DAR ES SALAAM
Na Ludovick Utouh
UTANGULIZI:
Juni 10, 2021, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, aliwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Hii ni Bajeti ya kwanza chini ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano; 2021/22 – 2025/26 na Bajeti ya kwanza ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan yenye dhima ya ‘Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu’.
Taasisi ya WAJIBU imefanya uchambuzi wa Bajeti pendekezwa kwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji na utawala bora hivyo kuja na maoni, changamoto na mapendekezo yanayolenga kuboresha ukamilishaji wa bajeti hii.
Makadirio ya mapato na matumizi yameweka malengo ya jumla kama ifuatavyo:
a) Kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuweka mazingira rafiki kwa mlipakodi kwa lengo la kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogo ndogo na za kati ili kupanua wigo wa kodi;
b) Kuboresha mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa kodi ili kupanua wigo wa kodi;
c) Kuimarisha uendeshaji wa mashirika ya umma ili yaweze kufanya kazi kibiashara;
d) Kuongeza uzalishaji wa mazao yatokanayo na sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi;
e) Kuboresha kilimo cha umwagiliaji, kuongeza mnyororo wa thamani na masoko ya mazao ya kilimo;
f) Kuchochea uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia (transfer of technology) kutoka nje;
g) Kuchochea uwekezaji hasa katika viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini;
h) Kupambana na utoroshaji wa madini na kujenga mitambo ya uchenjuaji madini nchini pamoja na viwanda vya kuongeza thamani katika madini yanayozalishwa nchini, zikiwamo jitihada za makusudi za kuwajengea uwezo zaidi wachimbaji wadogo katika ushiriki wao kwenye sekta hii ya uziduaji;
i) Kuboresha miundombinu ya sekta za usafirishaji na nishati;
j) Kuboresha utoaji huduma za kijamii hasa katika sekta za afya, elimu na maji; na
k) Kuimarisha ushirikiano wa nchi yetu na nchi jirani, kanda na kimataifa.
MIKAKATI YA KUONGEZA MAPATO
Mikakati iliyoainishwa kuchukuliwa na serikali ili kuboresha usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ni:
a) Kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini;
b) Kuboresha mazingira yatakayochochea ulipaji kodi wa hiari;
c) Kuongeza matumizi ya TEHAMA (ikiwemo usalama wa mifumo [systems security]) katika usimamizi wa makusanyo ya rasilimali za umma (mfano mifumo ya GePG, MUSE);
d) Kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi;
e) Kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato;
f) Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato;
g) Kuendelea kuwianisha na kufuta au kupunguza viwango vya kodi, tozo na ada kero; na
h) Kusimamia ukusanyaji wa mapato yote ya serikali ili kuhakikisha yanawasilishwa moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kulingana na matakwa ya Katiba ya JMT ya 1977 (kama ilivyorekebishwa) na Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 (kama ilivyorekebishwa).
MIKAKATI YA KUDHIBITI MATUMIZI
Ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utawala bora kwenye matumizi ya mapato ya serikali, Serikali inatarajia:
a) Kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yatakayochochea ukuaji wa uchumi na kuhakikisha kuwa miradi inayoendelea inapewa kipaumbele kabla ya miradi mipya kuanzishwa;
b) Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa kuendana na vigezo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
c) Kudhibiti uzalishaji na ulimbikizaji wa madeni;
d) Kuendeleza nidhamu ya matumizi ya fedha za umma katika ngazi zote za serikali na taasisi zake; na
e) Kuongeza matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.
UCHAMBUZI WA BAJETI YA MWAKA 2021/22
Kwa mwaka 2021/22, serikali imeendelea kutenga asilimia 63 ya bajeti yake katika matumizi ya kawaida na kuelekeza asilimia 37 ya bajeti katika matumizi ya maendeleo kama ilivyokuwa mwaka 2020/21.
Mapato kutoka vyanzo vya ndani yameongezeka kutoka asilimia 69 mwaka 2020/21 hadi asilimia 72 mwaka 2021/22 hivyo kupunguza utegemezi kwa misaada na mikopo kwa asilimia 3. Mchanganuo wa mapato ya serikali kwa mwaka 2021/22 ni kama ifuatavyo:
i. Mapato ya Ndani (yakijumuisha Halmashauri); 72%
ii. Mikopo na Misaada (kutoka ndani na nje); 20%
Mbali na kuwa Deni la Taifa ni himilivu, kuhudumia deni hilo imeendelea kuwa matumizi makubwa ya serikali (asilimia 29 ya Bajeti ya Taifa). Hii inaonyesha ukubwa wa gharama za kukopa ikilinganishwa na ukusanywaji wa mapato ya taifa hasa kutokana na gharama zinazosababisha kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.
