Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wakati ambao Tanzania ipo katika wakati wa kuwa nchi mwenyeji wa mkutano mkuu wa Nishati Afrika ulioanza leo hii jijini Dar es Salaam , Ubalozi wa India nchini umeadhimisha sherehe za 76 za sikukuu ya jamhuri ya taifa la India .
Rejea katika historia inaeleza taifa la India lilitambulika rasmi kama Jamhuri mnamo Januari 26,1960 miaka mitatu mara baada ya kupata uhuru wake kutoka kwa Waingereza.
Maadhimisho ya siku hiyo hufanyika kila mwaka katika tarehe husika ambapo kwa mwaka huu sherehe hizo ziliadhimishwa hapa nchini hapo jana zikiongozwa na balozi wa India nchini Bishwadip Dey.
Hafla ya siku hiyo ilipata kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa kiserikali, taasisi binafsi na wawakilishi wa balozi mbalimbali hapa nchini .
Akizungumza katika hafla hiyo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan , Naibu waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini ametoa salamu za pongezi kwa jamii ya watu wa India waishio hapa nchini katika kuadhimisha siku hiyo huku akigusia uhusiano mkubwa wa kidiplomasia uliopo kati ya taifa la India na Tanzania ambao umedumu kwa takribani miongo sita mpaka sita tangu mahusiano hayo yalipoasisiwa mwaka 1961 na waasisi wawili wa mataifa hayo, Julius Nyerere na Mahatma Gandhi.
Naibu Waziri Sagini amethibisha hoja hiyo kwa kupitia ziara iliyofanywa na Rais Samia mwezi Oktoba 2023 nchini humo iliyolenga kuendeleza uhusiano katika ushirikiano wa kimikakati.
Aidha Naibu Waziri Sagini pia amegusia mahusiano ya mataifa mawili ya Tanzania na India katika nyanja ya kibiashara ambapo ameeleza kuwa sekta biashara baina ya nchi hizo mbili inazidi kukuwa na kuifanya India kuwa mshirika wa pili wa kibiashara nchini.
“Katika uwekezaji inakadiriwa kuwa uwekezaji wa India nchini Tanzania umefikia jumla ya takribani Dola za kimarekani bilioni 4 na kuifanya India kuwa miongoni mwa wawekezaji watano wa juu nchini”
Aidha akiongeza Naibu waziri huyo ametoa pongezi kwa Dk Kaushi Ramaiya ambaye ametunukiwa tuzo ya Pravasi Bharatiya Samm (PBSA) 2025 ,kwa kutambulika mchango wake wa kipekee katika huduma za afya, hasa katika uwanja wa dawa na huduma zake muhimu katika jamii.
“Dk Kaushi anajulikana sana nchini Tanzania kwa mchango wake bora katika nyanja ya matibabu na kujitolea katika kuendeleza huduma za afya nchini Tanzania na kwingineko.” amesema Naibu waziri Sagini.
Kwa upande wake Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufungua milango kwa wawekezaji kutoka nchini India kuja kuwekeza nchini huku akiahidi kuwa wataendelea kudumisha uliopo kati ya mataifa hayo mawili.
Maadhimisho ya siku hiyo ya Jamhuri yalifanyika hapo jana katika ukumbi wa The dome ulioko Masaki, Dar es salaam.