Nafahamu kuwa nchi iko kwenye joto la uchaguzi na joto hilo ni kubwa ndani ya chama tawala ikilinganishwa na ilivyo nje (kwenye vyama vingine). Wasomaji mnajua kuwa safu yangu ya uchumi na biashara huwa sizungumzii siasa hata tone. Hata leo sichambui siasa ndani ya makala hii; hivyo usiwe na shaka. Twende pamoja.
Wasomaji wa muda watakumbuka kwamba mwaka huu nimeshapata kuandika makala inayosema, “Tunahitaji Rais na wabunge wajasiriamali”. Nimeinua kalamu leo baada ya kuvutiwa sana na kauli ya mmoja wa waliotangaza nia kuomba ridhaa ya kugombea Urais kwa tiketi ya CCM, Ndugu Edward Lowassa.
Akiongea na wahariri wa vyombo vya habari mjini Dodoma alisema, “Ni kudanganya watu kwamba nikiwa maskini ndiyo ninakuwa kiongozi mzuri….Tusiwabeze matajiri, matajiri wawe mfano kwa wengine. Napenda watu wawe matajiri na ninataka mnihukumu kwa hilo.”Baada ya kuisikiliza ile hotuba yake, niliandika hivi katika ukurasa wangu wa Facebook, “Mengine sijui lakini kwa kauli hii, Lowasa kamata tano zangu.”
Najua kuwa hili joto la uchaguzi lilivyopanda, kumtaja mgombea yeyote unaweza kujikuta unakudwa shati! Na ninajua kuwa zipo hoja nyingi zinazohoji uhalali wa utajiri wa Lowassa; hayo mimi siyajui na ninawaachia wachambuzi wa siasa. Mimi naichukua kauli hiyo hapo juu, kama mtazamo (mentallity) na ninaitumia kuangalia kiuchumi kwa viongozi wote, madiwani, wabunge mpaka Rais.
Urais si msahafu kuwa ni lazima awe Lowassa (kama kambi yake inavyoamini), Rais anaweza kutoka CCM ama akatoka upinzani, wenye uamuzi ni wapiga kura. Hata hivyo, iwe Rais atakuwa Lowassa ama mtu mwingine, iwe atatoka CCM ama upinzani; kauli aliyoitoa Lowassa (under ceteris peribus) inatakiwa kuwa ndiyo mtazamo wa aina ya viongozi wa kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano hadi kumi ijayo.
Harakati za urais, ubunge na udiwani naona zimepamba moto karibu kila kona nchini. Ukifuatilia kwa umakini hata sasa katika nchi hii,{utagundua kuwa} uadilifu wa kiongozi unapimwa kwa kuangalia kiwango chake cha umaskini. Kiongozi akionekana ana mali chache inahesabika kuwa ndiye mwadilifu, na mwenye mali nyingi anaonekana kuwa sio muadilifu.
Kuna maswali huwa tunasahau kuuliza linapokuja suala la kuwatathmini viongozi wetu. Mosi, ikiwa kiongozi analeta ‘swaga’ za kutaka kujionesha ni maskini (ama wa kawaida), anatakiwa atueleze mambo mawili. Kwanza, ni kwa nini amekuwa maskini katika nchi yenye utajiri mkubwa namna hii?
Kama yeye anayetafuta kutuongoza ameshindwa kukabiliana na umaskini, atawezaje kutuongoza sisi maskini kuufikia utajiri. Kuongoza ni kuonesha njia, inawezekanaje mtu kutuonesha njia ya kwenda mahali ambako “eti” anasema hakujui, hajawahi kufika na hana mpango wa kufika! Ndiyo, kiongozi anaetuletea taswira ya kujifanya masikini ama wa kawaida anawezaje kutufikisha kwenye mafanikio na utajiri?
