Tume tatu zimeundwa kuchunguza ubadhirifu, utendaji, utoaji vitambulisho kwa watu wasio raia na mwenendo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Katika hali ya kushtua, mfanyakazi wa NIDA (jina linahifadhiwa) ambaye ni mke wa mmoja wa wakurugenzi wa taasisi hiyo aliyekuwa anafanya kazi katika kituo cha Kawe, jijini Dar es Salaam, hivi karibuni amekumbwa na kashfa ya kutoa vitambulisho kwa Waarabu saba, ila “wakubwa wakafunika kombe mwanaharamu apite,” kimesema chanzo chetu.

“Nchi hii wanapelekwa magerezani wasio na watetezi. Tume imeundwa imebaini kuwa ametengeneza vitambulisho 10 na kati ya hivyo vitambulisho saba amewapa Waarabu bila kufuata utaratibu, akafanikiwa kujiingizia wastani wa Sh 2,300,000 kwa siku, lakini wapi bwana. Huyu mama kwa kuwa analindwa, alihamishiwa Kivukoni, na walipoona anaweza kufuatwa wakampeleka TCU (Tume ya Vyuo Vikuu).

“Hatujui hadi anabainika alikwisha kutoa vitambulisho vingapi kwa watu wasio Watanzania na kwa kweli hata kupelekwa TCU ni geresha tu, kwani bado anaweza kupiga simu Kibaha akaagiza atengenezewe vitambulisho anavyotaka kwa kutumia jina la mume wake,” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI linafahamu kuwa mfanyakazi huyo alitumia neno siri (password) za wafanyakazi Shafina Dwatwa na Pendo Mtui, ambao hawakuwa kazini siku alipochapisha vitambulisho hivyo, lakini pamoja na kwamba mmoja kati ya hao yuko likizo ya uzazi, nao wamepewa barua za uhamisho kama mkakati wa kumlinda mke wa bosi ‘anayefanya biashara ya vitambulisho’.

Uchunguzi unaonyesha kuwa mbali na mume wa mama huyo aliyetoa vitambulisho, anayefanya uhamisho naye ni wifi wa mama huyo ambaye ameolewa na ndugu yake.

Aidha, watendaji wanaowezesha kazi kufanyika kwa haraka nao wanapigwa vita. Mathalani, mmoja wa watumishi (jina lihahifadhiwa) ambaye alikuwa Kibaha akaongeza uzalishaji wa Namba za Utambuzi za Taifa (NIN) kutoka wastani wa 150,000 hadi 1,000,000 kwa mwezi, amepigwa vita na kuhamishwa, kwani kwa kufanya kazi kwa kiwango hicho ameonekana kuwachongea mabosi wake walioshindwa kuzalisha NIN nyingi kiasi hicho kabla yeye hajasimamia kituo.

Tuhuma za ufamilia ndani ya NIDA ambazo wao wanaziita ‘undugunaizesheni’ zina madhara ndani ya NIDA.

“Ili upige hela inakulazimu mtumishi wa NIDA ufanye kila linalowezekana hata kwa kuloga uwe kwenye ‘list ya familia’. Mchakato wa kuwahisha kutoa vitambulisho hufanywa na wale wenye access (fursa) na kuulazimisha mfumo kuchakata taarifa za mteja kwa haraka, ambapo ruhusa ya kuamuru hilo ipo kwa mwanafamilia ambaye ni mmoja wa vigogo.

“Simu moja na amri ya kigogo huyo kwenda Data Center (DC Kibaha) hufanya kila kitu kizito kuwa chepesi NIDA. IT Technicians wa DC – Kibaha wenye access ya mfumo wanaodhaniwa kuwa wawili tu, baada ya kuona wanatumika kuwaingizia fedha wanafamilia, na wao wakaweka utaratibu wa kulipwa Sh 20,000 kwa kila kitambulisho kinachochapishwa kwa haraka, na wanalipwa nao maisha yanakwenda,” imesema sehemu ya andiko ambalo JAMHURI imeliona likitumwa kwa wakubwa kulalamikia utendaji wa baadhi ya wakurugenzi wa NIDA wanaowataja kwa majina kuwa wanaiweka nchi katika hatari.

Mke wa Naibu Katibu Mkuu, ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu (jina linahifadhiwa) naye ameleta kasheshe NIDA. Amesababisha mfanyakazi Fortunate Shein kuhamishwa kituo cha kazi baada ya mmoja wa wanafamilia kuambiwa kuwa “hakumhudumia vizuri” mke huyo wa Naibu Katibu Mkuu, hivyo bila kumpa nafasi ya kujitetea akahamishiwa Kibaha.

