Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; imedaiwa kuwa anaendesha kampeni kali ‘kimyakimya’ kuhakikisha anateuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania kiti cha urais mwaka huu.
Habari za kiuchunguzi zisizotiliwa shaka ilizozipata Gazeti la JAMHURI, zinaonesha kuwa Membe amesuka mkakati mzito na sasa amekubalika katika mioyo ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, na anaungwa mkono na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Membe amepata uungwaji mkono wa Mzee Mwinyi, baada ya kumhakikishia kuwa katika uchaguzi ujao iwapo CCM watamteua kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho, basi atamteua mtoto wake, yaani Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa sasa, Dk. Hussein Mwinyi, kuwa Mgombea Mwenza kutoka Zanzibar na hatimaye kuwa makamu wake wa Rais.
Katika kinachoelezwa kuwa ni mpango mkakati wa muda mrefu, fursa ya Dk. Mwinyi kutumikia kama Makamu wa Rais itakuwa tiketi ya baadaye kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, miaka 10 baadaye yaani  mwaka 2025.
Hoja mbili mwaka huo zitakazotumiwa ni kuwa Dk. Mwinyi atakuwa na uzoefu wa kutosha na itakuwa zamu ya Zanzibar kumtoa mgombea urais wakati huo, baada ya Tanzania Bara kuwa imetoa marais watatu mfululizo yaani Mkapa, Mwinyi na Mungu akipenda Membe.
“Mpango huu ni muziki unaofurahisha katika masikio ya Mzee Mwinyi, ambaye anaona familia yake itakuwa mahala salama hadi mwaka 2035, hivyo nilivyomwangalia amekubali kumuunga mkono Membe kwa kila hali,” amesema mtoa habari wetu.
Kwa upande wa Mzee Mkapa, inaelezwa kuwa aliyefanikisha mpango wa Mkapa kumuunga mkono Membe ni Balozi Costa Mahalu aliyewakutanisha wawili hao.
“Wamekutana na kuzungumza kwa zaidi ya saa 3. Mzee Mkapa aliuliza maswali mengi ya msingi yakiwamo ya kiuchumi, kimataifa na uhusiano wa kijamii, ambapo Membe aliyajibu na kumshawishi, kisha akasema hana pingamizi katika ombi lake,” kinasema chanzo kingine cha JAMHURI.
Taarifa za uhakika zinasema kwamba tayari vimekuwapo vikao vingi, ila vitatu vya uamuzi vimeketi kati ya Januari na Februari, mwaka huu kufanikisha mpango wa Membe kuwania nafasi hiyo nyeti kumpokea kijiti Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake Oktoba, mwaka huu.
Kwa mujibu wa mtoa habari kutoka kambi ya Membe, vikao vimeketi Zanzibar (kimoja) na viwili jijini Dar es Salaam vikiongozwa na Mkapa na kukubaliana kuwa Mgombea Mwenza wa Membe atakuwa Dk. Mwinyi.
Kikao cha Zanzibar kilifanyika katika Hoteli ya Bawani, wakati vile vya Dar es Salaam vimeketi Hoteli ya Courtyard na nyumbani kwa Jack Gotham, Mbezi Beach Dar es Salaam. Gotham ni mfanyabiashara na mdau mkubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kikao cha kwanza kilifanyika baada ya sherehe za Mapinduzi Zanzibar mwaka huu. Kikao hicho kilifanyika katika Hoteli ya Bwawani ambako pamoja na mambo mengine ilielezwa kuwa majina mawili ya mgombea mwenza wa Membe yaliwekwa mezani.
Majina hayo, mbali ya Dk. Mwinyi, pia alitajwa Waziri Kiongozi wa zamani wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha.
“Mwisho walikubaliana Dk. Mwinyi awe mgombea mwenza,” anasema mtoa taarifa na kuongeza kuwa kikao hicho kiliendelea kwenye Hoteli ya Courtyard Dar es Salaam, Februari 21, mwaka huu.
Kikao kingine kilifanyika siku mbili baadaye nyumbani kwa Jack Gotham huko Mbezi Beach Dar es Salaam ambako pia taarifa iliwasilishwa ikisema Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, ameridhia mwanaye kuwania umakamu wa rais.
 Katika timu hiyo, Dk. Mwinyi ametajwa kuwa amekubali ateuliwe kuwa mgombea mwenza na hatimaye Makamu Rais wa Membe huku Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Mwinyi, ambaye ni baba wa Dk. Mwinyi akiridhia mpango huo bila kinyongo.
Dk. Mwinyi alizungumza na JAMHURI wiki moja iliyopita kuhusiana na harakati hizi, lakini bila kutaka kuingia kwa ndani akasema: “Hapa nipo kwenye msiba, nahifadhi mwili wa (John) Komba hapa Lugalo. Nitafutieni kesho (Jumapili).”
 Tangu wakati huo juhudi za kumpata Dk. Mwinyi zimegonga mwamba, lakini wakati anazungumza na JAMHURI hakukanusha wala kuthibitisha uwapo wa mpango huu, na sauti yake ilisikika kujaa unyenyekevu uliosheheni matumaini.