Kwa nini amekuwa wa kawaida katika nchi ambayo ni nzuri zaidi ya kawaida? Ikiwa kiongozi anayetafuta urais amewahi kuwa mbunge ama waziri, ni dhahiri kwamba kuna mamilioni tulikuwa tukimlipa kupitia kodi zetu. Akisema hana mali za maana itabidi atueleze ni akili gani alikuwa anaitumia kujisimamia katika eneo la fedha?
Lakini tukikukuta wewe mtafuta madaraka una mali za kupindukia ambazo huenda tuna mashaka nazo; tutahitaji utupe maelezo ya kina namna ulivyozipata. Hii itatusaidia kwa namna mbili. Kwanza tujiridhishe ikiwa ni mali halali na pili ikiwa ni halali, basi itatuhamasisha na sisi wananchi unaotaka kutuongoza kufuata nyayo zako. Kwa maana chuma hunoa chuma, kiongozi tajiri atazalisha wananchi matajiri na kiongozi maskini atazalisha wananchi maskini.
Nafahamu wazi kuwa wagombea wengi wanaifahamu mitazamo ya sisi Watanzania tulio wengi; ambapo tunapenda na kufurahia viongozi maskini. Kwa hiyo, wagombea wengi hutaka kijionesha mbele ya wapiga kura ya kwamba wao hawana mali, ni maskini, ni watu wa kawaida. Kinachofanyika ni kwamba huficha kwa makusudi utajiri wanaomiliki. Mtu anayetuficha mali zake ni rahisi kutuibia tumpapo madaraka.
Sifa ya mjasiriamali ni kujilipa mwishoni. Mjasiriamali daima anatanguliza maslahi ya biashara mbele. Tunamtaka Rais na wabunge ambao wataiendesha Serikali kiujasiriamali. Fedha ya kodi ikikusanywa mtazamo wa kijasiriamali utataka zianze shughuli za maendeleo ndipo kufuatie kujaza matumbo.
Viongozi wanaoanza kukumbuka posho na masurufu yao halafu zinazobaki ndizo wanaangalia kujenga matundu ya vyoo mashuleni; hawa bado hawaifai nchi kama hii. Bila kuwa na viongozi waliofurika roho ya ujasiriamali nchi hii itabaki maskini mpaka mwisho wa dunia! Ieleweke kwamba hapa siongelei kiwango cha mali ama biashara wanazopaswa kumiliki hao viongozi bali naongelea mtazamo wa kijasiriamali.
Viongozi wenye mtazamo wa kijasiriamali hawawezi kucheka na watu wanaokwepa kodi kwa sababu kodi ndiyo uchumi. Mjasiriamali yeyote hupambana ili afikie hatua na kujitegemea. Wanaofanya biashara wanatambua kuwa kadiri unavyokuwa na pesa yako binafsi (owners equity) ndivyo unavyokuwa na uhuru na nguvu. Tunataka Rais na wabunge ambao watapambana kufa na kupona kuhakikisha kampuni tunayowapa (nchi) inafikia ama inaanza kuelekea kwenye kujitegemea zaidi.
Kuwa na wabunge ambao kutwa kucha wanapiga kelele kuhusu miradi iliyokwama kutokana na ukosefu wa fedha; na wakati huohuo hawapo tayari kusamehe posho zao; bado ni mzigo kwa nchi hii. Kiongozi anayesimama majukwaani kusisitiza vijana wajiajiri halafu yeye mwenyewe hana hata mpango wa walau kufuga mbuzi tu nyumbani kwake; huyo hawezi kushawishi vijana kujiajiri.
Kwanza vijana hawa wanaoambiwa wajiajiri huwa wanahisi kama wanachorwa tu, kwa sababu viongozi wao hawana mkao wa kijasiriamali. Wanaoambiwa wajiajiri kuna wakati hujiuliza, ikiwa kujiajiri ni kuzuri mbona hao wanaotambia hawaachi ajira zao kuja kujiajiri? Mbona kila siku wanahangaika kuwapachika watoto na ndugu zao katika hizo ajira?
