Mgogoro wa kugombea uchinjaji wanyama baina ya Waislamu na Wakristo unaendelea kuwanyima usingizi viongozi wa dini na serikali.
Baadhi ya viongozi hao hivi sasa wanajizatiti kuweka mikakati ya kusaka ufumbuzi wa mgogoro huo, huku wengine wakiufananisha na ujinga usiostahili kumilikiwa na Watanzania.
Viongozi wa dini na serikali waliozungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti wiki iliyopita, wameahidi kuchukua hatua zinazostahili kuhakikisha mgogoro huo sasa haupati mwanya wa kutowesha amani na utulivu nchini.
Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, yeye pamoja na mambo mengine, anawatazama wanaojikita katika kugombea uchinjaji huo kama watu wajinga wasiojua mambo muhimu ya kushughulikia.
“Mgogoro huo [kugombea uchinjaji wanyama] ni sehemu kubwa sana ya ujinga, kwanini tusishughulikie vitu vya maendeleo?,” amehoji.
Hata hivyo, Askofu Mokiwa amesema anaunga mkono kauli ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwingi, aliyoitoa katika Kongamano la Utamaduni wa Kiislamu katika Nchi za Afrika Mashariki lililofanyika Dar es Salaam, hivi karibuni.
Katika kongamano hilo, Mwinyi almaarufu ‘Mzee Ruksa’, alisema, “Wakati wa uongozi wangu kulitokea vurugu zinazofanana na hizo baada ya watu kuvunja mabucha ya nguruwe, ambayo yalikuwa yanakwaza wale wanaofuata Dini ya Kiislamu.
“Niliwambia wananchi ‘ruksa’ kula chochote watakacho, pia nilikuwa sitaki imani ya mtu mmoja kumuudhi mwingine, au ivunje sheria.
“Imani ni nafsi ya mtu na haitakiwi kumlazimisha kula nyama iliyochinjwa na mwenzie. Kama unaona aliyochinja mwenzio ni kibudu basi usile, chinja yako, kula hata ukitaka kula chura, mjusi, konokono, kula utakacho ruksa ilimradi tu usiingie katika jinai.”
Kwa upande wake, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba, amesema pamoja na mambo mengine, kamati aliyoiunda hivi karibuni itashughulikia pia tatizo la mgogoro wa uchinjaji wanyama kwa ajili ya kitowewo.
“Nimeshaunda kamati ya watu ninaowatuma kwenda kuwaomba viongozi Kikristo ili nikutane nao tuzungumzie migogoro ukiwamo wa uchinjaji,” amesema Mufti Sima na kuendelea:
“Nia yangu ni kukutana na viongozi wakuu wa madhehebu ya Kikristo tuzungumze. Sisi [viongozi wa dini] ndio wadau wakuu wa amani, mgogoro wa kuchinja si mkubwa, sisi ndio tunashughulikia migogoro ya dini.”
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, naye ameunga mkono kauli ya Mzee Ruksa kuhusu suala la uchinjaji akisema Wakristo hawazuiwi kuchinja kitoweo chao kwa ajili ya kula katika familia zao.
Hata hivyo, amesema kutokana na ustaarabu uliojengeka tangu zamani, Waislamu wataendelea kuchinja kitoweo cha jamii yote kama ilivyokubaliwa na Maaskofu na Masheikh.
Amefafanua kuwa hali hiyo haina maana kwamba Waislamu ni bora kuliko watu wa dini nyingine bali inatokana na miiko ya dini yao ya kutokula kitoweo kilichochinjwa na muumini wa dini nyingine.
“Unajua wenzetu [Wakristo] hawana miiko, dini yao inawaruhusu kula kitoweo kilichochinjwa na Waislamu na ndiyo maana wako tayari hata kuchinjiwa kitoweo chao na Waislamu,” amesema Sheikh Salum.
Kwa upande wa serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, hakuwa tayari kuzungumzia mgogoro huo kwa madai yake kuwa hana muda.
“Sitaweza kuzungumzia suala hilo, na kwanza ninaingia kwenye cabinet (Baraza la Mawaziri).
Wakati viongozi hao wa kiroho wakizungumza hayo, Wakuu wa Mikoa ya Geita, Shinyanga, Mbeya na Mwanza, wamesema wanaendelea na juhudi za kuwaunganisha Waislamu na Wakristo ili kudunia amani na utulivu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga, ameliambia JAMHURI kuwa mgogoro wa uchinjaji huo umeshughulikiwa kwa mafanikio mkoani humo baada ya pande zote kukubaliana kuishi kama zamani.
“Sisi huku Shinyanga kwa sasa hatuna tatizo hilo, tumeshalishughulikia tukakubaliana pande zote kwamba turejee kuishi kama zamani, Waislamu waendelee kuchinja,” amesema Rufunga.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa mkoa amesema bado ofisi yake inaendelea na jitihada za kuimarisha ushirikiano baina ya viongozi wa madhehebu tofauti ya dini mkoani humo.
“Tumetengeneza ratiba ya kuwakutanisha viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kwa lengo la kuhamiasisha ushirikiano wao kwa manufaa ya Taifa,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula, amesema anachoshughulikia zaidi kwa sasa ni kuhakikisha Waislamu na Wakristo wanaishi kwa amani na upendo. “Sasa hivi watu wanaendelea na shughuli zao za kimaisha kama kawaida. Tunachofanya ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na upendo.
Migogoro inavuruga amani na kurudisha nyuma maendeleo,” amesema Magalula. Akizungumza na JAMHURI, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, amesema kwamba kwake yeye kuzungumzia suala la mgogoro huo kwa sasa ni sawa na kufukua makaburi.
Mbali ya hilo, amekataa kulizungumzia suala hilo kwa kile alichoeleza kuwa yeye si mtaalamu wa masuala ya dini, na suala hilo ni la kitaifa, si Mkoa wa Mbeya pekee.
Haya hivyo, amewashukuru Waislamu na Wakristo wa mkoani Mbeya kwa kumaliza tofauti zao kuhusu uchinjaji na sasa hali ni shwari.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikillo, amesema anaendelea kujikita katika msimamo wa serikali uliotangazwa na Rais Jakaya Kikwete kwenye hotuba yake ya mwisho wa Machi, mwaka huu, kwamba mgogoro huo unaendelea kushughulikiwa.
“Lakini kwa ujumla hali ni nzuri mkoani Mwanza, wameshaelewana [Waislamu na Wakristo], hili ni suala la imani, hakuna problem (tatizo) kwa sasa,” amesema Ndikillo.