Nimeishawahi kusema kwamba Watanzania tuna kumbukumbu dhaifu, kwa maana kwamba hatukumbuki jana na wala hatutaki kujua nini kitakachotokea kesho.
Mwaka 1984 si mbali, ni majuzi tu, na kwa bahati nzuri baadhi ya waliokuwa wanapanda mabasi kwenda bungeni wapo, na wamekuwa ndiyo vinara wa kung’ang’ania kununuliwa mashangingi ya milioni.
Maisha ya binadamu yanategemeana sana na mabadiliko ya maendeleo ya kila siku, ambayo yanasababishwa na kuboreka kwa afya, uchumi, teknolojia na hata mila na desturi.
Kama miaka 30 iliyopita, wabunge wetu walitumia usafiri wa kawaida wa mabasi unaotumiwa na kila mtu kwenda bungeni, na naamini kwamba walifanya hivyo kwa vile nchi yetu ilikuwa na uwezo mdogo kiuchumi, hivyo haikumudu kuwanunulia wabunge magari ya thamani wakati wananchi wa kawaida wanaishi maisha duni.
Tukumbuke kipindi hicho nchi yetu ilikuwa imeyumba sana kiuchumi, ilikuwa ombaomba iliyosababishwa na matokeo ya vita dhidi ya Uganda ya kumtoa madarakani Idi Amin, hivyo ilikuwa si busara wabunge kutanua na magari ya fahari wakati nchi inaomba chakula na dawa kutoka nchi za nje.
Wabunge wanakula majogoo peke yao!
Baada ya miaka 30 nchi yetu uchumi umekua, kwa vile idadi ya watalii kutoka nchi za nje imeongezeka na idadi ya wawekezaji imeongezeka, hasa baada ya kubinafsisha viwanda vyote vya umma na mashirika pia.
Tunachimba madini mbalimbali yakiwamo dhahabu, ambapo Tanzania ni nchi ya tatu katika Bara la Afrika kwa uzalishaji wa dhahabu.
Tumegundua gesi nyingi kule mkoani Mtwara, tumegundua mafuta kule mkoani Mtwara na pia tumewauzia wawekezaji ardhi kubwa kwa ajili ya uwekezaji.
Hivi vyote ni vithibitisho kwamba uchumi wetu umekuwa, ndiyo maana Serikali imeamua wabunge wetu wanapoenda bungeni kutunga sheria na kujadili mambo muhimu ya kijamii na maendeleo wasipande tena mabasi, bali wapande mashangingi ya mamilioni.
Huo ni uamuzi mzuri kwa vile tunajituma kwa ajili ya kujinufaisha sisi wenyewe. Lakini mbona wote tunajituma kwa pamoja isipokuwa kwenye kufaidi wanafaidi wabunge peke yao?
Ningependa tu kuishauri Serikali kwamba kama mwaka 1984 wote kwa pamoja bila ya kujali mbunge au raia tulifunga mikanda na tukapanda mabasi, iweje leo hii umefika muda wa matanuzi wajitanue wabunge peke yao? Ni kwanini wote tusijiachieeee?
Wengine tumeshindwa hata kumudu daladala (mabasi), lakini wenzetu wabunge wanatanua na mashangingi ya mamilioni. Je, haya ndiyo matunda ya Uhuru tulioupigania kwa miaka kwa kila hali?
Mwisho, nasema uchumi ukikuwa usiishie mifukoni mwa wabunge peke yao, bali usambae na kufika mifukoni mwa makabwela kama sisi.
Dr. Noordin Jella
Email: [email protected]
Mobile: 0782 000 131