ipate hasara ya Sh bilioni 1.559.
Vilevile imebainika kuwa Bodi ya UDA iliingia mkataba wa kumuuzia mwekezaji hisa 7,880,303 ambazo hazikugawiwa kwa bei ya Sh 145 kwa jumla ya Sh bilioni 1.142 badala ya Sh 744.79 kwa hisa kulingana na ripoti ya mshauri ambako hisa hizo zingekuwa na thamani ya Sh bilioni 5.869. Hatua hiyo ililisababishia Shirika hasara ya Sh bilioni 4.727.
Kwa kutumia bei ya hisa ya Sh 298 na 145 badala ya Sh 744.79 kwa hisa moja iliisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 6.285 (Sh 1,558,694,380 + Sh 4,726,526,936).
JAMHURI imeambiwa kuwa mnunuzi (mwekezaji) alilipa Sh 145 kwa hisa moja na kulipa jumla ya Sh milioni 285 kinyume cha thamani ya hisa ya Sh 744.79 au 656.15 kwa hisa moja.
Bodi ya Wakurugenzi ya UDA chini ya Simba, ikatoa punguzo la bei ya hisa hadi kufikia Sh 145 kwa hisa moja ukilinganisha bei ya punguzo iliyokuwa imeshafanyika mwanzoni ya Sh 298 kwa hisa moja ambako inaonekana iliongeza tena punguzo la asilimia 53.
Ripoti ya Makadirio ya Thamani ya Hisa na Mali za UDA
Ripoti ya makadirio ya thamani ya hisa iliyoandaliwa Oktoba 30, 2009 na Novemba 15, 2010, ilionyesha thamani ya mali za UDA ikiwa ni pamoja na mitambo na vifaa. Makadirio yaliyofanyika Agosti, 2009.
Makadirio hayo hayakuainisha Shirika ukiondoa madeni yote (Net Assets). Pia haikuonyesha madeni ya Shirika ambayo ni Sh milioni 473.241 ambayo yaliripotiwa kuwa yalishahamishiwa kwa Msajili wa Hazina.
Haijafahamika ni sababu zipi zilizosababisha hisa za UDA ziuzwe kwa punguzo la asilimia 60 kutoka kwenye bei ya makadirio ya thamani ya kiasi cha Sh 744.79 kwa hisa.
Mkataba wa kuwasilisha hisa wa Februari 11, 2011 unatamka kwamba mnunuzi atalipa Sh bilioni 1.143 kama bei ya ununuzi ya hisa zote ambazo hazijatolewa na UDA ingawa mkataba haukuonyesha akaunti ya benki ambayo malipo yangelifanyika.
Hata hivyo, ilibainika kuwa mnunuzi wa UDA alilipa Sh milioni 285 katika akaunti namba 0J1021393700 ya Benki ya CRDB inayomilikiwa na UDA.
Hapakuwapo malipo mengine ya ziada yaliyofanywa na mwekezaji/mnunuzi kuhusu ununuzi wa hisa za UDA. Malipo hayo ni sawa na asilimia 24.9 ya bei ya kuuza iliyokubaliwa.
Mwaka 2009 mnunuzi alithibitisha kumlipa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya UDA (Simba) Sh milioni 320 kama ada ya kukubali kununua UDA. “Mwenyekiti wa Bodi alikubali, alipokea kiasi cha Sh milioni 320 katika akaunti yake binafsi kutoka kwa mwekezaji ikidaiwa kuwa ni ada ya ushauri alioutoa kwa mwekezaji, ambayo ilizua mgongano wa kimaslahi,” uchunguzi ulibaini.
Ukiukwaji taratibu katika kuuza hisa za UDA
Imebainika kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya UDA haikupata kibali kutoka kwa wanahisa wake kuhusu uuzaji hisa kama inavyoagiz Sheria ya Mashirika ya Umma, kifungu Na. 257.
Ibara ya 39(2) ya Sheria ya Mashirika ya Umma iko wazi kuwa PSRC/CHC inaweza ikaelekeza njia ya uundwaji upya wa mashirika ya umma ambayo itatekelezwa, uthamini wa mali, ualikaji wa wanunuzi wenye nia na shirika linalobinafsishwa na kubaini bei ya hisa na rasilimali zitakazouzwa.
Utaratibu wa zabuni ya uuzaji wa hisa za UDA haukuwa wa kiushindani kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.21 ya mwaka 2004 na kama ilivyopendekezwa na Shirika Hodhi la Mali za Serikali, yaani CHC.
Ripoti ya uangalifu ilionyesha kwamba mwekezaji hakukamilisha masharti yaliyowekwa na PSRC kwa ajili ya kuwekeza kwenye Shirika la UDA.
Habari zilizopatikana mwezi huu zinasema Bodi ya Wakurugenzi ya UDA haikuzingatia kanuni na sheria na iliendelea na uuzaji wa hisa hizo ikitambua kuwa ilikuwa ikivunja sheria.
