Tanzania imeelezwa kuwa na uchumi imara unaoendelea kukua vizuri chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametanabaisha.
Kwa mujibu wa waziri mkuu, uimara huo ni kati ya sababu lukuki zinazoifanya Tanzania kuwa chaguo la wawekezaji na mshindani mkubwa wa kuvutia mitaji mikubwa katika ukanda huu na Afrika kwa ujumla.
Akihutubia Kongamano la Fursa za Uwekezaji mkoani Pwani lililokwenda sambamba na uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji mkoani humo hivi karibuni, waziri mkuu aliwaambia wawekezaji kutokuwa na hofu ya kuwekeza nchini kwani mitaji yao itakuwa salama.
“Nchi ina uchumi imara na tulivu na unaotabirika. Kwa miaka minne mfululizo uchumi wetu umeimarika sana na kukua kwa wastani wa asilimia saba kati ya mwaka 2015 na 2019,” Majaliwa aliwaambia washiriki wa kongamano hilo lililofanyika Ijumaa ya Oktoba 18 kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Pwani mjini Kibaha.
Kiongozi huyo pia alisema kuwa Tanzania ni kati ya nchi tano Afrika zinazoongoza na kufanya vizuri kiuchumi zikiwa na ukuaji wa kasi kubwa wa pato la taifa (GDP). Kwa mujibu wa mashirika ya fedha na maendeleo ya uchumi ya kimataifa, nchi nyingine kwenye orodha hii ni pamoja na Ethiopia inayoongoza, Rwanda, Ghana na Senegal.
Majaliwa alisema kiashiria kingine kikubwa cha uimara wa uchumi ni viwango vya kuridhisha vya muda mrefu vya mfumuko wa bei. Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, mfumuko wa bei umekuwa katika tarakimu moja ikiashiria kutopanda kwa kasi kubwa kwa gharama za maisha.
Taarifa za hivi karibuni kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinaonyesha kuwa mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2019, umepungua hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.
NBS inasema hii inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa kipindi hicho imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.
Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimekuwa na viwango vya chini vya mfumuko wa bei miongoni mwa nchi za SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kati ya Januari na Septemba mwaka huu, wastani wa mfumuko wa bei hapa nchini ulikuwa ni asilimia 3.4 kwa mwezi.
“Mfumuko wa bei umedhibitiwa vizuri na umekuwa katika tarakimu moja kati ya asilimia tatu na tano kwa muda mrefu kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano,” waziri mkuu alisema kwenye hotuba yake ambayo pia iliainisha hatua ambazo serikali inazichukua kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara hapa nchini.
Hatua hizo ni pamoja na kuanzisha wizara maalumu inayoshughulikia masuala ya uwekezaji iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Majaliwa alisema serikali ambayo ni sikivu kwa wafanyabiashara, pia imefanikiwa sana kudhibiti rushwa ambayo hapo nyuma ilikuwa kikwazo kikubwa kwa wawekezaji.
Aliupongeza Mkoa wa Pwani kwa kuwa mstari wa mbele kuvutia wawekezaji na kujenga viwanda huku akiitaka mikoa ambayo bado haijatekeleza agizo lake la kuandaa makongamano ya uwekezaji ihakikishe inafanya hivyo mara moja.