Hali hii inalazimu nchi kuongeza vyanzo vipya vya mapato pamoja na kutegemea zaidi misaada na ukopaji wa madeni yaliyo na riba nafuu ili kukabiliana na gharama za kuhudumia Deni la Taifa.
Kiasi cha makadirio ya mapato 36.33; 100% Kuhudumia Deni la Taifa 10.66; 29%
Mishahara 8.15; 22% Kiasi kinachobaki 17.52; 48%
MUONO WA UJUMLA KUHUSU BAJETI
Bajeti ina viashiria vya kusaidia kukuza uchumi kwa kuhusianisha uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji.
Serikali inaonyesha lengo la kulinda viwanda vya ndani kwa kupunguza ushindani wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi kwa kupunguza kodi kwa baadhi ya malighafi zinazopatikana ndani ya nchi.
Kupandisha kiwango cha chini cha idadi ya waajiriwa wanaostahili kulipiwa tozo (SDL) kutoka 4 wa sasa hadi 10 kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wa tozo waajiri wenye idadi ndogo ya waajiriwa na kuchochea ukuaji wa uwekezaji nchini.
Bajeti inaashiria kuboresha hali ya kiuchumi kwa jamii kwa kuongeza wigo wa kipato kinachotokana na mshahara kwa kupunguza kiwango cha wastani wa kodi ya PAYE kutoka asilimia 9 hadi 8, kupandisha vyeo watumishi na kupunguza muda wa mkataba (kutoka 12 – 6) kwa watumishi wa Jeshi la Polisi.
Bajeti inaonyesha eneo la kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa limetengewa kiasi cha Sh trilioni 7.44. Miradi ya kielelezo imetengewa Sh trilioni 3.13 na miradi mingine imetengewa Sh trilioni 4.31. Maeneo mengine yenye umuhimu katika kukuza uchumi yaliyotengewa bajeti ni:
a) Ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini pamoja na kuzalisha bidhaa zitakazotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana nchini, Sh trilioni 1.3;
b) Kuboresha Biashara na Uwekezaji (Blueprint) Sh bilioni 31.6;
c) Kuchochea maendeleo ya watu Sh trilioni 4.43; na
d) Kuendeleza rasilimali watu Sh bilioni 50.5.
BAJETI INAJIBU MAPENDEKEZO YALIYOTOLEWA KATIKA KAGUZI ZA MIAKA ILIYOPITA?
Mapendekezo ya Bajeti ya Taifa ya mwaka 2021/22 yanaonyesha kuzingatia baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa katika kaguzi za miaka iliyopita zilizofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ili kuendelea kukuza uwazi, uwajibikaji na utawala bora katika usimamizi wa makusanyo na matumizi ya rasilimali za umma, serikali haina budi kuzingatia mapendekezo yanayotolewa na taasisi za udhibiti (mfano CAG, PPRA, TRA, TAKUKURU n.k) katika upangaji wa bajeti.
Katika mapitio ya bajeti ya mwaka 2021/22, Taasisi ya WAJIBU imebaini mambo kadhaa ambayo yamezingatia mapendekezo ya kaguzi za miaka iliyopita:
a) Mabadiliko ya Sheria ya Ukaguzi wa Umma SURA 418;
– Mabadiliko haya yatafanya mashirika yote yanayomilikiwa na serikali moja kwa moja au kupitia taasisi zake sasa kukaguliwa na CAG (Pendekezo la CAG ukaguzi wa Benki ya Azania mwaka 2014/15).
– Kumwezesha Waziri mwenye dhamana ya Fedha kuwasilisha bungeni majibu kuhusu taarifa ya CAG kwenye kikao kinachofuata cha Bunge baada ya CAG kuwasilisha taarifa yake badala ya utaratibu wa sasa unaotaka taarifa zote kuwasilishwa kwa pamoja katika kikao kimoja cha Bunge.
(Hii ilitokana na mabadiliko ya Sheria ya Ukaguzi wa Umma mwaka 2013 ambayo hayakutekelezeka hadi sasa).
b) Mabadiliko ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, SURA 134.
– Mabadiliko haya yatairuhusu serikali kudhamini kampuni au taasisi yoyote ya umma kukopa kiasi kisichozidi thamani ya Hisa za Serikali ya Tanzania kwenye kampuni au taasisi husika baada ya kupata ridhaa ya Baraza la Mawaziri. (Hii inajibu hoja ya CAG ya upungufu wa mitaji kwa mashirika yanayomilikiwa na serikali).
c) Serikali kulipa madeni yanayodaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kutenga fedha kwenye bajeti na kutumia utaratibu wa kutoa hatifungani maalumu isiyo taslimu (Non-cash Special Bonds) zitakazoiva kwa nyakati tofauti kuanzia miaka miwili hadi 25.
