Ndugu msomaji, sikulazimishi kuamini ninachokiamini mimi, ila ninakushawishi kukitafakari ninachokiandika. Mjadala huu ni maoni na mtazamo wangu siyo tamko la dini fulani na siy tamko la gazeti hili la JAMHURI.
Ndugu msomaji, kumbuka kwamba hakuna mtu mjinga kuliko mwingine, na hakuna mtu mwerevu kuliko mwingine – wanadamu wote wanao mwanga pia wanalo giza. Nitashukuru kama utajiuliza maswali yaliyo na majibu na yasiyo na majibu baada ya kumaliza kusoma mjadala huu. Kuna methali ya Kihausa isemayo, ‘Muziki ukibadilika na dansi inabadilika’.
Katika maisha mabadiliko yanapotokea, huibuka makundi matatu ya watu. Wapo wale wanaokubali mabadiliko, ‘Mabadiliko huwatunza’. Wapo wanaoyakataa, lakini wanataka wabaki kwenye mfumo, ‘Mabadiliko huwaondoa’. Wapo ambao hawajui nini kinaendelea, ‘Mabadiliko huwashangaa’.
Tukubali kubadilika penye sababu ya kubadilika. Wakati mwingine Watanzania wanaonekana kama watu ambao akili zao zimekusanywa kwa pamoja na kukabidhiwa kwa ‘mtunza akili’. Hii ni kutokana na dhana ya kushikilia baadhi ya imani ambazo ni potofu, kama dhana ya uchawi na ushirikina.
Utafiti uliofanywa mwaka 2010 na asasi ya Marekani inayoitwa PEW Research Centre ulibaini na kuonesha kwamba, asilimia 93 ya Watanzania wanaamini katika ushirikina. Yaani kati ya nchi 19 za Afrika ambako utafiti huo ulifanyika, Tanzania ilishika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Cameroon yenye asilimia 78. Ni kichekesho kwelikweli.
Haishangazi sana kila kona ya miji yetu tunapopita tunakutana na vibao barabarani vya waganga wa kienyeji. Matangazo yao utaona yanasomeka hivi, “Dk. Bingwa kutoka Koromije” Anatoa huduma zifuatazo:- Kumrudisha mpenzi wa zamani, Kuongeza nguvu za kiume,Kuongeza akili za darasani, Kumsahaulisha mdai wako, Kuongeza mvuto kwa warembo, Kupandishwa cheo kazini.”
Ifahamike kwamba, karne ya 21 ni karne ambayo kila nchi duniani inajishughulisha na utafiti wa kisayansi na kiteknolojia, lakini hapa kwetu mambo ni tofouti, imani za kishirikina ndiyo kipaumbele.
Jamii yoyote ile ni lazima itembee katika ukweli, haki, maadili, mwanga na elimu. Hakuna jamii inayoweza kuendelea pasipo watu wake kuwa wakweli na wenye maadili na akili tafakari na akili bainifu. Hatuwezi kuendelea kutambua kwamba sisi ni wajinga na bado tukaendelea kuishi maisha ya kijinga.
Lazima tukubali kubadilika. Tunahitaji kufahamu lipi linaweza kubadilishwa na lipi haliwezekani na zaidi kufahamu tofauti zake. Kwa hali ilivyo sasa, Watanzania wanahitaji kupikwa na kupikika kifikra. Duniani kote hakuna mabadiliko ya kweli na ya kudumu nje ya uhuru wa kifikra.
Kwa usemi mwingine, tunaweza kusema kwamba akili iliyo huru ni nyenzo muhimu sana katika mapinduzi yoyote yale. Hapa Tanzania kuna baadhi ya wasomi mahiri na viongozi mahiri wameweka akili zao mifukoni kwa sababu ya maslahi binafsi wanayotaka yawanufaishe wao wenyewe na familia zao.
Sina hakika kama yupo msomi au kiongozi hapa Tanzania ambaye walau amejaribu kushirikisha ujuzi wake kwa Watanzania kama ambavyo Mwalimu Nyerere alivyotumia vipaji vyake vyote kwa manufaa ya Watanzania. Ninachokiona kwa wasomi na viongozi wetu wa Kitanzania ni ubinafsi wa kutoshirikisha tunu zao kwa Watanzania wenzao.