Mfanyakazi aitwaye Zera alikwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA kumweleza kuwa baadhi ya wakurugenzi wanawalazimisha kufanya retirement (kurejesha masurufu) ya fedha ambazo hawajazitumia, lakini badala ya Mkurugenzi Dk. Arnold Kihaule kumlinda, akaishia kumhamisha kituoa cha kazi na wale aliowaripoti wakaanza kumpa maonyo wakimwambia “mshahara wa usaliti ni mauti.”

Zipo tuhuma nyingine nyingi ndani ya NIDA na JAMHURI limezungumza na Mkurugenzi Mkuu Dk. Kihaule ambaye mbali na kukanusha, amekiri kuwa kuna matatizo.

“Haya unayoyasema na mengine, tunayafahamu. Kuna tume tatu zimeundwa na mambo yote likiwamo hili (la kutengenezea Waarabu 7 vitambulisho)… sasa wana-compile report (andaa ripoti)… tuliandikiwa barua na TAKUKURU, walifanya uchunguzi baadhi ya wilaya za Dar es Salaam taarifa zikiwa tayari wahusika watawajibishwa,” amesema.

Dk. Kihaule amesema ikibainika kuwa mtumishi huyo aliyehamishwa kutoka Kawe alitenda makosa hayo, kwa kuwa bado anafanya kazi serikalini atawajibishwa, kwani kuhama kituo hakumfutii uwajibikaji. Amekanusha kuwa hana taarifa za kuendeshwa kwa mfumo wa udugu, ila akaahidi kulifanyia kazi na yeye binafsi akakana kuwa na urafiki na watu waliotajwa kuwa marafiki zake wa karibu.

“Hapa wanaonea watu tu. Leo utaambiwa huyu Thomas kuwa anasafiri sana au anaingia ofisini kwangu, anaingia kutokana na majukumu yake. Sasa kama ninataka kushughulikia masuala ya fedha niwasiliane na nani kama si Mkurugenzi wa Fedha au masuala ya Utawala niwasiliane na nani? Huyo mtu mwenyewe wanayemtuhumu anakaimu… lipo tatizo wanalolifahamu chanzo chake, ambalo ndilo chimbuko la matatizo haya na malalamiko yote wewe kachunguze utapata majibu,” amesema Dk. Kihaule.

Katika uchunguzi, JAMHURI limebaini kuwa wafanyakazi wengi wa NIDA kwa sasa hawana fedha na hili limekuwa chimbuko la malalamiko. Taarifa zinasema kuna baadhi walikopa mikopo mikubwa inayozidi mishahara yao, kwa hiyo wakati mwingine wanakatwa marejesho na kubaki na Sh 30,000.

“Hili linawatia uchungu. Posho walizozoea kuzipata wakisafiri mara kwa mara hazipo. Kwa sasa wanaishi kwa mishahara na mishahara yenyewe haipo, maana waliishaikopa. Sasa haya ni makosa yalifanyika siku za nyuma na yana gharama kubwa,” amesema mtoa habari.

Kuhusu NIDA kushindwa kukusanya Sh bilioni 18.5 ambazo zimetokana na matumizi ya taarifa za Watanzania kusajili laini za simu milioni 37 ambazo kila laini inapaswa kulipiwa Sh 500, Dk. Kihaule amesema yeye amelipigania suala hili lakini liko nje ya uwezo wake.

“Niliandika barua kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Kangi Lugola, akaahidi kuipeleka kwa Waziri wa Fedha na Mipango tupate kibali cha kukusanya fedha hizi, lakini hadi sasa Wizara ya Fedha wanasema wanalifanyia kazi” amesema.

JAMHURI limewatafuta Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango na Katibu Mkuu, Doto James, ambao hawakupatikana kujibu suala hili, ila Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja, amesema analifuatilia suala hili kufahamu limefikia wapi.

Kuhusu kununua mitambo miwili kutoka Ujerumaini ambayo haina vifaa vinavyohitajika ambavyo ni 1. HSM ambacho kina neno siri (passwords) la kuendeshea mashine hizo. 2. Compressor za kuendeshea mitambo hiyo; na 3. Servers kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu za taarifa za Watanzania watakaotengenezewa vitambulisho, Dk. Kihaule amesema mchakato wa ununuzi unaendelea ili kupata vifaa hivyo.

