NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam unatuhumiwa kumpunja mjane mafao yaliyotokana na kifo cha mumewe.

Mjane huyo, Salome Leguna, ameushitaki ubalozi huo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula.

Salome ni mjane wa Andrew Nassoro aliyekuwa mtumishi wa ubalozi huo kwa miaka 30 hadi alipofariki dunia Mei 9, 2018.

Kwa mujibu wa nyaraka alizonazo Salome kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pia kutoka Ubalozi wa Marekani, mjane huyo anahoji uhalali wa kulipwa Sh milioni 88.769; ilhali taarifa nyingine zikionyesha kuwa ameshalipwa Sh milioni 172.07.

Mkanganyiko huo unatokana na Salome na wanufaika wengine wa mirathi hiyo kutilia shaka kiwango walicholipwa.

Barua aliyomwandikia Balozi Liberata inasema: “Sijaridhishwa na majibu ya barua zote mbili (kutoka ubalozini). Ukisoma vizuri utaona kuna utata katika ulipaji uliofanyika. Barua moja iliyosainiwa na Janine Young inadai tulilipwa na mimi nilisaini – na kiasi chote tulicholipwa ni Sh 88,769,150. Barua ya Juni 2, 2021 iliyosainiwa na Ryan Reynolds (Ofisa Rasilimali Watu) inataja tumelipwa mafao yote kiasi cha Sh 172,070,470.

“Tunadhani kumefanyika ujanja wa kutudhulumu mafao kwani hata mchanganuo wa nani kapata kiasi gani kutoka katika hizo Sh milioni 172 hatujapewa. Na inavyoonekana marehemu hawezi kulipwa kiasi hiki (Sh milioni 88) ukilinganisha na miaka aliyofanya kazi,” anasema Salome.

Katika barua hiyo, Salome, anawatuhumu baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushiriki kuhujumu mafao yake halali.

Katika mirathi hiyo, pamoja na Salome, wanufaika wengine ni Makumbula Andrew, Sabrina Andrew, Faidhana Andrew, Kida Juma, Celina Juma, Cecilia Nassoro (marehemu) na Agness Nassoro.

Barua ya Reynolds ya Juni 2, mwaka jana ambayo ni majibu kwa hoja za Salome na wenzake sita, inasema malipo ya mwisho ya Sh milioni 172 yameshafanywa kulingana na wosia wa marehemu Andrew lakini Salome anasema kiasi hicho si walicholipwa.

“Tunasema hivyo kwa sababu hata aliyekuwa Kaimu Balozi, Inmi Patterson, alishakiri kuwa kuna matatizo kwenye ulipaji mafao ya marehemu Andrew na akaahidi kushughulikia tatizo hilo. Akatuhakikishia kuwa malipo tuliyokuwa tumepokea yalikuwa ya awali tu, na kwamba malipo ya pili yalikuwa yanakuja. Baada ya taarifa tukaambiwa ameondoka kurejea Marekani.

“Ndiyo maana majibu yenu ya Oktoba 7, 2020 ya kwamba tumeshapewa Sh milioni 172 yalitushitua mno. Kama kweli mlishatupatia hizo fedha tupeni uthibitisho, ukiwamo mchanganuo wa asilimia kulingana na wosia ulioandikwa,” amesema Salome.

Mjane huyo katika barua yake ya Agosti, 2020 ameandika kwa urefu juu ya ‘zengwe’ la ulipwaji mafao, akisema dalili mbaya za kudhulumiwa zilianza kuonekana muda mfupi baada ya kifo cha mumewe.

“Mume wangu alipofariki dunia niliulizia mirathi yake, Mei, 2019 mliniandikia barua mkisema msingetoa mirathi bila hukumu ya mahakama ya kunitambua kama msimamizi wa mirathi. Mliniagiza kufanya hivyo mkitambua kuwa mlikuwa na mamlaka kisheria ya kutoa mirathi kwa sababu taarifa zote za warithi mlikuwa nazo – ndiyo maana nasema tangu awali kabisa kulikuwa na dalili za mchezo mchafu.

“Baada ya kufuata taratibu zote za kimahakama, nilipitishwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu Andrew Septemba 23, 2019. Niliandika barua kwenu nikiambatanisha na hukumu ya mahakama, lakini bado ubalozi haukuchukua hatua zozote. Mlikaa kimya bila kujibu barua zangu licha ya kwamba ni ninyi hao hao mliotaka nipate kibali cha mahakama.

“Ukimya wenu ukanifanya nihisi kuwa huenda kulikuwa na mchezo mchafu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya maofisa katika ubalozi wenu. Novemba 29, 2019 kwa mshangao nikapokea simu kutoka kwa mmoja wa maofisa wa ubalozi akinitaka niende Benki ya CRDB nitazame akaunti yangu.