– Hii itasaidia kuyajumuishi madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwenye Deni la Taifa na kusaidia mifuko hiyo kufanya uwekezaji wa fedha hizo.
d) Serikali kuongeza mapambano dhidi ya rushwa, udanganyifu na ubadhirifu wa mali za umma. Kila mwaka ripoti za CAG zimekuwa zikiripoti upotevu wa mali za umma hasa kutokana na rushwa, udhaifu wa mifumo ya ndani wa serikali katika ngazi zote na taasisi zake nk.
e) Mapato ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), kuanzia mwaka 2021/22, yatakuwa yakikusanywa na taasisi hizo kupitia mfumo wa GePG na kuingizwa kwenye akaunti za makusanyo (holding account) zilizopo Benki Kuu.
Mfano:
Ripoti ya CAG ilionyesha upotevu wa TZS 3.93 bilioni kutokana na miamala ya udanganyifu katika bandari ya Kigoma na Mwanza uliosababishwa na udhaifu wa mifumo ya ndani katika usimamizi wa malipo.
CHANGAMOTO
Katika kutekeleza bajeti pendekezwa, WAJIBU inaona changamoto zifuatazo kama kikwazo katika utekelezaji wake:
a) Ingawa serikali imeonyesha dhamira ya wazi kulinda viwanda vya ndani kupitia kupunguza viwango vya kodi, hatua hizi zisitumike kulinda udhaifu wa kiutendaji katika viwanda vya ndani na kuwadhuru walaji kwa kuwapunguzia uhuru wa uchaguzi wa bidhaa kuendana na thamani na ubora wa bidhaa katika soko;
b) WAJIBU inaipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kutumia PPP kama njia mojawapo ya kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo. Hata hivyo, WAJIBU inaona kuna umuhimu wa kuifanyia marekebisho Sheria ya PPP ya mwaka 2010 ili kufanikisha mpango huo;
c) Kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta kunakotokana na ahueni ya ugonjwa wa UVIKO – 19 duniani, hali hii itaongeza bili ya uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi;
d) Serikali inaendelea kuwekeza katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo. Miradi hii inatekelezwa kwa kupitia fedha nyingi za mikopo kutoka nje ya nchi.
WAJIBU inaona changamoto ya serikali kutokuwa na fedha za kigeni za kulipa madeni hayo.
e) Serikali bado inakabiliwa na changamoto ya ufanisi duni katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa matumizi na utoaji huduma; Baadhi ya changamoto hizo ni:
– Kutokuwa na muingiliano katika Mifumo ya TEHAMA, – Uwepo wa mifumo inayofanya kazi zinazofanana, – Kutofanya kazi ama kutokuwepo kwa baadhi ya moduli katika mifumo ya TEHAMA, na
– Utekelezaji duni wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016.
f) Madhara ya uwepo wa UVIKO – 19 katika shughuli za kiuchumi nchini; na
g) Marekebisho ya Kanuni Na. 15 ya Ukokotoaji wa Kodi za Kimataifa (Transfer Pricing Regulations) kwa kufuta kifungu kinachoweka adhabu ya asilimia 100 kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya sheria.
– Marekebisho haya yatatoa mwanya kwa wafanyabiashara kukwepa kodi kupitia eneo hili (Transfer Pricing Regulations).
MAPENDEKEZO
Ili kuwa na uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa Bajeti pendekezwa, WAJIBU inashauri yafuatayo:
a) Mbali na kuwa Deni la Taifa ni himilivu, kulihudumia deni hilo imeendelea kuwa matumizi makubwa ya Serikali (asilimia 29 ya Bajeti ya Taifa). Hivyo, WAJIBU inashauri yafuatayo yafanyike:
– Serikali kuongeza vyanzo vipya vya mapato;
– Serikali kuboresha mahusiano na nchi wahisani ili kupata misaada katika kugharamia Bajeti ya nchi; na
– Serikali kukopa mikopo yenye riba nafuu (Concessional Loans).
b) Ni wazo zuri kutumia mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Hususan pendekezo la serikali la kukusanya tozo ya pango kupitia ununuzi wa umeme kupitia LUKU, WAJIBU inapendekeza yafuatayo:
– Ili kuondoa uwezekano wa vitendo vya rushwa kushamiri kutokana na uwepo wa ‘Discretional decisions’ katika kuamua mtumiaji gani alipe kiasi gani, serikali iweke kiwango kimoja kwa wote lakini kilipwe kulingana na matumizi.
– Serikali kuweka mfumo mbadala ili kusaidia pale mfumo mkuu ukishindwa kufanya kazi,
– Serikali kuongeza ulinzi wa mifumo ya TEHAMA.