Kuachiwa kwa Iddi Simba
Kuachiwa kwa mwanasiasa Iddi Simba ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kabla ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kuamuru awe huru, kuliibua mgongano mkubwa serikalini.
Miongoni mwa mashitaka yaliyomkabili Simba ni pamoja na kuingizwa kwenye akaunti yake binafsi Sh milioni 320 kutoka kwa mnunuzi wa UDA.
Simba alikiri kupokea fedha hizo akisema zilikuwa ni malipo kutokana na ushauri (wa kuuza UDA?) aliompatia mnunuzi, kampuni ya Simon Group.
Ripoti ya Ukaguzi Maalumu ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilipendekeza Simba na wenzake washitakiwe.
Hata hivyo, katika hatua iliyoiwashitua wengi, kesi ya uhujumu uchumi iliyofunguliwa dhidi ya watuhumiwa hao ilifutwa kwa uamuzi wa DPP wa wakati huo, Eliezer Feleshi. Kwa sasa mwanasheria huyo ni Jaji wa Mahakama Kuu.
Mgongano wa wazi ulijitokeza kati ya ofisi ya DPP, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Wizara ya Katiba na Sheria, na Ikulu.
Ilielezwa kuwa kuliibuka mvurugano wa wazi kati ya DPP na Takukuru. Takukuru walikasirishwa na uamuzi wa DPP wa kumwachia Simba aliyetuhumiwa kuisababishia UDA hasara ya shilingi zaidi ya bilioni saba.
Kwa upande mwingine, Ofisi ya DPP nayo iliwalalimikia Takukuru kwamba hawakuipatia ushirikiano, kitendo kilichoifanya ichukue uamuzi wa kufuta kesi hiyo. Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Jaji Frederick Werema, alinukuliwa akieleza mshangao wake juu ya kuachiwa kwa Simba licha ya kuwapo ushahidi unaojitosheleza.
Mmoja wa maofisa katika ofisi ya AG alisema: “AG nimemsikia akisema kufutwa kwa kesi hiyo ni embarrassment (aibu)…ametumia hilo neno embarrassment akionyesha kutoridhishwa na kilichofanywa na DPP.”
Jaji Werema alipoombwa na JAMHURI aweze kueleza msimamo wake juu ya jambo hilo, alijibu kwa kifupi: “Sasa tupo Dodoma, ngoma turudi Dar es Salaam, kwa sasa sina taarifa zozote zaidi ya kusoma kwenye magazeti kuwa kesi imefutwa.”
Alipoombwa afafanue kama kuachiwa kwa Simba ni aibu, alijibu kwa ukali kidogo: “Nasema ngoja nirudi Dar es Salaam.”
Kwenye mitando ya kijamii ilidaiwa kwamba kuachiwa kwa Simba ulikuwa ni uamuzi na shikikizo kutoka Ikulu kwa wakati huo.
Simba alitajwa kuwa karibu na Ikulu wakati huo ikiwa ni kipindi kifupi tangu alipojiuzulu Uwaziri wa Viwanda na Biashara kutokana na kashfa ya minofu ya samaki.
Uamuzi wa DPP uliifanya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimwachie huru Simba, na wenzake wawili -Salum Mwaking’inda, aliyekuwa Mkurugenzi wa UDA na Meneja wa Shirika hilo, Victor Milanzi.
Juni 18, 2013 kesi hiyo ilipofikishwa Kisutu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, Wakili wa Serikali, Awamu Mbangwa aliwasilisha hati chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Mashauri ya Jinai (CPA), kwa niaba ya DPP akiomba kesi hiyo ifutwe kwa sababu hana nia ya kuendelea kuwashitaki watuhumiwa.
Baada ya kuwasilisha hati hiyo, Hakimu Mugeta alikubaliana na ombi hilo na kuifuta. Mmoja wa mawakili wanaowatetea washitakiwa hao, Alex Mgongolwa alisema hawakuwa na pingamizi la kufutwa kwa shauri hilo ingawa walitaka waelezwe sababu za hatua hiyo.
Mgongolwa alisema walitaka kujua sababu hizo kwani walikuwa na wasiwasi kuwa wateja wao wangeachiwa huru na kukamatwa tena baada ya muda mfupi na kupandishwa kizimbani. Waliiomba Mahakama iwape kinga.
Hakimu akiifuta kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 3/2013 na kuwaachia huru washitakiwa hao ambao, Hakimu Mugeta alisema maombi ya upande wa mashtaka yamekubaliwa.
Akizungumzia uamuzi huo wa DPP wa kuwafutia kesi wateja wake, nje ya viwanja vya mahakama hiyo, Wakili Mgongolwa alisema: “DPP anapoona hana mashahidi thabiti wa kuja kujenga kesi yake anatumia kifungu hicho kufuta kesi kwani kuendelea kuwa na kesi za jinai mahakamani ambazo anaona kabisa hana mashahidi thabiti wa kuwaleta mahakamani ni matumizi mabaya ya sheria na kuisababishia Serikali gharama pamoja na mrundikano wa kesi mahakamani.”