Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita nimeandika makala kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Nimewaandika wabunge, mmoja wao akiwa Jerry Silaa wa Jimbo la Ukonga, ambaye jimbo lake lina matatizo mengi kuliko umri wake. Kimsingi, nimechagua barabara moja tu, ambayo ni moyo wa Jiji la Dar es Salaam, kwa maana ya Jiji la Ilala.

Sitanii, kwa wasiofahamu Jiji la Dar es Salaam tangu agizo la Rais (hayati) John Pombe Magufuli Februari 24, 2021 ni Ilala. Magufuli alifariki dunia chini ya mwezi mmoja baada ya agizo hili, kwa maana alifariki dunia Machi 17, 2021. Agizo hili halijawahi kubatilishwa. Hospitali ya Mkoa wa Dar es Salaam ipo Kivule. Hadi ufike Kivule, unapitia Banana – Kitunda – Matembele kwenda mbele. Baada ya makala ya wiki iliyopita, nimepata mrejesho mkubwa. Nimeelezwa wajawazito wanapata tabu sana kwa mashimo, ambayo ni ngazi ya makorongo kwa barabara hii.

Nimeisemea barabara hii si kwa jingine, bali kutokana na mazingira kwamba inatumiwa na wagonjwa wengi. Nimemfahamu Mbunge wa Ukonga, Silaa, kitambo kidogo. Enzi hizo kabla hajawa hata Meya wa Ilala akiwa msaidizi wa Meya Abuu Jumaa.

Enzi hizo tulikuwa na mbunge Dk. Makongoro Mahanga. Aliijenga barabara hii kwa kiwango cha lami, japo kwa kilomita moja ya uhakika, nyingine tia maji. Baadaye serikali imejenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huko Kivule.

Hivi unaweza kuamini kuwa magari yanayobeba wagonjwa na wajawazito (ambulance) wanapita katika barabara hii yenye makorongo?

Nimerejea barabara hii kwani nimepata mrejesho mkubwa kutoka karibu kila Kata ya Ukonga. Hadi nikakumbushwa kuwa mwaka 2015 Jerry Silaa aliwaambia wapigakura pale Gongolamboto kuwa “Msiponipigia kura watanipigia wake zenu.” Alikiona cha moto.

Sitanii, baada ya kuandika makala hii wiki iliyopita, nimefahamishwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesaini mkataba wa kuijenga barabara hii ya Banana – Kitunda, inayounganisha barabara ya Kitunda – Kivule. Heri. Ila nimeambiwa mkandarasi ameelekezwa aanze na kuziba mashimo kabla ya kuanza ujenzi wa lami. Hili limeendelea kuwa changa la macho. Nasubiri nione uhalisia.

Sasa amenipigia mtu mmoja, akasema hivi: “Kaka hawa ndio watesi wa Rais Samia [Suluhu Hassan]. Rais Samia amefanya mambo makubwa sana kitaifa. Rais hawezi kwenda hadi mtaa au kata kufahamu barabara ina mashimo, hakuna maji, hospitali haina dawa… hawa madiwani na wabunge ndiyo kazi yao. Wanapaswa kushinda na wapigakura mitaani, hata kama ni waziri, wakapeleka haya matatizo yakatatuliwa. Jerry Silaa amejisahau tu.”

Idadi ya simu nilizopata kuhusiana na Jimbo la Ukonga na majimbo mengine nchini ni nyingi hadi nimeshangaa. Kumbe idadi ya wabunge wa sasa ambao hawatarudi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu kutokana na utendaji wao mbovu ni wengi kuliko nilivyofikiria. Napenda kuamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitajipunguzia matatizo kwa kuwakata wasiokubalika, bila kusubiri wakatwe na wapigakura.

Sitanii, wiki hii nakwenda Songea. Safari ya Songea nakwenda kwenye uchaguzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania. Sijivuni, bali nafundisha kwa mifano. Mwaka 2021 niliahidi mambo kadhaa, ikiwamo kukuza heshima ya taaluma ya uandishi wa habari nchini, wahariri wakanichagua. Nafurahi kusema yote niliyoahidi nimeyatekeleza nikaongeza hadi chenji.

Sitanii, narudia sitanii, unajua kilichotokea? Aprili 4, 2025 tunafungua Mkutano Mkuu Maalumu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa TEF.

Mgeni rasmi ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea Mwenza wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa tiketi ya CCM mwaka huu, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi. Kwa sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, naomba nikutonye!!!

Wahariri wamenipa heshima ya pekee. Hadi Ijumaa, Machi 28, 2025 kati ya wahariri wa vyombo vya habari vyote nchini unavyovifahamu, ambao kwa sasa ni wanachama 189, mimi nimekuwa mgombea pekee. Hakuna aliyejitokeza kunipinga. Kanuni yetu iko wazi, tusubiri Msimamizi wa Uchaguzi atatangaza kinachofuata baada ya nafasi ya Mwenyekiti kuwapo mgombea mmoja.

Sitanii, nawashukuru wahariri kwa heshima hii kubwa waliyonipa. Hii haikutokea kwa bahati mbaya, ni kutokana na utendaji. Ndiyo maana nawasihi wabunge watimize wajibu wao. Ukiwatumikia vema wapigakura kwa viwango vinavyotakiwa, wao watakuomba uendelee kuwatumikia, si wewe kupitapita ukipenyeza rushwa wakufikirie!!!!!!! Natamani wabunge wetu wengi waombwe na wapigakura kuendelea na kazi ya ubunge baada ya kazi iliyotukuka, badala ya wao kuwaomba wananchi wawafikirie!!!

Naomba msomaji nihitimishe makala hii kwa kukueleza yanayojiri kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025. Dominika ya Machi 30, 2025 tulikuwa na Mkutano wa Halmashauri ya Walei Jimbo Kuu la Dar es Slaaam, tuliofanyia Parokia ya St. Gaspar del Bufalo, Mbezi Beach. Padri mlezi wa walei Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Vitalis Kasembo, ametufikishia maagizo ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa’ichi.

Amesema Askofu Mkuu Ruwa’ichi ameagiza wote wanaotaka kugombea uongozi wa Serikali Oktoba, 2025 tuwapime kwa mambo matano. Jambo la kwanza wawe wazalendo. La pili, anayeomba kuchaguliwa awe mcha Mungu. La tatu, mgombea awe mkweli. La nne, mgombea awe mwajibikaji, na la tano, mgombea awe mwadilifu. Sitaki kuongeza neno. Je, wewe unazionaje sifa hizi? Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827