Demokrasia ya Afrika imezidi kumea na kuchukua mwelekeo mpya kwa kuendelea kuibua taswira mpya ya tafsiri ya demokrasia na utawala bora, tangu kuibuka kwa wimbi la upepo wa mageuzi kwenye utawala wa kidemokrasia kupitia sanduku la kura kwa nchi nyingi za Afrika kama vile Kenya, Nigeria, Zambia, Gambia mwanzoni mwa miaka ya 1990. 

Afrika ilishuhudia kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa na kuwa mbadala wa mfumo wa chama kimoja, ambao ulidumu kwa muda mrefu kwa nchi nyingi za Afrika baada ya kupata uhuru, Tanzania ikiwa mojawapo.

Tangu kutangazwa kwa mfumo wa vyama vingi kwa zaidi ya miongo miwili sasa, tayari chaguzi zinazohusisha mfumo wa vyama vingi zimeshafanyika katika nchi nyingi za Afrika. 

Wakati wa chaguzi ndani ya Bara la Afrika, kumekuwa kukishuhudiwa machafuko na mivutano ya hapa na pale ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiathiri sana mustakabali wa amani katika Bara la  Afrika, na muda mwingine husababisha machafuko na kuibua vita. Ni nadra sana ndani ya Afrika kushuhudia viongozi wakibadilishana madaraka kwa kuheshimu matakwa ya wananchi kupitia sanduku la kura. 

Mfano mzuri ni kile kinachoendelea nchini Gambia ambako Rais aliyehudumu kwa muda wa miaka 22, Yahya Jemmeh, ambaye awali alikubali kushindwa, ameibuka tena na kuyakataa matokeo yaliyomtangaza Adama Barrow kutoka upinzani kuwa ndiye mshindi wa uraisi nchini humo.

Desemba 7, mwaka huu, wananchi wa nchi ya kwanza kupata uhuru barani Afrika, Ghana, walipiga kura kuchagua viongozi baada ya muda  wa miaka minne kwa mujibu wa katiba yao, ambapo  viongozi wa ngazi mbalimbali kwa nafasi za rais na wabunge waliwania nafasi hizo. Ni wazi kuwa uchaguzi huu katika taifa kongwe kabisa la Afrika ulitazamwa kipekee hususani kwa kuzingatia historia ya Ghana na mchango wake katika Bara la Afrika, hususani kusaidia nchi nyingine kupata uhuru lakini zaidi ni mchango wa Kwame Nkrumah ambaye ni kati ya waanzilishi wa Umoja wa Afrika.

Katika uchaguzi ambao unatajwa kuwa na msisimko wa kipekee tangu nchi hiyo irejee kwenye misingi ya uchaguzi wa kidemokrasia mwaka 1992, ambapo watu wengi ndani na nje ya Ghana walikuwa wakimpa nafasi kubwa zaidi mgombea ambaye alikuwa anatetea nafasi yake, John Mahama, kupitia chama chake cha NDC (National Development Congress). 

Dunia na Afrika kwa ujumla ilishuhudia tume ya uchaguzi wa Ghana kupitia Mwenyekiti wake, Charlotte Ossei, akimtangaza mgombea wa urais kupitia chama cha upinzani cha NPP, Mwanasheria Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Nana Addo Dankwa Akuffor Addo, kuwa ndiye mshindi wa nafasi ya urais kwa kupata asilimia 53 ya kura dhidi ya mgombea aliyekuwa anatetea kiti chake, Mahama, aliyepata asilimia 44. 

Pia chama cha NPP kikinyakua zaidi ya viti 171 bungeni, hivyo kuwa na uwakilishi mkubwa zaidi wa vyama vingine.

Katika uchaguzi huu wa Ghana, vyama vya upinzani barani Afrika vina mengi ya kujifunza kupitia mshindi wa uchaguzi huo Nana Addo, lakini pia kujifunza kupitia mchakato mzima wa uchaguzi na kampeni ulivyoendeshwa, hilo linaweza kudhihirika kupitia viunzi mbalimbali ambavyo chama cha NPP kilipitia kuelekea uchaguzi huu.

Mosi, katika kuelekea uchaguzi huu chama cha NPP kiliingia katika uchaguzi kikiwa na mpasuko mkubwa na migogoro baina ya wanachama wenyewe kwa wenyewe.

Na ikumbukwe pia kuwa mara nyingi hapa nchini kuelekea uchaguzi, vyama vya upinzani vimekuwa vikikabiliwa na hali hiyo, mfano halisi ni uchaguzi wa 2010 ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilikumbwa na migogoro ya ndani, kitu ambacho kinatajwa kuwa ni sababu ya wao kushindwa kufanya vyema katika uchaguzi mkuu wa 2010 kupitia mgombea wake, Dkt Willibrod Slaa. Uchaguzi huo ulimrudisha madarakani Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa anatetea nafasi yake kwa ushindi wa 62.83% dhidi ya 27.05% za mgombea wa Chadema.