Ninapenda kuwaalika wanateolojia, wanafalsafa, wanasayansi na wanahistoria na watu mbalimbali wajitokeze hapa gazetini kuthibitisha ama kukana uwepo wa uchawi. Lengo kuu ni kuporomosha dhana ya uchawi/ushirikina kutoka kwenye bongo za Watanzania na waafrika kwa ujumla wake.
Kabla sijaendelea na mjadala, ninaomba kutoa fikra zangu. Binafsi siamini uwepo wa uchawi. Siamini uwepo wa majini, siamini uwepo wa mizimwi na mahoka. Hata kwa chembe kidogo siamini. Ukiniuliza je, wachawi wapo au hawapo? Nitakujibu. Hawapo, isipokuwa katika mawazo ya mtu anayesadiki na anayeogopa kwamba wachawi wapo.
Kama wachawi wapo wanapatikana wapi? Kama wachawi wapo wanashindwa nini kuwapa wachezaji wa timu ya Taifa dawa la kushinda kwa kila mechi wanazocheza? Kama wachawi wapo wanashindwa nini kuiba pesa benki? Mimi nawatafuta hao watu wanaoitwa wachawi.
Ningefurahi sana kama mwenye tafiti za kina za uwepo wa uchawi angejitokeza hapa gazetini na kuthibitisha hoja yake ya uwepo wa uchawi. Binafsi nimefanya tafiti ya uwepo uchawi kwa baadhi ya makabila ya hapa Tanzania. Nilichobaini ni hofu tu. Hakuna uchawi. Mwenye hoja ya uwepo wa uchawi namsubiri ajitokeze.
Msinitake kucheka. Eti mchawi ni mtu ambaye anaweza kuingia mlango ukiwa umefungwa. Anaweza kupaa bila kifaa chochote. Anaweza kumdhuru mtu yeyote. Anaweza kumgeuza panya akawa mbwa. Anaweza kuwasiliana na mapepo, shetani, majini n.k. Binafsi siamini sifa hizo.
Ninazisikia tu. Hizo ni sifa ambazo kimaumbile binadamu hawezi kuwa nazo. Lakini naamini hazipo kwa binadamu ninayemfahamu. Uchawi haupo ila shetani yupo. Hakuna binadamu mchawi, ila yupo binadamu mjanja mjanja anayekuzidi ujuzi fulani. Nisikilize; ni kwamba dhana hii ya uwepo wa uchawi/ushirikina ilipandikizwa na mababu zetu.
Kwa wakati wao walipandikiza dhana hii kulingana na mazingira yao yalivyokuwa. Kwetu sisi hatupaswi kuishi nadharia za mababu zetu. Hata Ulaya hii dhana ya uchawi/ushirikina ilikuwapo. Asia napo ilikuwapo kwa bahati nzuri wenzetu wa mabara mengine walibandukana na dhana hii.
Bahati mbaya ni kwetu sisi Waafrika ambao bado tumeikumbatia dhana hii potofu. Wenzetu wanatushangaa. Sisi ni binadamu tunaokua kiumri lakini tusiokuwa kifikra. Waafrika hatujaonesha dhamira ya dhati ya kubandukana na dhana hii ya uchawi/ushirikina. Tatizo liko wapi?
Kwa bahati mbaya sana, wale ambao wangekuwa mstari wa mbele kuporomosha dhana hii ya uchawi/ushirikina kutoka kwenye bongo za wanajamii wetu nao wanaamini uwepo wa uchawi. Kwa tafsiri nyingine uwepo wa hofu ya uchawi/ushirikina kwa wanajamii wetu ni mtaji kwa baadhi ya watu na taasisi za kidini. Ni mtaji makanisani.
Katika jamii yetu kuna wimbi la makanisa yanayoota kama uyoga. Wachungaji wa haya makanisa wengi wao wanaamini uwepo wa uchawi/ushirikina. Ni hao hao wanaopandikiza hofu ya uwepo wa uchawi kwa waumini wao kwa kuwatungia vitabu na sala kadha wa kadha za kupambana na wachawi. Wanaaminisha kwamba uchawi upo, hivyo wapambane nao kwa nguvu za maombi.
