Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Riziki Pembe Juma ameeleza kuridhishwa na namna Wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanavyoongeza viwango vya ubora na ubunifu katika huduma na bidhaa wanazozalisha.
Waziri Riziki Pembe Juma ameeleza hayo alipozungumza kwenye sherehe za ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu kama Juakali, zilizofanyika Desemba 11,2022 katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
Amesema hatua iliyofikiwa na Wajasiriamali hao ni dalili nzuri ya kufikiwa kwa lengo la kuyafanya maonesho hayo ya Juakali kuwa jukwaa la fursa ya kukuza masoko, kubadilishana uzoefu na teknolojia.
Ameongeza kuwa hali hiyo inatokana na ukweli kuwa wajasiriamali hao bado wanahitaji kuendelea kujifunza zaidi, kubadilishana uzoefu na teknolojia baina yao katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Sote tumeshuhudia bidhaa mbalimbali zinazouzwa katika baadhi ya mabanda yaliyopo katika maonesho haya ambayo yamejumuisha nchi zote wanachama, bidhaa zina ubora na ubunifu wa hali ya juu. Ongezeko hili la ubunifu na ubora wa bidhaa za wajasiriamali hawa kila mwaka, ni dalili njema kuwa wana Afrika Mashariki katika siku za usoni tutakuwa na bidhaa zinazotosheleza mahitaji yetu kwa ubora na wingi hali ambayo itasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje” alisema Waziri Riziki
Waziri Riziki pia alieleza kuridhishwa na namna Wanawake walivyojitokeza kushiriki katika maonesho hayo.
Asilimia 87 ya idadi ya Wajasiriamali zaidi ya 300 wa Tanzania kwenye maonesho haya ni Wanawake, hali hii inadhirisha na uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan unatoa kipaumbele kwa wanawake kwa kuzingatia kuwa mwanamke ni kiungo thabiti katika maendeleo ya familia na nchi kwa ujumla, alisema Mhe. Waziri.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda Robinah Nabbanja ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni katika sherehe hiyo ya ufunguzi wa maonesho,ametoa wito kwa Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kufanya mabadiliko muhimu ya sera za uchumi ili ziweze kuleta msukumo katika kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kurahisha zaidi ufanyaji wa biashara katika Jumuiya.
“Kundi la wajasiriamali wadogo na wakati linachangia asilimia 60 ya pato la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku 99% ya biashara ndogo na kati zikimilikiwa na wazawa wa Afrika Mashariki, ni muhimu kukumbuka kuwa katika kila Waafrika 10; 6 kati ya hao wamejiajiri katika sekta ya biashara ndogo na kati, hivyo ni sawa na kusema kuwa, biashara ndogo na za kati zinazalisha wastani wa ajira 8 katika kila ajira 10 mpya,” alisema Waziri Mkuu Nabbanja
Mheshimiwa Nabbanja alisisitiza kuwa endapo sera zitakuwa rafiki zaidi kiasi cha kutatua changamoto zinazowakabili wazalishaji wadogo italeta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Jumuiya, kwa kuwa asilimia 99 ya Wajasiriamali ni wazawa wa Afrika Mashariki hivyo maboresho hayo yatawanufaisha wao moja kwa moja na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda na upatikanaji wa ajira za kutosha kwa Vijana na wanawake.
Nabbanja amesema maonesho ya juakali ni jukwaa muhimu linalowawezesha Wajasiriamali kuonesha na kuuza huduma na bidhaa wanazozalisha, vilevile yanatoa fursa hadhimu kwa Wajasiriamali kuongeza wigo wa soko, kujifunza zaidi kuhusu ubunifu na kubadilishana uzoefu na teknolojia katika masuala mbalimbali kama vile kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo.