UKUAJI wa uchumi kwa Tanzania Bara na Zanzibar unatarajiwakuendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha kwa takribani asilimia 6 na asilimia 6.8, mtawalia. Ukuaji huu unatarajiwa kuchangiwa na ongezeko la uzalishaji katika
shughuli za kilimo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi, maboresho katika usafirishaji na ugavi, nishati ya uhakika, pamoja na utekelezaji wa sera za fedha na kibajeti.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba wakati akisoma ripoti ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya BOT iliyoketi jana kwenye kikao chake cha kila robo mwaka kutathmini mwenendo wa hali ya uchumi wa dunia na hapa nchini.
“Mfumuko wa bei uliendelea kuwa tulivu katika kipindi chote cha mwaka 2024, ukiwa chini ya lengo la asilimia 5 kwa Tanzania Bara na kukaribia lengo hilo kwa upande wa Zanzibar.
Katika robo ya nne ya mwaka 2024, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa kwa wastani wa asilimia 3 kutokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha,
utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti, na kupungua kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta ghafi. Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.5 mwezi Novemba 2024,” amesema Tutuba.
Na kuongeza kuwa, mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ukibakia katika viwango vya kati ya asilimia 3.1 na asilimia 4. Hali hii itatokana na kuendelea kuwepo kwa chakula cha kutosha, utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, umeme wa uhakika, na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta ghafi. Uwezekano wa mabadiliko katika maoteo haya ni mdogo.
“Ukuaji wa ujazi wa fedha na mikopo kwa sekta binafsi uliendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha mwaka 2024, ambapo ulifikia wastani wa asilimia 12.5 na asilimia 16.9, mtawalia,” amefafanua gavana huyo na kuongeza kuwa.
“Katika robo ya nne ya mwaka 2024, ujazi wa fedha ulikua kwa wastani wa asilimia 14.8 kwa mwaka ikilinganishwa na asilimia 13.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, huku mikopo kwa sekta binafsi ikikua kwa wastani wa asilimia 16.8 ikilinganishwa na asilimia 17.8.
Mwenendo huu unatokana na ongezeko la mahitaji ya mikopo mipya kufuatia kuimarika kwa uchumi wa dunia na hapa nchini, pamoja na kupungua kwa vihatarishi katika ukopeshaji kufuatia kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu kufikia asilimia 3.6 mwezi Novemba 2024 kutoka asilimia 4.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.”