Chunguza; utabaini kwamba uwepo wa makanisa haya ni kichocheo cha uwepo wa ushirikina. Ibada nzima unakuta mchungaji anahubiri habari za uchawi. Sipingi uwepo wa makanisa. Hapana, ila napinga uwepo wa wachugaji ambao hawafahamu teolojia ya Maandiko Matakatifu.
Siwezi kuchelea kuandika, baadhi ya wachungaji wengi wa makanisa hawafahamu teolojia ya Maandiko Matakatifu. Wengi wao ni wababaishaji. Ninawaomba wakasome. Watakuwa msaada mkubwa wa kuporomosha dhana hii ya uwepo wa uchawi/ushirikina kutoka kwenye fikra za waumini wao. Waafrika na Watanzania wakiwamo tunaishi ni kwa sababu tu tumepata fursa ya kuishi.
Tunastahili kuishi, lakini hatustahili kuishi haya maisha tunayoishi. Tufikirie upya mfumo wa maisha tunayostahili kuishi. Mwandishi wa kitabu cha ‘Passages’, Gail Sheely, ameandika “Kama hatubadiliki hatukui. Kama hatukui ni dhahiri hatuishi”. Tunakuwa kiumri lakini hatukui kifikra.
Tunahitaji ukombozi wa kifikra. Ukosefu wa fikra sahihi na bainifu kwa maisha ya mwanadamu yeyote yule ni ugonjwa. Ni ugonjwa usioonekana kwa vipimo vya kisayansi lakini ni ugonjwa unaoua kwa haraka sana kuliko magonjwa mengine. Ni ugonjwa unaoonekana kwa vitendo na kwa uamuzi mbalimbali wa mhusika. Dhana ya uchawi inatudhalilisha sana sisi Watanzania. Ni Tanzania kiongozi akiwa anawania nafasi ya uongozi anaenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta nyota ya mvuto.
Anaona elimu aliyopata haijampa uwezo wa kujieleza na kujenga hoja na jamii ikakubaliana na hoja yake. Tumefika mahali Watanzania wanaamini kupata utajiri mpaka kuiba au kujiunga na mtandao wa kishetani [Freemason].
Hii ni dhana kuntu inayohitaji kuondolewa kutoka kwenye bongo za Watanzania. Ni ajabu sana. Kwa uhalisia wake, Watanzania wanahitaji uponyaji wa kifikra. Tuko gizani. Tunaishi ni kwa sababu tunaishi.
Watanzania tumekuwa kama mbuzi wa kiangazi. Mbuzi wa kiangazi wanazunguka kutwa nzima pasipo kuelewa wanaelekea wapi. Hatuwezi kulikomboa Taifa letu pasipo tafiti za kisomi. Umefika wakati sasa wa kuacha kuishi maisha ya kimazoea. Umefika wakati sasa wa kuacha kuishi maisha ya kuazima.
Umefika wakati sasa wa kuacha kuishi maisha ya kuibia. Tanzania yenye watu wenye akili pevu inawezekana. Tanzania yenye uchumi wa kati, juu inawezekana.
Watanzania tunahitaji ukombozi wa kifkira tumekwama katika mengi, tumedumaa katika mengi, tumenyanyapaliwa katika mengi. Hatushituki? Hatutafakari? Kila kukicha mwanadamu anakabiliwa na zoezi la kufanya uchaguzi fulani.
Ulimwengu huu hauna nafasi kwa watu wanaopuuzia maarifa ya muhimu. Kila kukicha yeyote anaalikwa kuukaribisha utajiri na kuuaga umaskini au kuuaga utajiri na kuukaribisha umaskini. Methali ya Kichina yasema wazi kwamba, ‘Dunia ni ya wale ambao wanavuka madaraja mengi katika kufikia kwao kabla ya wengine kuona daraja hata moja’.
Mantiki inatunong’oneza ukweli kwamba fikra zilizotufikisha katika mazingira tuliyomo kwa sasa na hali tuliyonayo leo, fikra hizo kwa uhalisia wake hazitaweza kututoa kwenye matatizo tuliyonayo kwa sasa. Methali ya Kifaransa inatukumbusha kwamba, “Yeye anayengoja kuvaa viatu vya marehemu anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu.”
