Hivi karibuni nilishiriki mjadala unaohusu uamuzi wa Ridhiwani Kikwete kugombea ubunge Jimbo la Chalinze.
Kama ilivyo ada, mijadala ya aina hii mara zote imekuwa na mvuto. Kumekuwapo hoja kwamba wanaohoji uhalali wa mtoto wa Rais na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania ubunge kupitia chama kinachoongozwa na babaake, ni wivu na husda!
Lakini wapo wanaoona kuwa kitendo hicho, ingawa ni haki yake ya kikatiba kama walivyo Watanzania wengine, hakiwezi kutolewa maelezo hata kikaweza kueleweka kwa wananchi walio wengi.
Sikukusudia kuendelea na mjadala huu kwa sababu tayari nilishaweka bayana faida na hasara za uamuzi wa Ridhiwani. Hata hivyo, makala kadhaa zilizoandikwa kwenye magazeti zimenifanya nirejee kutetea hoja yangu.
Katika moja ya makala kwenye gazeti la Mwananchi, mwandishi amejitahidi kutuaminisha kuwa si kosa wala dhambi kwa mtoto wa kiongozi kufuata nyayo za uongozi za babaake. Kwa sababu hiyo, haoni kama kuna dosari ya kimantiki ya mtoto kushiriki kuwania uongozi.
Kwanza naomba nikubaliane na mwandishi wa makala hayo pale anaposema si dhambi kwa mtoto kufanya kile kinachofanywa na mzazi au wazazi wake. Kwa maneno mengine anachotaka kusema mtoto wa seremala kuwa seremala ni jambo lisilohitaji mjadala.
Amejitahidi kutoa mifano ya watoto wa “wakubwa” ambao baadaye wamekuja kuupata “ukubwa”. Kwa mifano yake, amewataja watoto kama Makongoro Nyerere na mdogo wake Rosemary Nyerere; Thuwaiba Kisasi, Vita Kawawa na dadaake, Zainab Kawawa; Namalok Sokoine, Mahmoud Kombo, Mansour Himid, Amani Abeid Karume, Uhuru Kenyatta, George W. Bush, Joseph Kabila, na wengine kadhaa.
Lakini akaenda mbali zaidi kwa kutoa mifano ya watoto wa wachezaji maarufu wa mpira na hata ngumi ambao wameweza kufuata nyayo za wazazi wao.
Ni ukweli ulio wazi kwamba hawa ni watoto wa wakubwa na wamefanikiwa kufanya kile kilichofanywa na wazazi wao. Lakini ni ukweli ulio wazi kwamba mifano iliyotolewa na mwandishi wa makala hayo; kwa kutaka kuonesha kuwa hata Ridhiwani yuko sahihi kuwania madaraka, ni miepesi mno.
Kwa mfano, ni kweli kwamba Makongoro alikuwa Mbunge wa Arusha mwaka 1995 wakati babaake, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa hai. Tofauti na Ridhiwani, Makongoro aligombea ubunge katika chama ambacho babaake hakukiunga mkono.
Itakumbukwa kwamba alihama CCM na kujiunga NCCR-Mageuzi baada ya kuona ndani ya hicho chama “cha babaake” asingepenya! Kwa kulitambua hilo, na pengine kwa kujua hana nguvu za kifedha za kupenya, na kwa kutambua kuwa babaake asingeweza “kumbemba”, aliamua kuingia kwenye chama cha upinzani ambako masuala ya mizengwe na rushwa za kupitishwa kuwania uongozi havikuwapo.
Makongoro alichofanya ni kumweleza mzazi wake kwamba ameamua kuwania ubunge kupitia NCCR-Mageuzi kwa sababu ambazo alimweleza na bila shaka yoyote, Mwalimu alimwelewa.
Mwalimu ambaye kimsingi ndiye aliyemkosesha Augustino Mrema urais, asingekuwa radhi kumtumia Mrema kuhakikisha mwanaye anashinda ubunge. Alichokifanya Mwalimu ni kumwacha Makongoro mwenyewe ahangaike, na kwa kweli hatima yake ikawa kupata ushindi ambao nao haukudumu kwa sababu ulitenguliwa katika mazingira yanayotia shaka! Mahakama ilitengua ubunge wa Makongoro bila kujali kama huyo ni mtoto wa Baba wa Taifa, au la!
Kwa maelezo haya, ni rahisi kuamini kuwa huyu mtu alishinda ubunge bila kutumia mgongo wala ushawishi wa babaake kama tulivyoona kwa Ridhiwani ambako vikao vya juu vya uteuzi vipo chini ya babaake.
Pili, wanasiasa kama Kabila, Amani Karume, familia ya Kawawa, familia ya Sokoine, na wengine, hawa wamepata nyadhifa wakati wazazi wao wakiwa wameshatangulia mbele ya haki. Hakuna mtoto wa Kawawa ambaye kawa mbunge wakati baba yao akiwa Katibu Mkuu wa CCM au akiwa na wadhifa wowote mkubwa katika jamii. Hakuna.