“Nilienda kuangalia na kukuta Sh 34,534,553 zisizokuwa na maelezo wala mchanganuo wowote. Baadaye akanipigia simu tena na kunitaka niende ubalozini nisaini kukiri kupokea fedha. Ubalozini nilipofika nikapewa karatasi ya kawaida nisaini – ilikuwa karatasi ya ‘kihuni’ mno ambayo huwezi kuamini inaweza kutolewa kwenye ubalozi wa nchi kubwa kama Marekani. Kwa mujibu wa ofisa wenu Boston Straun, nilistahili kulipwa mirathi inayotokana na bima ya maisha, malimbikizo ya mishahara ya likizo, na pensheni ya miaka 30 ambayo marehemu mume wangu amefanya kazi katika ubalozi wenu.

“Kwa hesabu za kawaida kabisa za mwanafunzi wa shule ya msingi marehemu asingelipwa Sh milioni 34 kama malipo yake kamili. Kitinda mimba wa marehemu aitwaye Joshua hakuwekwa kwenye mirathi licha ya kwamba ubalozi ulikuwa unamtambua na kumgharimia matibabu yake – na stakabadhi zipo. Ilishangaza kuona watoto ambao hata hawakuwa wa marehemu waliwekwa kwenye orodha ya mirathi,” amesema Salome.

Amesema baada ya kuona sakata hilo kupitia kwa mwanasheria wake akauandikia ubalozi barua ya kutaka apewe mchanganuo wa stahiki za marehemu mumewe. Akataka pia kujua kigezo kilichotumika kuamua mirathi iwe Sh milioni 34 pekee.

Bado ubalozi haukumjibu na ndipo alipoamua kuandika barua Ikulu kuomba asaidiwe kupata stahiki zake.

Desemba Mosi, 2020 Selestine Kakele kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alimwandikia barua Salome alimhakikishia kuwa wizara imeomba kukutana na ofisa mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani ili wapate majibu ya mgogoro huo.

“Wizara inapenda kukujulisha kwamba imeshatuma malalamiko haya mapya dhidi ya Ubalozi wa Marekani juu ya mirathi ya marehemu mume wako na kuomba walete mchanganuo wa malipo ya mirathi ambao unaonyesha ni kiasi gani ulistahili kulipwa, na kiasi gani kimelipwa na wanufaika gani wamelipwa katika malipo hayo,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Utata zaidi

Mchanganuo uliotolewa baadaye na Ubalozi wa Marekani kupitia barua yake ya Juni 29, 2021 unaohusu malipo ya Sh milioni 172 (ambazo Salome anakana kuzipokea), unazidisha utata wa suala hili.

Awali, ubalozi uliainisha kiasi cha mirathi na asilimia za kila mnufaika kama zilivyoainishwa kwenye wosia. Salome anasema: “Mmeonyesha mimi (Salome nililipwa Sh 34,534,553; Celina (Sh 4,586,393), Sabrina (Sh 6,592,690), Faidhana (Sh 4,586,393), Kida (Sh 4,586,393), Makumbula (Sh 22,083,635) na Agnes (Sh 94,380,413). Hii jumla yake ni Sh 172,070,470. Huu ni uongo mtupu.

“Kwa mujibu wa wosia uliowekwa saini na Andrew mwaka 2007, kiwango mlichoandika hapa kinatofautiana na kile mlichotoa Juni 29, 2021 na ambacho kilisainiwa na Reynolds.”

Kwa mujibu wa nyaraka za wosia, Salome alistahili kulipwa asilimia 20, Celina (10%), Sabrina (15%), Faidhana (10%), Kida (10%), Makumbula (15%) na Agnes (10%).

“Ukipiga hesabu za hizo asilimia kutoka kwenye malipo ya Sh milioni 172 wanazodai tumelipwa, utaona udanganyifu wa hali ya juu. Haziendani kabisa na hicho nilichokueleza hapo juu.

“Chukua mfano mmoja tu wa Agnes. Barua ya Reynolds inatulazimisha tuamini kuwa Agnes alilipwa Sh 94,380,414 kutoka kwenye kiasi cha Sh 172,070,470 lakini kwenye hati ya wosia iliyosainiwa na Andrew mwenyewe Januari 8, 2007 inaonyesha asilimia za Agnes ni 10. Kwa hiyo asilimia 10 ya Sh 172,070,470 ni Sh 17,207,047. Huu ni mkanganyiko mkubwa. Ndiyo maana tunauliza, kati ya michanganuo hii miwili kutoka ofisi moja tuamini upi?

“Ndiyo maana tunahisi fedha zetu zimechukuliwa na baadhi ya maofisa wa ubalozi na sasa wanajitahidi kutudanganya wakiamini sisi ni wajinga,” amesema Salome.

JAMHURI limewasiliana na maofisa wa Ubalozi wa Marekani kupata ufafanuzi wa madai ya Salome na wenzake bila mafanikio. Licha ya kupelekwa maswali kwa barua pepe kama walivyotaka tangu Januari 27, mwaka huu; hadi wiki iliyopita walikuwa hawajajibu. Mara kadhaa JAMHURI limewasiliana nao kwa simu ili kupata majibu, lakini hakuna ushirikiano wowote uliotolewa.