Kusubiri maendeleo yatokee pasipo kufanya kazi kwa bidii ni kwamba unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu. Kulalamika kwa kila jambo pasipo kubuni mbinu na mikakati ya kukuinua kiroho, kimaadili, kisiasa, kiafya na kiuchumi ni kwamba unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu.
Dhana ya kung’ang’ani imani za uchawi ni kusubiri viatu vya marehemu. Kila mtu sasa na ajihisi kama mvumbuzi, mtafiti na mtatuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yetu. Uhodari wa kuishi si uhodari wa kuishi miaka mingi, la hasha. Ni uhodari wa kuwa msaada katika jamii inayokuzunguka na ulimwengu kwa ujumla wake.
Lakini yote katika yote, tunahitaji kuandika upya historia mpya ya maisha yetu na Taifa letu. Hannibal [183-247] mgunduzi wa silaha za kivita anatushauri hivi, ‘Lazima tuone njia kama haipo tuitengeneze’. Tanzania inahitaji kipindi cha ufahamu. Hiki kipindi naweza kukipachikia jina la falsafa ya ufahamu (Philosophy of consciencism).
Falsafa ya ufahamu ni falsafa inayotoa mtazamo mzima juu ya ufahamu wa Taifa letu lianzie wapi na liwezeje kujiendeleza kiuchumi, kisisa, kijamii, na kiutamaduni. Mawazo ya Hegel yanasema, ‘Haitoshi tu kuufahamu ulimwengu ulivyo bali ni kubuni mawazo yanayoweza kuuongoza ulimwengu’.
Katika historia yote ya kuyatafakari mawazo ya mwanadamu na mifumo ya miundo yake, wanafikara adhimu karibu wote dunini wanakubaliana kuwa tendo la kuelewa hususani kufikiri huwezekana tu katika mfumo wa udhanishaji wa mawazo jumla (universal concepts).
Waafrika na walimwengu kwa ujumla wanastaajabia mapinduzi makubwa ya kiuchumi ya taifa la China na wanajenga hoja kwamba tuwaige Wachina lakini wanashindwa kufahamu kuwa kile tunachokiona kwa Wachina leo hii ni matokeo ya akili na uwezo wao wa kuyafikiri mambo kwa kina na kuyaumba kwa vitendo.
Hegel anasema “Mifumo yote ya kiuchumi na kijamii ni ujielezo wa ulimwengu wa akili wa jamii husika”. Naye Plato anasema “Kile kionekanacho katika matukio ni kivuli cha ulimwengu wa fikara wa jamii husika”. Ni hakika kwamba ulimwengu tulionao uko huru kutokana na mategemeo na matarajio yetu.
Hata hivyo, ni pale tu ambapo tutautambua huo ulimwengu, ndipo tutakapojitambua na sisi wenyewe. Kwa muktadha huo tutambua tunajua nini na nini hatujui, tunakosa nini na nini hatukosi, tunataka nini na nini hatutaki, njia ipi inafaa kupita na njia ipi haitufai kupita.
Falsafa inatufundisha kwamba, ukweli halisi hauko katika dunia ya vitu mwonekano.Vitu mwonekano ni vivuli vya vitu halisi na vitu halisi vinaishi katika dunia ya uwazo. Bila elimu bora ni ndoto kwa Watanzania kuishi kwenye dunia ya uwazo.
Kwa muda mrefu Watanzania tumekuwa mateka wa kifikra kwa sababu ya mfumo wetu mbovu wa elimu. Tujitahidi sana kukilea hiki kizazi chetu katika misingi ya kifalsafa ili kisiwe mateka wa fikra.
Ninaomba kutamatisha makala yangu kwa kukubaliana na Libba Bray kwamba, ‘Hatuwezi kurudi nyuma. Tunaweza tu kwenda mbele’. Tanzania bila imani za uchawi inawezekana. Afrika bila dhana ya uchawi inawezekeza. Mungu ibariki Afrika watu wake wafikiri vyema.
0719 700446