Mtoto wa Sokoine amekuwa mbunge ikiwa ni miongo zaidi ya miwili tangu babaake afariki dunia. Huyu huwezi kusema kabebwa na babaake. Amani Karume kawa Rais wa Zanzibar si kwa sababu kapigiwa au kabebwa na babaake, bali ni kutokana na uwezo wake wa kisiasa ingawa yapo manung’uniko ya kwamba “jina” lilimsaidia.
Bado naamini kwa dhati kabisa kuwa kama Sheikh Karume angethubutu kujenga mazingira ya siku moja mwanaye awe mrithi wa kiti chake cha urais, Wazanzibari wangekuja juu. Vivyo hivyo, Mzee Kenyatta, angekuwa madarakani halafu akaanza mikakati ya kumfanya mmoja wa watoto wake kumrithi, Wakenya wangehoji na pengine wangekataa.
Hivi karibuni nchini Uganda kuliibuka mjadala mkali baada ya kuwapo tetesi kwamba Rais Yoweri Museveni anamuandaa mwanaye, Muhoozi kuwa Rais wa Uganda baada ya yeye Rais Museveni kung’atuka. Kelele nyingi zilipigwa, na ikamlazimu Rais Museveni mwenyewe awathibitishie Waganda na walimwengu kwamba hana mpango huo.
Kelele zilizopigwa hazikulenga kupinga uwezo wa mtoto huyo kuwa Rais wa taifa hilo, bali ilionekana kuwa ni mpango wa babake kumbeba! Kwa ufupi ni kwamba kinachopingwa na wananchi wengi ni ile hali ya kuwapo mazingira ya mzazi kumbeba mtoto, na si kuhoji uwezo wa huyo mtoto.
Mimi napenda mchezo wa masumbwi. Mmoja wa wanamasumbwi ninaowapenda ni Floyd Mayweather Jr. Huyu ni mtoto wa Floyd Mayweather Sr,. Floyd amekuwa maarufu mwenye mchezo wa masumbwi kama alivyokuwa babaake. Amepigana mapambano mengi na hadi ninavyoandika makala haya, hajashindwa!
Kumfananisha Floyd Mayweather na Ridhiwani, kwa maana ya mtoto kufanya kazi inayofanywa na babake, ni kuvuruga mjadala! Ni kuvuruga mjadala kwa sababu mchezo wa ngumi habebwi mtu! Unapanda ulingoni ukijijua una ubavu, kinyume cha hapo mzazi wako atashtukia uko mochari. Hata kama baba mtu angempenda vipi mwanaye, hayo mapenzi hayawezi kumpa ushindi huyo mtoto. Kinachompa ushindi ni juhudi zake binafsi ulingoni.
Floyd anapoingia ulingoni kupambana na mpinzani wake, babaake hubaki kando akisali ili mtoto wake aibuke mshindi. Hawezi kusema hapa mwanangu kazidiwa, ngoja niingie ulingoni kumsaidia. Sana sana anachoweza kufanya ni kuingia ulingoni kuvuruga mchezo ili mtoto wake asikabiliwe na kifo kutokana na makonde ya mpinzani wake.
Ridhiwani si hivyo. Ngumi za kisiasa zinapiganwa na mtoto na baba. Aliye ulingoni anapigana, na aliye nje ya ulingo (baba) anapigana. Tena basi, pambano linakuwa la upande mmoja kutokana na ukweli kwamba anayeamua mtoto (Ridhiwani) apambane na nani, ni babaake. Wapinzani waliojitokeza kupambana na Ridhiwani ni wapweke. Hawawezi kupambana naye wakamshinda! Hawawezi kumshinda kwa sababu nguvu inayotumika Chalinze ni kubwa mno.
Kumlinganisha Ridhiwani kwamba anafuata nyayo kama ilivyo kwa mtoto wa mwanasoka kufuata nyayo za babaake, ni kuuhadaa umma. Ni kujaribu kulinganisha vitu viwili visivyokuwa na nasaba hata kidogo.
Mtoto anayeingia kucheza mpira kama ilivyo kwa babaake, haingii kucheza kwa sababu yeye ni mtoto wa mcheza mpira maarufu! Kinachomwezesha kuingia uwanjani ni uwezo wake wa kimchezo, na si vinginevyo. Hata kama babake angekuwa Pele, hawezi kuingizwa uwanjani kucheza ilhali ikijulikana wazi kwamba hana pumzi wala uwezo wa kimchezo. Vita ya uwanjani ni vita inayomhusu mchezaji mwenyewe, na si kubebwa na jina la mzazi au ndugu yake maarufu. Anapobaki na kipa, ni wajibu wake kufunga. Hawezi kubaki na kipa kisha akamuita babaake amsaidie kufunga bao. Hakuna kitu cha aina hiyo.
