Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Dodoma kuhakikisha vinawasaka na kuwabaini wote waliohusika na uchomaji moto katika bonde la mzakwe hii.

Senyamule ametoa agizo hilo jana mara baada ya kufika katika eneo hilo kujionea athari za uharibifu zilizosababishwa na moto ulioanza majira ya saa saba mchana.

Amesema asilimia 70 ya maji katika Jiji la Dodoma yanatoka katika bonde la Mzakwe na ni eneo la hifadhi hivyo ni muhumimu kukakikisha linalindwa na kuhifadhiwa kwa ustawi wa afya na mazingira ya watu wote.

Aidha, amewapongeza vijana wa JKT Makutupora walioshiriki katika zoezi la kuzima moto uliotokea katika Bonde la Mzakwe Jijini Dodoma. Senyamule amewapongeza kwa uzalendo walionyesha wa kudhibiti moto huo na kuzuia  madhara makubwa ambayo yangeweza kujitokeza, amesema wameonyesha uzalendo mkubwa, uhodari na ushupavu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akipata maelezo ya awali kutoka kwa Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma Julishaeli Mfinanga kuhusu moto ulioteketeza eneo la bonde la Mzakwe Jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu

“Tumesikitishwa sana na moto huu kwa kuwa si kwamba umeathiri ikolojia ya eneo hili lakini pia umeharibu miundombinu ya Tanesco ikiwa ni pamoja na nguzo, hivyo kwanza nawapongeza vijana wetu kwa jitihada za kufanikisha kuzima moto huu na pili vyombo vyote vinavyohusika na uchunguzi vifanye kazi yake ili kubaini chanzo” Senyamule amesisitiza.

Aidha Senyamule amemuagiza Meneja wa Bonde la Wami Ruvu kuhakikisha kuwa wanachonga barabara maalumu kwa lengo la kukinga moto katika bonde hilo ili athari za moto zisiwe kubwa pindi moto utokeapo.

Awali Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Dodoma Julishaeli Mfinanga amesema kuwa walipata taarifa kwa njia ya simu kupitia namba za dharura 114 na kuwahi eneo la tukio kwa haraka. Amesema moto umedhibitiwa na hakuna madhara makubwa na wanaendelea na doria kuhakikisha usalama katika eneo lote la bonde.

Sehemu ya eneo lililoathirika na moto katika bonde la Mzakwe, chanzo cha moto huo bado hakijajulikana
Please follow and like us:
Pin Share