Pia kuelekea uchaguzi wa mwaka 2015 ilishuhudia jinamizi la migogoro likiikumba Chadema, kupitia mgogoro kati ya chama na baadhi ya wanachama wake waliotajwa kuwa na ushawishi mkubwa na kushika nafasi nyeti katika chama. Mgogoro huu ulishuhudia aliyekuwa Mbunge wa chama hicho kupitia Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, akipoteza uanachama wake, pamoja na wanachama Profesa Kitila Mkumbo, na Samson Mwigamba. Hii ilikuwa mwaka 2013.

Lakini kama hiyo haitoshi, upinzani ulipata nguvu katika muungano wao uliojulikana kama Ukawa, uliojumuisha jumla ya vyama vinne vya siasa kwa kuwa na mgombea mmoja, yaani Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na chama cha NLD. Katika kipindi kifupi kuelekea uchaguzi, Ukawa walipata mtikisiko wa kuondokewa na wanachama nguli na wenye ushawishi kwa wakati huo kutoka vyama viwili vyenye nguvu – ambapo Dk Slaa alijitoa kwenye mchakato  pamoja na Profesa Ibrahim Lipumba, kitu kinachotajwa kuathiri kwa namna moja ama nyingine ushindi wa Ukawa.

Suala kama hili kama nilivyodokeza awali, kuwa chama cha NPP nacho kilipitia njia hii ambayo ilishuhudia mvutano wa pande mbili kati ya wanaomuunga mkono mgombea Addo na wale wanaompinga. 

Mgogoro huu ulisababisha kufukuzwa uanachama kwa viongozi wa juu kabisa wa chama hicho akiwamo Mwenyekiti wa chama, Paul Afoko, Makamu Mwenyekiti, Sammy Grabe, na Katibu Mkuu Kwabena Ayepong, kitu kilichosababisha mvutano wa mahakamani na baadhi ya wanachama kuhama chama hiki, haikuwa rahisi kwa NPP kushinda katika kipindi hiki dhidi ya NDC, kwani wao walionekana na umoja zaidi kuliko wapinzani wao.

Katika hili tunapata somo kuwa katika kuelekea uchaguzi, vyama vya upinzani vimekuwa vikikumbwa na jinamizi hili la migogoro ya ndani, lakini endapo suluhisho la mgogoro huo litakuwa chanya basi ushindi unawezekana, lakini pia dhana ya ‘chama kwanza mtu baadaye’ inazidi kupata mashiko kupitia mfano huu, kwani NPP wameweza kushinda uchaguzi ingawa viongozi wao wa juu walikwishafukuzwa uanachama.

Pili, matumizi ya rasilimali wakati wa kampeni. Katika chaguzi nyingi hapa nchini, vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamika sana kukumbwa na ukata wa fedha pamoja na gharama nyingine za kuweza kumudu mchakato mzima wa kampeni, lakini pia uchache wa rasilimali watu pamoja na vitu kama magari na kadhalika. Ni changamoto kubwa sana, hivyo hali hii husababisha vyama vya upinzani kushindwa kufanya kampeni zao ipasavyo. 

Katika uchaguzi wa Ghana, hali hii pia ilijitokeza, ambapo chama tawala NDC kilifanya kampeni kubwa zaidi na yenye gharama kubwa, kwani ilishuhudia wakisambaza mabango makubwa nchi nzima, vipeperushi, matangazo kupitia vituo vya redio pamoja televisheni, gharama ambazo chama cha NPP hakikuweza kumudu, lakini pia inatajwa katika upande wa timu za kampeni, chama cha NDC kilikuwa na timu zenye nguvu zaidi kwani Rais aliyekuwa anatetea wadhifa wake alikuwa na timu yake, timu nyingine iliongozwa na makamu wa rais, na timu nyingine iliongozwa na mawaziri wa serikali iliyokuwapo madarakani.

Upande wa NPP wao walikuwa na timu mbili tu, moja ikiongozwa na mgombea urais huku nyingine ikiongozwa na mgombea mwenza. Lakini pamoja na chama cha NDC kupiga kampeni yenye nguvu, na gharama kubwa dhidi ya wapinzani wao waliangukia pua, ambapo katika hili vyama vya upinzani vinapaswa kujifunza kuwa, muda mwingi suala si kuwa na rasilimali nyingi, badala yake ni kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali ambayo yanaweza kufanikisha ushindi.

Tatu, nafasi ya historia. Kwa muda mrefu sana vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamika historia kutokuwa upande wao kwani imekuwa ikikipendelea zaidi chama tawala, hivyo kuwapa nafasi ndogo zaidi wao, kwamba muda mwingine hata wapiga kura wamekuwa wakipigia kura chama tawala kwa sababu ya historia.

Chama kiliundwa na Baba  wa Taifa, pamoja na maneno mengine, kwa upande wa uchaguzi wa Ghana tunajifunza kuwa  historia muda mwingine haina nafasi kabisa kuelekea uchaguzi kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia nchini Kenya, Nigeria, Gambia na sasa Ghana.

