Republican presidential candidate Donald Trump, left, stands with Democratic presidential candidate Hillary Clinton at the first presidential debate at Hofstra University, Monday, Sept. 26, 2016, in Hempstead, N.Y. (AP Photo/ Evan Vucci)

Republican presidential candidate Donald Trump, left, stands with Democratic presidential candidate Hillary Clinton at the first presidential debate at Hofstra University, Monday, Sept. 26, 2016, in Hempstead, N.Y. (AP Photo/ Evan Vucci)

Huku siku za kampeni nchini Marekani zikiwa zimekwisha, ushindani mkali unaonekana kati ya Hillary Clinton wa Democratic na Donald Trump wa Republican, hali inayoashiria ugumu katika uchaguzi huo.

Wagombea hao – Hillary Clinton na Donald Trump – wamefanya mikutano sambamba ya kampeni North Carolina, jimbo ambalo kila mmoja lazima ashinde kama akitaka kwenda Ikulu ya Marekani (White House) wiki hii.

Katika mikutano hiyo, kila mgombea amejaribu kuwavutia wapiga kura kwa kuweka wazi sera huku kila mmoja akijitahidi  kumpiga kijembe mpinzani wake kwa kuonesha udhaifu wake anaodhani unaweza kumpunguzia uungwaji mkono. 

Wakati wagombea hao wakiendelea kunyukana, mpinzani wa zamani wa Clinton, Seneta Bernie Sanders, ameweza kumtambulisha mgombea huyo huko Raleigh, North Carolina karibu na alipokuwa Donald Trump akifanyia mkutano wake.

Wote walishambuliana kwa maneno ya kudhalilisha uwezo wa kila moja wao kufanya kazi huku kila moja akijaribu kuwavutia wapiga kura wake na kueleza huu ni wakati muhimu katika historia ya Marekani.

Awali, huko Greenville North Carolina, Clinton alionya kwamba Trump ni mtu anayeweka mbele maslahi yake bila ya kujali nani ataumia.

Clinton kwa mara nyengine tena amepata nguvu kutoka kwa Rais Barack Obama ambaye amekuwa na mwendelezo wa kumpigia kampeni.

Obama alifanya kampeni kwa ajili ya Hillary Clinton wiki iliyopita huko Chapell Hill North Carolina, eneo linaloelezwa pia kuwa na ushindani mkubwa na jimbo muhimu kwa wagombea hao.

Katika kampeni hiyo, Obama anasema hakuona kama nchi ingekuwa hatarini kama angeshindwa katika uchaguzi dhidi ya John McCain mwaka 2008 au Mitt Romney 2012, miaka michache iliyopita lakini si kwa mtu kama Trump.

Aliwaonya wapiga kura wa North Carolina kutoridhika na kufikiri kura zao hazina umuhimu, na kusema kubaki nyumbani siku ya upigaji kura kutawasaidia wale wanaotaka kuzuia sauti zao na wasioitakia mema Marekani.

“Nahitaji kila mtu kufahamu kwamba kila jambo tulilofanya linategemea na mimi kuweza kupeleka tochi kwa mtu ambaye anaamini katika mambo kama yale tunayoyaamini sisi kama Wamarekani wote,” anasema Obama.

Wakati kampeni hizo zikiwa zimefika ukingoni, kura za maoni za urais nchini humo siku chache zilizopita zimekuja na habari njema kwa kambi ya mgombea urais wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton.

Clinton aliungwa mkono na asilimia 43 ya wapiga kura waliohojiwa katika utafiti huo ulioendeshwa kwa pamoja na mashirika ya habari ya NBC na The Wall Street Journal, kulinganisha na Trump aliyepata asilimia 37 ya kura.

Mgombea urais wa chama cha Libertarian, Gary Johnson ameendelea kushikilia nafasi ya tatu baada ya kupata asilimia tisa ya kura huku wa chama cha Green, Jill Stein akiambulia asilimia tatu ya kura hizo.

Awali, baada ya mkutano mkuu wa Democratic Julai mwaka huu, kura za maoni zimekuwa zikionesha Clinton anaongoza kwa asilimia 10 kabla ya wiki za karibuni wagombea hao kuonekana wakikaribiana, kufungana au Trump kuongoza kwa asilimia chache.

Utafiti uliofanywa na mashirika ya habari ya Fox News na CBS/New York Times wiki iliyopita, ulionesha kukaribiana kwa wagombea hao, hali ambayo wachambuzi wa kisiasa wanadai kuwa ni ngumu kutabiri nani atashinda.

Trump ameendelea kuungwa mkono kwa kiwango kikubwa na makundi ya  jamii, akiwa na asilimia 46 ya kura dhidi ya Clinton aliyepata asilimia 44, ikiwa ni asilimia ndogo mno tofauti na utafiti wa hivi karibuni.

Hali kadhalika, waliohojiwa walieleza wasiwasi kuhusu maneno na matendo ya Trump katika kampeni huku asilimia 69 wakiripoti kuwa na shaka na kampeni yake na asilimia 54 wakisema wana ‘wasiwasi mkubwa’.

 

Taarifa hii imeandaliwa kwa misaada ya mitandao ya kimataifa ya Fox News, VOA, BBC na 24news.