Taarifa zinasema hata Rais Jakaya Kikwete anaunga mkono timu hiyo kwani katika kikao cha tatu kilichoketi nyumbani kwa Gotham, Rais Mwinyi pia alihudhuria na taarifa ya Kikwete kuwa ‘pamoja nao’ iliwasilishwa.
Taarifa zinasema hofu pekee ya kambi ya Membe kupata urais ni jina la Edward Ngoyai Lowassa ambalo ulikuwapo mpango wa kujadili suala hili katika kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichoketi wiki moja iliyopita jijini Dar es Salaam, lakini ilishindikana kutokana na shinikizo la baadhi ya wajumbe.
Wajumbe hao wakiongozwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) waliungana pamoja na kutaka haki sawa kwa watuhumiwa wote wanaodaiwa kuanza kampeni mapema kabla ya kufungiwa mwaka mmoja wakiwekwa kwenye ‘chungu kimoja’ cha uangalizi.
Vijana hao wa UVCCM wanasema kwamba walipata taarifa za mipango ya kukatwa majina ya makada wengine ambao ni January Makamba, William Ngeleja na Steven Wasira wakasema ‘patachimbika.’
Akina Lowassa na Membe walitiwa hatiani na Kamati Ndogo ya Nidhamu ambayo iliwataka kutojihusisha na shughuli za kijamii kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu Februari 18, mwaka jana.
Hoja ya vijana hao ni kuwa kama Membe na Lowassa ndiyo wagombea wenye nguvu, basi waachiwe huru wachuane kwa wajumbe na hatimaye kwa wananchi bila Lowassa au Membe kukingiwa kifua na yeyote, ambapo hatimaye mshindi halali atapatikana.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Membe hakuishia kwa Mwinyi na Mkapa pekee. Tangu mwaka huu umeanza, kimyakimya amekutana na aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa David Msuya, kuomba amuunge mkono.
Mbali na Msuya amekutana na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza mstaafu mwingine, Jaji Joseph Sinde Warioba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na pia amekutana na Mzee Peter Kisumo, ambaye ni mmoja kati ya waasisi wachache wa Taifa hili waliodai uhuru. Wote hawa wameonesha nia ya kumuunga mkono.
JAMHURI ilipowasiliana na Membe, alikiri kukutana na Mzee Mkapa, lakini akasema ajenda haikuwa urais: “Haya mambo yanashangaza yanavyokwenda kasi. Mimi unajua nimefungiwa kushiriki siasa, lakini sijazuiliwa kufanya kazi nyingine au kukutana na watu.
“Ni kweli nilikutana na Mzee Mkapa, tena kweli alikuwapo Balozi Mahalu, na inashangaza kuona mna taarifa zinazofanana na ukweli, lakini uhalisia zimechezewa kidogo. Kile kikao tulichokutana hakikuwa cha kisiasa, bali tulikuwa tunajadili jinsi ya kumaliza mgogoro wa Sudan Kusini.
“Nilitumwa kwenda kumuomba Mzee Mkapa atusaidie jinsi ya kushughulikia matatizo ya Sudan Kusini, na kweli tulikaa kwa zaidi ya saa tatu, ila tulikuwa hatuzungumzi masuala ya urais kama mlivyoambiwa. Mimi nipo kifungoni, sifanyi siasa kwa siasa kwa sasa kaka,” anasema Membe.
Alipoulizwa juu ya mkutano na Dk. Mwinyi Zanzibar, alisema: “Jamani ile ilikuwa tunaadhimisha Mapinduzi Matukufu. Nilikutana si na Dk. Mwinyi tu, bali nilikutana na watu wengi tukawa tunajadili historia yetu na kwa nia njema kabisa tunajadili mustakabali wa Taifa yenye amani, wala pale napo hazikuwa siasa.”
Juu ya kukutana na Mzee Mwinyi, Kisumo, Warioba na Msuya, alisema: “Kwa mtu mwenye tabia ya kuheshimu wazee wetu waliolitumikia Taifa letu kwa unyenyekevu ni lazima uwe na tabia ya kuwatembelea na kuwasalimia, sidhani kama nyie hamtembelei wazee ambao ni ndugu au jamaa na marafiki. Na sidhani mnapowatembelea mnakuwa mmekwenda kufanya siasa. Sidhani.”
Makada waliopewa adhabu ya kuwa chini ya uangalizi mbali na Lowassa na Membe ni William Ngeleja, January Makamba, Stephen Wasira na Frederick Sumaye.
Wakati hao wakiwa na adhabu yao imeongezwa kwa muda usiojulikana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda tayari ametangaza ‘kimyakimya’ kugombea urais mwaka huu. Wengine waliotangaza nia ya kugombea urais ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla.
Mwingine ni Stephen Wasira, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Dk. John Pombe Magufuli, Januari Makamba na alikuwa akitajwa Profesa Anna Tibaijuka, ambaye mgawo wa escrow umetia doa ndoto yake hiyo, na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa (zamani), Dk. Asha Rose Migiro.
Oktoba mwaka huu, Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu ambapo sasa ikiwa ni takribani miezi saba kabla ya uchaguzi, joto na nani atateuliwa na chama tawala au vyama vya upinzani kupeperusha bendera na hatimaye kuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kitendawili kigumu.