Matukio ya kubakwa watoto wa kike wenye umri chini ya miaka 18 katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro yanaongezeka licha ya baadhi ya washitakiwa kufungwa jela.
Taarifa zinaonyesha kuwa kati ya Januari, mwaka jana hadi Mei mwaka huu, mashauri 34 yamefunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same. Washitakiwa watatu kati ya hao wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja; na mmoja amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Washitakiwa hao ni Joel Mrutu aliyembaka msichana mwenye umri wa miaka 17 katika shauri la jinai namba 87/2018, Elitwaza Mbwambo aliyembaka mtoto mwenye umri wa miaka 11; na Isaac Eliet aliyembaka msichana mwenye umri wa miaka 16.
Yumo pia Adam Athuman Mtengi ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 16 katika shauri la jinai namba 181 la mwaka 2018.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Same, Judith Kamala, amezungumza na JAMHURI ofisini kwake na kukiri kuwa kuna mashauri mengi ya watuhumiwa wa ubakaji na ulawiti.
Bila kuingia kwenye undani, Hakimu Kamala anasema katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana mashauri 17 ya ubakaji na ulawiti yalifunguliwa katika Mahakama hiyo; na idadi kama hiyo kuanzia Mei, mwaka huu.
Mmoja wa mawakili wa Serikali aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina anasema ongezeko la ubakaji na ulawiti wilayani Same ni jambo linalosikitisha kwa kuwa watoto wanaathirika kisaikolojia.
Anasema kuna changamoto kadhaa zinazokwaza usikilizaji wa mashauri hayo. Miongoni mwazo ni mashahidi kutofika mahakamani kutoa ushahidi.
“Pamoja na adhabu kutolewa kwa wahusika, lakini bado matukio ni mengi. Mashahidi hawatoi ushirikiano. Tatizo jingine ni umaskini ambao nao huchangia mashauri mengi kufa,” anasema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi (OCD) Wilaya ya Same, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Irene Richard, anasema katika kipindi cha Januari hadi Desemba, mwaka jana kesi 44 za matukio ya unyanyasaji dhidi ya watoto zilifunguliwa; kati ya hizo, kesi tano zikihusisha watoto wa kiume na 39 zikihusisha watoto wa kike.
Akitoa taarifa kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika wilayani Same, amesema katika kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu, kesi 31 zilifunguliwa na kati ya hizo 28 zilihusisha watoto wa kike.
“Kwa takwimu hizi hakuna shaka kuwa watoto wa kike ndio waathirika wakubwa wa matukio ya unyanyasaji ikilinganishwa na watoto wa kiume ambako katika kesi 34 zilizofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same, kuna kesi mbili zinazohusisha watoto wa kiume kulawitiana.
“Kesi nyingi zilizofunguliwa polisi zilihusisha matukio ya ubakaji, kunajisi, kulawiti, utupaji wa watoto na shambulio la kudhuru mwili na katika kesi 21 zilizofikishwa mahakamani, kesi mbili zilitolewa uamuzi,” anasema.
Kamati yaundwa
Katika kukabiliana na vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto, Halmashauri ya Wilaya ya Same imeunda kamati za ulinzi na usalama wa mama na mtoto zikihusisha kata zote 34 za wilaya hiyo.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Same, Victor Kabuje, amesema kuundwa kwa kamati hiyo ni miongoni mwa majukumu ambayo halmashauri hiyo imepewa ikiwa ni mkakati wa Serikali kuhakikisha watoto wanalindwa.
Majukumu mengine ni kutoa elimu kwa jamii juu ya ulinzi na kumwendeleza mtoto ili kuondoa ukatili kwa kuzingatia Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009.
Mengine ni kuhakikisha watoto waliofanyiwa ukatili wanasimamiwa katika mashauri yanayofunguliwa mahakamani kwa usimamizi wa ofisa maendeleo ya jamii na dawati la jinsia la polisi.
“Halmashauri inalo jukumu la kuunganisha wadau waliopo wilayani ikiwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, vituo vya kulea watoto na wadau wengine muhimu katika suala la ulinzi na usalama wa mtoto,” amesema.
Kuhusu mimba za utotoni, Kabuje anasema zimepungua kutoka 26 mwaka jana hadi nne Mei mwaka huu. Sababu za kupungua ni kampeni iliyoendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Sitaki.