Nchini Ghana chama cha NDC kinatajwa kama mwasisi wa mfumo wa utawala wa kidemokrasia baada ya machafuko ya kisiasa nchini humo tangu alipopinduliwa Kwame Nkrumah na serikali yake mwaka 1966. Licha ya kutawala kijeshi kwa vipindi tofauti mwaka 1993, Rais Jerry Rawlings alitangazwa kuwa Rais wa Ghana katika uchaguzi wa  kidemokrasia kupitia chama cha NDC, alipoongoza kuanzia mwaka 1993 hadi 2001 huku akishinda chaguzi zote.

Katika uchaguzi wa 2001, NDC kupitia mgombea wake, John Atta Mills, alipoteza nafasi, hivyo chama cha NPP kilishinda uchaguzi huu kupitia mgombea  John Kufuor ambaye pia alipoteza mwaka 2008, kisha NDC kushinda tena  kupitia mgombea, John Atta Mills, kwa kumshinda Nana Addo. mwaka 2016 Nana Addo anavunja mwiko wa historia kuipendelea NDC mara nyingi na kuandika ukurasa mpya  wa utawala wa vyama vya upinzani, akimshinda Rais aliyehudumu kwa muda wa miaka minne tu. 

Lakini pia historia inaendelea kuonesha kutokuwa na upendeleo kwani licha ya chama cha CCP kilichoasisiwa na Kwame Nkrumah kusaidia katika harakati za uhuru, tangu utawala na mfumo wa vyama vingi hakijawahi kushinda katika uchaguzi kwa ngazi ya urais na ikumbukwe kuwa nchini Ghana kuna vyama zaidi ya 20 vya siasa vyenye usajili wa kudumu kama Tanzania.

Kudondoka kwa chama tawala NDC

Kama dunia ilivyoshuhudia, licha ya kuwa na nguvu ya fedha pamoja na kusaidiwa na dola katika uchaguzi, John Mahama ameshindwa kutetea nafasi yake, na kilichomdondosha yeye na chama chake ni udhaifu wa uongozi na utawala wa serikali katika kipindi chake ambapo pia inatafsiriwa kama ndiyo uimara wa NPP. Ripoti za wachambuzi wa siasa za ndani ya Ghana, wanatanabahisha kuwa chama cha NDC kimepoteza viti vyake kwa sababu zifuatazo:

Rushwa iliyokithiri katika serikali ya NDC ambapo wananchi wamekuwa wakilalamika sana kuongezeka kwa rushwa na hata ripoti mbalimbali zilitanabahisha kuongezeka kwa rushwa na ufisadi nchini Ghana, huku kashfa kubwa mbalimbali zikiibuka na kuiandama serikali ya Mahama, kitu ambacho kilichukiwa zaidi na wananchi kwani waliona dhahiri kuwa serikali ya NDC haitaweza kupambana na rushwa.

Taarifa ya rushwa iliyotolewa na GYEEDA ambayo iliituhumu serikali kwa rushwa zilizokithiri kama vile rushwa kubwa inayotajwa ya Alfred Wayome, ya milioni moja za Ghana ambayo Rais alishindwa kutoa utetezi wa kueleweka ambao ungewashawishi wananchi.

Hali ngumu ya uchumi kwa wananchi

Kwa miaka miwili mfululizo serikali ya Ghana imekumbwa na hali ngumu ya uchumi kwa wananchi, kitu kilichosababisha malalamiko ya makali na kupanda kwa gharama za maisha, kuna muda hali ilikuwa tete zaidi, kitu kilichosababisha Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuingilia kati na kuishauri serikali ya Ghana namna ya kupunguza matumizi ya serikali ili kuweza kuinusuru hali ya uchumi pamoja na kutafuta njia mbadala. 

Mchango wa elimu

Tafiti za Ghana zinabainisha kuwa kwa miaka yote NDC imekuwa ikipata ushindi kutoka maeneo ya pembezoni na si mjini, lakini kuongezeka kwa elimu hadi maeneo ya pembezoni kulikochagizwa na uhamaji wa watu wengi kwenda mijini, kumesababisha mbegu na chachu ya mabadilko, kitu ambacho kimechochea sana ushindi wa NPP.

Hitimisho 

Ingawa kijiografia Tanzania na Ghana zinatofautiana, lakini ni ukweli usiopingika kuwa mazingira ya uchaguzi baina ya nchi hizi mbili yanaendana waziwazi, pia ikumbukwe kuwa hata katika uchaguzi wa mwaka jana  hapa nchini, kilio cha wananchi kilikuwa ni rushwa, hali duni ya maisha na ufisadi, vitu ambavyo vimewezesha kushinda kwa NPP Ghana lakini sababu hizo hizo zimesababisha upinzani kushindwa Tanzania.

Kwa ujumla, somo adhimu tunalopaswa kujifunza ni kuwa demokrasia ni watu, watu wanachagua nani awaongoze, bila kujali una pesa kiasi gani wala mali kiasi gani, bila kujali gharama na kampeni ya kuburudisha na mbwembwe nyingine. Sera madhubuti na ushawishi kwa wananchi ndivyo vinavyokufanya ushinde uchaguzi.