Wiki mbili zilizopita nimekuwa nikiandika waraka wa kiuchumi kwa wafanyakazi. Kwa ujumla wake, waraka huo utaendelea hadi sehemu ya 10. Kutokana na urefu huo, nimepanga kutouleta kwa mfululizo wa wiki zinazofuatana, badala yake nitakuwa ninauleta kwa wiki tofauti, mwaka huu.
Leo ninapenda tuperuzi nafasi ya uelewa wetu sisi Watanzania, linapokuja suala la uchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Unapotaja Afrika Mashariki ni kwamba kuna mambo ya msingi ambayo yanaushikilia uhusiano huu.
Pamoja na mambo mengine, nguzo kuu ya kuwapo kwa EAC ni suala la uchumi. Ndiyo maana tunaongelea soko la pamoja, sarafu moja, kusafiri kwa mitaji na rasilimali watu.
Mambo mengine yanayojadiliwa na kushughulikiwa katika ushirikiano huu, yanasaidia tu kuboresha lengo kuu la msingi; ambalo ni kuboresha uchumi wa ukanda huu. Kwa tafsiri rahisi ni kuwa lugha ya Afrika Mashariki ni uchumi. Ili kunufaika na Jumuiya hii lazima kuijua lugha hii, kuyajua matendo ya kiuchumi, kuelewa mwenendo wa kiuchumi na kutambua nafasi ya mtu mmoja mmoja katika uchumi.
Wakinga tuna msemo usemao, “Kama wewe si mchawi, hakikisha unamfahamu mganga mzuri.” Si lazima uwe mjuzi ama mtaalamu wa mambo ya uchumi na lugha za uchumi wa darasani ili kuijua lugha ya Afrika Mashariki; bali unaweza kujifunza na kujizoesha kutoka kwa waganga (wataalamu) na baadaye nawe ukawa mchawi (mtumiaji).
Je, Watanzania tunaijua kwa kiasi gani lugha inayotumika Afrika Mashariki? Je, tunaelewa maana na matendo ya kufanya tunaposikia viashiria vya masoko ya hisa, masoko ya mitaji, sarafu ya pamoja, ushirikiano wa kodi na ushuru, au tunapoambiwa mtiririko wa rasilimali watu? Kwa bahati mbaya sana ni kuwa kutojua lugha hizi hakutoi msamaha wa kuhurumiwa linapokuja suala la utekaji wa fursa zilizopo kwenye EAC.
Hebu tuangalie mifano michache ya lugha ya Afrika Mashariki. Unaposikia masoko ya mitaji na hisa kichwani kwako lazima kuje maneno kama DSE (Dar es Salaam Stock Exchange), USE (Uganda Stock Exchange) na NSE (Nairobi Securities Exchange). Haya ni masoko ambayo kunatokea ununuzi wa hisa na ubadilishanaji wa mitaji.
Hapo kuna kampuni ambayo zinazopeleka sehemu yake kuwa miliki ya umma, hivyo unaweza kununua ama kuuza sehemu za hisa za kampuni hizo. Kujua kuhusu DSE, NSE na USE hakuhitaji hadi uwe unamiliki hisa ama mtaji pale isipokuwa mwenendo wake unaathiri uchumi wa eneo hili na hivyo kuathiri ustawi wako binafsi kiuchumi.
Nikisema habari za hisa na mitaji mtu anaweza kudhani ninaongelea masuala ya kitaalamu sana. Kumbuka ninaongelea lugha ya Afrika Mashariki. Namna kampuni zinavyojiandikisha na kuuza mitaji kwenye masoko ya hisa na mitaji, kunaonesha mtiririko na mwelekeo wa mitaji katika ukanda mzima.
Nasi tunajua kuwa ulipo mzoga ndipo wakutanikapo tai. Tai wanajuaje kuwa sehemu fulani kuna mzoga? Jibu ni rahisi, wanatumia harufu kutambua. Je, unajuaje kuwa Uganda ama Rwanda kuna fursa za kuwekeza?
Ni kwa kuangalia mwenendo wa mitaji na hisa kama kiashiria kimoja kati ya vingi vilivyopo. Ubaya ni kwamba hata kama wewe usipoisikiliza harufu ya ‘mzoga wa uwekezaji’, wenzako kutoka nchi nyingine za Jumuiya wataisikiliza harufu iliyopo hapa Tanzania nao watakusanyika.
Ninapoongelea habari za DSE, USE na NSE naelewa kuwa si rahisi sana kwa wengi kuelewa fursa zilizopo ndani yake, pengine kutokana na historia ya uchumi na mazoea yetu. Wenzetu Kenya NSE ilianza (japo si rasmi) mwaka 1954 wakati sisi DSE ilianza mwaka 1996.
Wanzetu wana uzoefu mkubwa na lugha hii wameizoea kwa kiasi kikubwa. Pale NSE kampuni zilizojiandikisha ni zaidi ya 50 wakati hapa kwetu DSE kuna kampuni pungufu ya 20, tena nyingine zikiwa ni zile zile za kule Kenya (Cross-listing).