Ridhiwani kwa jina la babaake akibaki na kipa anaweza kusaidiwa na babaake kufunga bao! Kwenye siasa hilo linawezekana, lakini kwenye mpira halipo. Kwa hiyo litakuwa jambo la ajabu kwa yeyote awaye kusimama na kuhoji kwanini fulani kampanga mtoto wake kucheza mpira. Watu watahoji uwezo wa mtoto kwa sababu ndiyo unaoamua, na si ukoo au umaarufu wa wanaomzunguka.
Tumeona karibu viongozi wote wakuu wa CCM wameenda Chalinze kuhakikisha mtoto wa bosi wake anashinda! Tumeona mama, ambaye ni mke wa Rais, akisimama jukwaani kumuombea kura mtoto wake. Mkwere gani anaweza kuwa na jeuri ya kumpuuza mke wa Rais anayepanda jukwaani kumuombea kura mwanaye?
Tumeona kwa kawaida uchaguzi wa mtu binafsi ni wa mtu binafsi na walio karibu naye. Lakini uchaguzi wa Chalinze tunashuhudia hata Ofisi ya Ikulu ikisambaza picha za mikutano ya kampeni ya mtoto wa Rais. Bado tunasubiri baba aende kuongeza nguvu. Hapa ni sawa na kutoa kikosi cha makomandoo kwenda kumuua mbweha! Nguvu zote hizi kwa mgombea gani wa kumtia shaka Ridhiwani kushinda uchaguzi wa Chalinze?
Hata kama Rais Kikwete hataenda kumpigia debe mwanaye, bado mtoto huyo ataibuka mshindi. Na kwa kweli hata kama ataupata ushindi bila babaake kuonekana jukwaani, bado hiyo haiondoi ukweli kwamba atashinda kwa sababu ya nguvu kubwa za kimamlaka alizonazo babaake pamoja na viongozi wa CCM walioamua, hata bila kupenda, kwenda kumnadi kijana huyo.
Ni katika mazingira ya aina hii, unaweza kusema uchaguzi wa Chalinze utakuwa huru, lakini si wa haki. Tayari si uchaguzi wa haki. Si wa haki kwa sababu kwenye mizani ya wagombea, mmoja ana nguvu za ziada zinazomwezesha kushinda bila hofu yoyote.
Kwenye mazingira ya aina hii hapakuwapo sababu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutumia mamilioni ya shilingi kushughulikia jambo ambalo liko dhahiri kabisa. Hapa ilipaswa busara itumike tu ambayo ingesaidia kumfanya Ridhiwani apite bila kupingwa ili fedha zinazovurugwa sasa kwenye kampeni na kwenye vifaa vya uchaguzi, zielekezwe kwenye miradi ya kijamii kama shule, na kadhalika.
Haya mambo tunayasema si kwa sababu tuna wivu au nia mbaya, bali ni kutokana na ukweli wenyewe ulivyo.
Wakati haya ya Chalinze yakiendelea, hatuna budi kujikumbusha malalamiko ya watoto wengi wa makabwela baada ya kubaini kuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuna watoto wengi wa wakubwa.
Pamoja na ukweli kwamba watoto hao wana sifa, bado makabwela wengi wanahoji ni kwanini basi uwezo huo wasiuoneshe kwenye maeneo mengine yenye “ukame”. Kwanini uwezo wao wa kiakili uwapeleke BoT ambako ndiko kwenye chungu cha fedha? Kwanini wasiende kufanya kazi kwenye mashamba ya mkonge? Kwanini wasiwe watumishi kwenye kampuni binafsi za ulinzi? Kwanini BoT, NBC, kampuni za simu, TANAPA, Ngorongoro na kwingine kulikonona?
Katika BoT wanasema kuna Salama Ali Hassan Mwinyi, Filbert Tluway Sumaye, Zaria Rashidi Kawawa, Blasia William Mkapa, Herriet Marten Lumbanga, Pamela Edward Lowassa, Rachel Muganda, Salma Omary Mahita, Justine Mungai, Kenneth Nchimbi, Violet Philemon Luhanjo, Liku Kate Kamba, Thomas Mongela, Jabir Abdallah Kigoda, na kadhalika!
Je, hawa wamekutana hapo kwa bahati mbaya au kwa sababu wazazi wao ndiyo hao hao walio kwenye kundi la “wakubwa” wa nchi hii? Kama ni kwa “bahati mbaya”, kwanini wasikutane kwenye biashara ya daladala?
Ukitafakari, tena si kwa kina, utaona wazi kabisa kuwa nchi hii kama wewe hutoki katika ukoo au familia inayomeremeta, huna chako. Ukijumlisha na elimu hii ya Academy vs Sekondari za Kata, kwa makabwela mbele ni kiza tu.