– Serikali kuhakikisha kuwa kanzidata na seva za mifumo ya TEHAMA zinasimamiwa na kumilikiwa na taasisi za serikali ndani ya nchi.
c) WAJIBU inaona umuhimu wa kuifanyia marekebisho Sheria ya PPP ya mwaka 2010 ili kufanikisha utekelezaji wa Bajeti pendekezwa.
Mfano wa changamoto zinazohitaji marekebisho ni:
– Anayegharamia upembuzi yakinifu analazimika kuingia kwenye ushindani ili kutekeleza mradi. Hii inahatarisha uwekezaji wa kwanza endapo aliyegharamia upembuzi yakinifu atashindwa kupata zabuni hiyo.
d) Ripoti zote za utendaji wa taasisi za udhibiti nchini (TAKUKURU, Msajili wa Hazina, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma) ziwe zinawasilishwa bungeni ili kujadiliwa na kufanywa kuwa taarifa za wazi (public documents) kwa wananchi.
e) Serikali kupitia TRA, Benki ya Tanzania na TCRA kufanya uwekezaji mkubwa katika kujenga uwezo wa kutambua na kutoza kodi biashara zinazofanyika kwa njia ya mtandao ambazo zinakua kwa kasi kubwa sana nchini.
f) Ripoti zinazotolewa na CAG (Management Letters) kwa maofisa masuuli na Bodi za Wakurugenzi na Bodi za Ushauri za taasisi za serikali ambazo hivi sasa ni siri, ziwe wazi kwa umma. Ikumbukwe kuwa watumishi wa umma wanasimamia tu rasilimali za umma kwa niaba ya wananchi ambao ndio wamiliki wa rasilimali hizo, hivyo wana haki ya kufahamu udhaifu uliobainishwa na CAG katika usimamizi wa rasilimali zao.
g) Bunge kupitia Kamati yake ya Kudumu ya Bajeti kufanya usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa Bajeti itakayoidhinishwa ili ifikie malengo yaliyokusudiwa. Hii ni pamoja na kupitia na kujadili ripoti za utekelezaji wa bajeti za robo mwaka zinazotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango; na
h) Serikali ianze majadiliano ya mauziano ya bidhaa na huduma za ziada zitakazotokana na miradi ya kimkakati nje ya nchi (mfano umeme, usafirishaji wa mizigo kupitia SGR). Hii itasaidia kuihakikishia serikali kuwa na fedha za kigeni za kuhudumia madeni yanayotokana na miradi hiyo pindi yatakapoanza kulipwa.
i) Serikali ihakikishe inaziongezea uwezo (rasilimali watu, miundombinu na fedha) Mahakama za Usuluhishi wa Kodi ili ziweze kusikiliza na kuamua mashauri ya kodi ambapo hivi sasa kuna Sh trilioni 360.08 na Dola za Marekani milioni 181.43 viporo vya kufanyiwa uamuzi ili serikali iweze kupata mapato stahiki kutoka katika mashauri hayo.
j) Serikali kupunguza idadi ya miradi inayopangwa kutekelezwa kwa mwaka ili kuipa nafasi serikali kutenga kiasi kikubwa zaidi katika kutekeleza miradi michache ambayo itakamilika kwa wakati.
k) WAJIBU inaipongeza serikali kupunguza muda wa miaka 12 hadi 6 wa watumishi wa Jeshi la Polisi kupata mafao yatokanayo na utumishi wao. Hata hivyo, WAJIBU inaishauri serikali kuondoa kabisa muda wa miaka (6) kwa watumishi wa Jeshi la Polisi ili kuwapa haki ya kupata mafao yanayotokana na utumishi wao. Utaratibu huu unawanyima watumishi wa Jeshi la Polisi haki ya kuanza kufaidi kupata mafao mara wanapothibitishwa kwenye ajira zao kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na binafsi.
HITIMISHO
WAJIBU inaipongeza serikali kwa kukamilisha uandaaji wa bajeti ya mwaka 2021/22 pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa mfano kodi ya laini za simu, hatifungani za manispaa pamoja na tozo ya pango kupitia LUKU za umeme. WAJIBU inatambua nia thabiti ya serikali kuongeza wigo wa mapato hasa kutokana na vyanzo vipya vilivyoibuliwa katika mapendekezo ya bajeti hii.
Bajeti inayopendekezwa, inalenga kukuza uchumi na kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja, hivyo kupunguza umaskini nchini. WAJIBU inaamini, mapendekezo yaliyotolewa yatazingatiwa na kufanyiwa kazi na Serikali na Bunge katika kukamilisha utayarishaji wa bajeti ya mwaka 2021/22.