Kwa upande wa Uganda hawana tofauti na sisi kwa maana ya kuanza, kwani USE ilianza 1997 lakini kasi yao ya kuijua lugha hii ni kubwa mno. Mwaka 2010 USE ilikuwa kinara wa masoko yote ya hisa kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa kutumia kipimo cha ALSI (All Shares Index) ikiwa na mrejesho wa faida ya asilimia 74% kwa hisa zinazonunuliwa na kuuzwa.
Sina lengo la kukupitisha porini katika takwimu za kitaalamu lakini kuna kitu nataka tujifunze; Kenya walitangulia miaka mingi, Uganda ni wapya kama sisi lakini wanajifunza kwa kasi ya jabu. Wenzetu walishatangulia na wengine wanakimbia lakini sisi tunazinduka polepole mno.
Nikiri wazi kuwa mambo kama haya ya hisa na mitaji kiasili yaliibuka kutokana na ubepari, lakini kwa kuwa tumeamua ‘kuchanganyika’ hatuna ujanja zaidi ya kuungana nao. Kumbuka kuwa kama wewe si ‘mchawi’ hakikisha unawajua ‘waganga wazuri’, hatuna ujanja inatakiwa tujifunze na kuizoea lugha hii tuweze kuelewana na wenzetu wa hapa jumuiyani.
Katika robo ya mwaka jana, kampuni nyingi za umma na binafsi katika nchi zote tano za Afrika Mashariki zimeendelea kutoa ripoti zao za kifedha na kiutendaji kwa mwaka ulioishia Desemba 2012.
Hapa napo tunaweza kuitathmini hali yetu tuliyonayo katika lugha ya Afrika Mashariki kwa kuangalia namna tunavyozipokea ripoti hizo.
Nianze na namna jirani zetu Kenya wanavyozipokea ripoti hizo. Wakati kampuni 20 kubwa (zilizopo kwenye 20 Shares Index) zikiachia ripoti zao nchini Kenya; kulikuwa na gumzo mitaani kila mmoja akihaha kuzifuatilia, kuzisoma na kuzitafsiri. Wanahisa na wasio wanahisa wanataka kujua kampuni gani imefanya vipi, ipi imeizidi ipi, ipi ina fursa na gawio zuri kwa kuwekeza, ipi ina mikakati gani ya muda ujao na mengine mengi.
Gazeti moja la nchini Kenya lilipiga picha inayoonesha watoto wa sekondari katika mji wa Naivasha wakisoma ripoti ya mojawapo ya benki za biashara. Walipoulizwa mmoja wao alijibu, “Mama ana hisa kwenye benki hii nataka nijue mwenendo wake.” Hapo ni Kenya! Hadi watoto wa shule za sekondari wanaongea lugha ya Afrika Mashariki!
Hali ni tete kwa Tanzania kwa sababu ripoti za kampuni za ndani ama za wawekezaji huwa hazipokelewi kwa hamasa yoyote. Kwanza ni wachache ambao wanafuatilia ripoti hizo na – achilia mbali uwezo wa kutafsiri – maana na athari za ripoti hizo kwa Afrika Mashariki na watu wake.
Kule Rwanda na Burundi wenzetu ndiyo kwanza wanajenga upya nchi zao; hivyo si rahisi sana kutoa hitimisho la moja kwa moja kuhusu hisia zao katika ålugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; lakini kiu yao ya kuinuka kiuchumi na kijamii inaonesha namna ambavyo wanaweza kutupita.
Unaposoma ripoti za kampuni hizi (financial statements) kuna ishara zinatoa ikiwamo, “Nenda katafute ajira sehemu fulani.” “Nenda kawekeze kitu fulani mahali fulani.” “Ondoka mahali fulani kwa sababu pameharibika.” Na kadhalika.
Kwa kutozijua lugha hizi, tunabaki tumeduwaa tusijue cha kufanya wala pa kuelekea. Kwa kuwa wenzetu wanaelewa lugha na matendo ya Kiafrika Mashariki ni rahisi na itaendelea kuwawia rahisi kunufaika na lugha hii.
Tatizo letu Watanzania wengi tunatumia malalamisho kama silaha ya kujiokoa na hatari za Afrika Mashariki. Juhudi zetu katika kuteka fursa za EAC zimeota matege na tumekuwa na mtazamo mdogo mno kuhusu mambo tunayotakiwa kufanya.
Kwa mfano, kitendo cha kukazana kujifunza Kiingereza ama kukazana kununua ardhi kwa ajili ya fursa za Afrika Mashariki si kibaya, lakini ni mtazamo mdogo sana. Tukiijua lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; tutaona na kuoneshwa mambo mengi yanayotuhusu katika Jumuiya hii.
Kwa leo nikomee hapa, lakini natarajia kuendelea na chambuzi mbalimbali kuhusu biashara, ujasiriamali na uchumi katika mtazamo wa Kiafrika Mashariki huko mbeleni.
Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi Afrika Mashariki.
[email protected], 0719 127 901