Ifahamike kwamba sifa nyingine ya mjasiriamali ni kutokuwa na upendeleo. Katika kila nafasi anazangatia uwezo na si kujuana na kubebana. Ukiwa na duka, kampuni ama biashara yoyote halafu linapokuja suala la wafanyakazi ukawa unawaajiri ama kuwaweka kwa kufahamiana, kulindana na kubebana pasipo kuzingatia uwezo; ninakuthibitishia kuwa hufiki mbali, utafilisika.
Tunataka rais, wabunge na madiwani ambao wataichukulia nchi hii kama biashara inayotakiwa kuzalisha faida. Kama zipo hasara zilizotokea huko nyuma basi vitabu vifungwe, zipigwe hesabu mpya ili biashara hii iitwayo Tanzania ianze kuzalisha faida.
Uti wa mgongo wa ujasiriamali ni uaminifu na uadilifu. Ukikosa uaminifu na uadilifu biashara ni lazima ikushinde. Wateja watakuchukia, wafanyakazi watakuchukia na utaporomoka tu. Tunamsubiri rais mjasiriamali, wabunge wajasiriamali na madiwani wajasiriamali. Hawa ni wale ambao watakuwa na rekodi za uaminifu na uadilifu na ambao wataendesha biashara yetu iitwayo Tanzania katika misingi hiyo.
Ninatamani nchi impate rais, wabunge, madiwani na kisha mawaziri ambao wamebeba roho na maono ya kijasiriamali mioyoni mwao(entrepreneural spirit and visions). Rais ambaye ataagiza kile kinachochukuliwa kwa uzito, mawaziri ambao wataonesha matokeo yanayofanana na sera na madiwani ambao watapanga wanachokielewa.
Nchi yetu haina mkao wa kijasiriamali kabisa. Wenye kutunga sera na wenye kusimamia ni kama wanaishi sayari tofauti. Sera inasema kuwawezesha akina mama na vijana wajitegemee kivipato. Lakini mwanamama akianzisha biashara ya mama ntilie, mgambo si tu wanamkataza kutafuta hicho kipato, bali wananyang’anya kabisa na mtaji! Machinga akipanga vitu vyake FFU; hawa hapa; kumpiga mabomu.
Huwezi kuwalaumu mgambo ama FFU kwa sababu wanatumwa. Huwezi kuwalaumu wanaowatuma kwa sababu hawajui walitendalo. Laiti wangejua maumivu anayopata mjasiriamali pindi unapomfukuza mahali penye wateja ama unaponyang’anya mtaji wake, wasingekuwa wanatenda wayatendayo. Ujasiriamali ni roho na katika uchaguzi wa mwaka huu natamani tuwapate viongozi wenye roho ya ujasiriamali.
Sifa nyingine ya mjasiriamali ni kuishi kwa alichonacho(living within your means). Tunataka viongozi ambao kwa dhati kabisa watatuita wananchi na kutuambia jamani enhee, tulichonacho ni hiki na tunagawana kidogo kidogo.Kama hakuna wanaokomba mboga, wananchi tutaelewa tu, maana chako kidogo kina heshima kuliko kingi chenye masimango.
Mimi hainisumbui, rais, wabunge na madiwani watatoka chama gani, ninachokizingatia ni mtazamo wao (mindset) katika eneo hili la ujasiriamali. Iwe ni kutoka UKAWA ama CCM, iwe ni kutoka mgombea binafsi ama vyama vingine vya upinzani; kura yangu nitampa kiongozi mwenye roho na maono ya kijasiriamali.
Ninachofurahi na kuamini ni kwamba chama changu cha siasa (maana mimi ni mwanachama wa kawaida katika chama changu) kitazichanga vema karata zake na kutuletea wagombea wanaouzika kwa muktadha huu wa roho ya kijasiriamali.
Tanzania inahitaji viongozi matajiri.