Na Mwandishi Wetu
Chama kikuu cha upinzani nchini Chadema kimetangaza kususia kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusaini kanuni hizo kwa niaba ya chama ametangaza kupitia mtandao wa X kuwa hatua ya chama hicho kutohudhuria hafla ya utiaji saini kanuni hizo unaofanyika leo Jumamosi mjini Dodoma chini ya uratibu wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) nchini.
Kati ya vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa Tanzania, 18 vimesaini kanuni hizo, na Chadema pekee ndicho kilichosusia.
“Katibu Mkuu @ChademaTz sitakuwepo kwenye kikao cha tarehe 12 Aprili 2025 cha kushauriana na kusaini maadili ya uchaguzi ya 2025.”
Ifahamike kuwa mwenye mamlaka ya kusaini maadili ya uchaguzi kwa niaba ya chama cha siasa ni Katibu Mkuu.
“Katibu Mkuu sijateua kiongozi au afisa yoyote kwenda kushiriki kwa niaba yangu katika kikao hicho kitakachofanyika katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi @TumeUchaguziTZ
Mkoani Dodoma,” ametangaza Mnyika kupitia mtandao wa X.
Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema kimetangaza kususia kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kati ya vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa Tanzania, 18 vimesaini kanuni hizo, na Chadema pekee ndicho kilichosusia.
“Katibu Mkuu @ChademaTz sitakuwepo kwenye kikao cha tarehe 12 Aprili 2025 cha kushauriana na kusaini maadili ya uchaguzi ya 2025.”
Ifahamike kuwa mwenye mamlaka ya kusaini maadili ya uchaguzi kwa niaba ya chama cha siasa ni Katibu Mkuu.
Kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi ni takwa la kisheria na moja ya maandalizi muhimu ya uchaguzi mkuu ambao unahusisha kinyang’anyiro cha nafasi za udiwani,ubunge na urais.
Jana Ijumaa, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima alitahadharisha katika mahojiano na runinga ya UTV ya Tanzania kuwa chama ambacho hakitasaini kanuni za maadili hakitashiriki katika uchaguzi wa Oktoba 2025.
“Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi…maadili hayo yanapaswa kusainiwa, kuzingatiwa na kutiiwa na chama cha siasa, mgombea, Tume na serikali. Sasa kama kuna chama cha siasa hakitasaini maadili hayo kesho hakitapata fursa ya kusimamisha mgombea,” alisema Kailima ambaye anaripotiwa kusisitiza kauli yake hiyo leo huko Dodoma.
‘No reforms, no election’
Msemaji wa Chadema, Brenda Rupia ametoa taarifa kwa umma akisema hatua hiyo ya kutosaini kanuni za maadili hii leo imetokana na kile alichodai kuwa ni kutokujibiwa kwa barua yao iliyotumwa Disemba 2024 kuhusu “mapendekezo na madai ya msingi ya Chadema kuhusu mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.”
Kwa mujibu wa Bi Rupia, ukimya wa tume “unathibitisha kukosekana kwa nia ya dhati ya kufanya mashauriano ya kweli na uwazi kuhusu mchakato wa uchaguzi.
Chadema tayari ipo katika kampeni ya ‘No reforms, no election’ ikimaanisha bila mabadiliko, hakuna uchaguzi. Kampeni hiyo ambayo imekuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu inalenga ‘kuzuia’ uchaguzi kufanyika endapo matakwa ya chama hicho hayatatekelezwa.
Lissu alishtakiwa kwa uhaini juzi Alhamisi akituhumiwa kuchochea uasi. Mashtaka hayo yanatokana na moja ya kauli zake aliyoitoa kuhusu kuzuia uchaguzi.
Makamu mwenyekiti wa Chadema, John Heche ametangaza kuwa kampeni hiyo itaendelea licha ya mwenyeliti Lissu kuwa mahabusu.
Chadema inaamini bila mabadiliko ya kimfumo, uchaguzi wa Oktoba 2025 hautakuwa huru na wa haki, madai yanayopingwa vikali na chama tawala cha CCM pamoja na serikali.
