Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

JESHI la Polisi nchini limeungana na wadau wengine dunia katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya uchunguzi wa sayansi ya Jinai (Forensic Day) leo Septemba 20, 2024 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Kurasini.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Polisi Uchunguzi wa Kisayansi, Naibu Kamishna wa Polisi, DCP. Mwamini Rwantale ambaye pia ni Mkuu wa kitengo cha Sayansi Asili Jeshi la Polisi amesema hiyo ni mara ya kwanza kwa Jeshi la Polisi kuadhimisha maadhimisho hayo muhimu.

“Uchunguzi wa sayansi ya Jinai umesaidia kuhakikisha haki inatendeka kwa kuwa imesadia kubaini wahalifu kirahisi na kuunganishwa na tuhuma zinazowakabili pasina shaka huku wasio na hatia kuachiwa huru.

“Maadhimisho haya yamekuja muda muafaka, jeshi lipo katika maboresho ya awamu ya pili yanayoenda sambamba na utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya haki Jinai yanalenga kubadilisha fikra na kuacha kufanya kazi kwa mazoea,” amesema Rwantale.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, DCP. Dkt. Lazaro Mambosasa amesema uchunguzi hauruhusu kumuadhibu mtu ambaye hana hatia ambapo amesema uchunguzi wa kisayansi unaleta taswira njema kwa Jeshi la Polisi na Serikali katika kutenda haki.

Naye Ofisa kutoka Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa serikali, Fidelis Sekumba amesema uchunguzi wa kisayansi unatoa ushaidi wa uhakika zaidi na kunarahisisha maamuzi ya kisheria kwenye mihimili nayohusika kutoa haki.

Awali, akitoa mada katika maadhimisho hayo, Ofisa kutoka Ofisi ya Mdhibiti wa Madawa ya Kulevya nchini, Peter Patrick amesema wameanzisha maabara ya Sayansi jinai katika utambuzi wa madawa mapya yanayozalishwa sehemu mbalimbali na kuingizwa nchini.

“Tatizo hilo ni kubwa na mwaka 2023 kulikuwa na dawa za kulevya mpya zaidi ya 1000 zilizoingizwa sokoni na majina yake ni tofauti zinazotambuliwa katika orodha ya madawa yaliyopo lakini maabara hii imekuwa ikitusaidia kudhibiti kwakuwa tunamitambo ya kisasa,” amesema Patrick.

Maadhimisho hayo hufayika kila mwaka 20 Septemba yakiunganisha wataalam wa uchunguzi wa kisayasi katika kutanzua uhalifu.

Please follow and like us:
Pin Share