Baada ya mbio ndefu za uchaguzi mdogo wa ubunge na Udiwni katika majimbo yote yaliyofanyika uchaguzi hatimaye matokeo yametoka ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepata ushindi wa kishindo na kuwaacha mbali vyama vya upinzani.
Akitangaza matokeo katika jimbo la Songea Mjini, msimamizi wa uchaguzi, Tina Sekambo amemtangaza Dkt Damas Ndumbaro kuwa mshindi kwa kupata kura 45,762 sawa na 97%.
Wagombea wengine ni Christina Thinangwa wa CUF amepata kura 608 huku Neema Tawete wa ADA-TADEA akipata kura 471 na kubainisha kuwa waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 28,841.
Katika jimbo la Singida Kaskazini ambalo liliachwa wazi na Lazaro Nyalandu CCM imerudisha jimbo hilo,ambapo msimamizi wa uchaguzi, Rashid Mandoa amemtangaza mgombea Justine Monko (CCM) kuwa mshindi baada ya kupata kura 20,857 sawa na 93.5%.
Matokeo ya wagombea wengine ni Dalphine Mlewa wa CUF kura 974, Aloyce Nduguta wa Ada-Tadea kura 265, Omar Sombi wa AFP kura 116 na Mchungaji Yohana Labisu wa CCK kura 86.
Mandoa amesema kura zilizopigwa ni 22,298, waliojiandikisha kupigakura ni 91,518, watu 69,220 ambao ni zaidi ya asilimia 70 hawakujitokeza kupiga kura.
Na kwa upande wa jimbo la Longido msimamizi wa uchaguzi, Jumaa Mhina amemtangaza Dkt. Stephen Kiruswa kuwa mshindi baada ya kupata kura 41,258 sawa na 99.1% .
Katika nafasi za udiwani pia CCM wamepata ushindi katika majimbo yafuatayo
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kiti cha Udiwani katika Kata ya Kurui Wilaya ya Kisarawe, Pwani baada ya mgombea wake, Mussa Kunikuni kupata kura 632 na kumzidi mgombea wa CUF mwenye kura 185.
Pia Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kiti cha Udiwani katika Kata ya Kimandolu Arusha, baada ya mgombea wake, Gaudence Lyimo kupata kura 8,981 na kumzidi mgombea wa CUF aliyepata kura 1,251.