Pia ameongeza kuwa Kampuni ya Atlantic Zeiser GmbH ya Ujerumani na IRIS Corporation Berhad ya Malaysia, zinafanya mazungumzo kuona jinsi zitakavyotumia kadi milioni 4.7 zilizopo ambazo haziingiliani na mitambo mipya.

Kuhusu mfumo amesema: “Tumetengeneza mfumo wa vitambulisho kwa kutumia wataalamu wa ndani. Mfumo huu umetupa uhuru mkubwa.” Hakufafanua kwa ufasaha mfumo wa vitambulisho unaotumika sasa iwapo utasitishwa au utaendelea sambamba na mfumo mpya, hivyo nchi kuwa na mifumo miwili ya vitambulisho. Ameongeza kuwa Kampuni ya Tigo imeipatia NIDA servers tatu, serikali ikawapa tatu na Vodacom imewapatia tatu nyingine.

Hivi karibuni JAMHURI limeripoti kuwa NIDA wamenunua mitambo miwili ya kuchapa vitambulisho Ujerumani, lakini kutokana na kupuuza ushauri wa wataalamu mashine hizo walizozinunua kwa gharama ya Euro 3,304,650 (karibu Sh bilioni 8), pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kila moja kuchapa vitambulisho 9,000 kwa saa, haziwezi kufanya kazi kwa sasa.

Mkataba wa kununua mitambo hii miwili ulisainiwa Julai 22, 2019. Mkataba huu umesajiliwa kwa No. EA/061/2018-2019/HQ/G/01-LOT 3 wenye thamani ya Euro 3,304,650.

Mashine hizo mbili zenye uwezo wa kuchapa vitambulisho 9,000 kwa saa kila moja, baada ya kufungwa Novemba, mwaka jana, imebainika kuwa zinahitaji vifaa vitatu ili ziweze kufanya kazi. Gharama ya vifaa hivi kwa ujumla ni zaidi ya Sh milioni 600.

Vifaa vinavyohitajika ni 1. HSM ambacho kina neno siri (passwords) za kuendeshea mashine hizo, 2. Compressor za kuendeshea mitambo hiyo; na 3. Servers kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu za taarifa za Watanzania watakaotengenezewa vitambulisho.

Wataalamu kutoka Kampuni ya Atlantic Zeiser GmbH ya Ujerumani iliyotengeneza na kuuza mashine hizo, walifika nchini wakijua kila kitu kipo wakafunga mashine hizo mbili na walipouliza kuhusu hivyo vifaa vitatu, wakaonyeshwa mashine tatu za zamani zilizokuwa zinatumika kuchapisha vitambulisho vya taifa, ndipo wakasema mitambo hiyo haiingiliani. Wakaondoka kwa maelezo kuwa vikipatikana waitwe waje kumalizia kazi.

Ukifuatwa mchakato wa ununuzi kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2004 kama ilivyorekebishwa mara kadhaa, mchakato wa kupata vifaa hivyo vitatu ambao hadi tunaandika habari hii haujaanza, utachukua siku 189. Yaani miezi sita kuanzia sasa.

Hadi sasa NIDA wamesajili Watanzania milioni 21, na waliopatiwa vitambulisho ni milioni 5.9 tu, hivyo watu milioni 15.1 wanasubiri kupewa vitambulisho. Kwa idadi hii ikiwa hizi mashine zitafanya kazi vizuri kwa saa 12 kila siku bila kupumzika, zinaweza kuchapisha wastani wa vitambulisho 200,000 kwa siku, hivyo kuchapa vitambulisho milioni 15.1 kwa siku 75, sawa na miezi miwili na nusu.

Hadi sasa NIDA ina akiba ya kadi za vitambulisho zipatazo milioni 4.7 kwenye ghala. Baada ya Wataalamu kufunga mitambo hii, walionyeshwa kadi zilizopo, wakasema mitambo hii haitumii kadi hizo, inatumia aina nyingine. 

Kadi hizi zimenunuliwa kati ya dola 2 na dola 2.5 au wastani wa Sh 5,000 kila kadi moja. Hii ina maana kuwa kadi 4,700,000 zilizopo kwa kuwa hazitatumika kwenye mashine hizi mpya itabidi zitupwe. Ukizidisha kadi hizo mara Sh 5,000, unaona serikali itakuwa imepata hasara ya Sh 23,500,000.