Rais Donald Trump wa Marekani ametukumbusha tena kuwa yeye ni mbaguzi wa rangi, tena wa kiwango cha kustahili nishani. Katika majadiliano hivi karibuni juu ya uhamiaji akiwa na viongozi wa Baraza la Seneti, na wa Baraza la Wawakilishi, Trump alikashifu watu na nchi za Haiti, El Salvador, na za Afrika.
Alitumia neno kufananisha nchi hizo na za Afrika lenye maana ya shimo la choo, lakini maana hasa ni kusema nchi hizo kuwa ni chafu, hazikaliki, na hazipendezi kwa hali yoyote.
Maneno kama haya, na hata mabaya kuliko haya, yanasemwa kila wakati na watu wa kila aina, na pengine hata na marais wenzake waliomtangulia. Bahati mbaya kwake yamevuja. Kuyasikia kutoka kwa rais wa Marekani, anayeongoza raia milioni 300 ambao baadhi yao wanatoka kwenye maeneo hayo anayoyafananisha na choo ni jambo la kushangaza.
Uongozi, siyo wa Marekani tu, ni suala ambalo linalazimisha kiongozi kuwa na mienendo ya staha na kujiheshimu inayoendana na jukumu hilo. Inavyoelekea Trump au haelewi hilo, au hajali kuwa maana ya kuwa kiongozi ni kuheshimu ofisi yake, na kuheshimu wengine.
Lakini kutokujali na kutokuelewa kwake hakumpi kinga dhidi ya shutuma anazostahili kwa kujishusha kutoka kwenye ngazi ya juu ya uongozi na kuwa msema hovyo.
Wanaofuatilia matamshi yake hawashangai sana kwa sababu wanaona kuwa ni mlolongo wa aina ya matamshi na misimamo ambayo anayo bila kutafakari athari zake. Yeye mwenyewe, baada ya kutafakari matamshi ambayo yameshutumiwa kila upande ametafakari na kuyakanusha, pamoja na kwamba Ikulu yake ilikiri mapema tu kuwa aliyasema.
Afrika, nchi zote huru 54 na watu wake zaidi ya bilioni 1.2, tumefananishwa na choo kimoja kikubwa. Tunapaswa kuchukizwa na suala hili, lakini na tunafarijika kuwa Umoja wa Afrika (AU) umetoa tamko kali kushutumu kauli ya Trump.
Aidha, tukubali pia kuwa watu kama Trump wanapata mwanya wa kudhihirisha hulka yao ya kibaguzi kwa sababu ni kweli kuwa Afrika inaandamwa na matatizo ya kila aina, mengine ya kujitakia, mengine yanayosababishwa na wengine.
Pamoja na utajiri mkubwa wa maliasili wa Bara la Afrika, utajiri huu unaishia mikononi mwa Waafrika wachache na kunufaisha zaidi nchi tajiri ambazo viongozi wake, kama Trump, tunawapa sauti ya kututukana. Usimamizi mbovu wa maliasili, unaochochewa na ufisadi wa sehemu kubwa ya viongozi wa Afrika unasababisha Waafrika kubaki fukara, na kuwa sababu mojawapo inayokuza wimbi la Waafrika wanaokimbia nchi zao kwenda Ulaya na Marekani kusaka nafuu ya maisha.
Inakadiriwa kuwa mwaka 2017 kati ya jumla ya wahamiaji milioni 258 wa dunia nzima, idadi ya wahamiaji kutoka Afrika walifikia milioni 36. Mwaka huo huo Marekani ilikuwa na wahamiaji milioni 50, ikiongoza ulimwenguni kama nchi inayokaliwa na wahamiaji wengi zaidi.
Tutaendelea kunyanyaswa, kutukanwa, na kudhalilishwa mpaka tutakapoweza kusimamia masuala yetu na kuhakikisha kuwa matatizo yanayowasukuma Waafrika kukimbia nchi zao na kuomba kuishi Ulaya na Marekani yanapunguzwa au kumalizwa kabisa.
Wabaguzi kama Trump wapo na hawataisha, na wanaendelea kuzaliwa kila siku. Hilo hatuwezi kubadilisha, lakini jambo ambalo tunaweza kulifanyia kazi ni kubadilishwa kwa fikra zetu.
Kwanza, kubadilisha mawazo ya kujihisi wanyonge, tunaoonewa, na kudhalilishwa wakati wote tukiamini kuwa hatuna uwezo wowote wa kuboresha hali yetu sisi wenyewe. Afrika siyo maskini. Bara Afrika ni tajiri kwa watu na rasilimali.
Mwaka 2012 nchi zinazoendelea zilipokea jumla ya dola trilioni 1.3 za Marekani za misaada kutoka nchi zinazoendelea. Hii thamani inajumuisha misaada, thamani ya miradi ya uwekezaji, na mapato mengine. Mwaka huo huo nchi zinazoendelea zilihamisha thamani ya bidhaa ya dola trilioni 3.3 za Marekani kupeleka nchi zinazoendelea.
Thamani ya utajiri uliohamishwa kutoka nchi zinazofananishwa na choo ilikuwa no dola trilioni 3.3. Hatupaswi kujisikia wanyonge, tunapaswa kukubali kuwa sisi ni wajinga.
Ujinga huu unanifikisha kwenye suala la pili la kutafakari. Waafrika tunapaswa kuchukua hatua gani kuziba mianya ya huu utajiri unaohamishwa kiholela kwenda nje na kuwapa watu nafasi ya kututukana?
Naamini tunahitaji mtazamo mbadala kuondoa ule wa kusifia uwekezaji kama suala la kutuletea ajira, teknolojia, na uzoefu. Uzoefu ndiyo, lakini siyo uzoefu tunaoambiwa; huu ni uzoefu wa kupewa dola trilioni 1.3 na kutoa dola trilioni 3.3. Tunachohitaji ni kujijengea uzoefu wa kuongeza utajiri tunaobaki nao mkononi.
Kujiongezea utajiri kuna maana ya kuwapunguzia utajiri wale ambao wananufaika na rasilimali iliyopo. Na hili linahitaji nchi za Afrika kuongeza ushirikiano miongoni mwao katika maeneo ya uchumi, miundombinu, mawasiliano, na siasa ili kuweza kuhimili mfumo uliopo unaokoleza umaskini na unyonge wetu wa kifikra. Umoja utaongeza sauti ya Waafrika kutetea maslahi yao na kuruhusu kasi kubwa zaidi ya maendeleo ambayo, miaka 60 baada ya uhuru wa nchi nyingi za Afrika, bado haijafikia hatua ya kuridhisha ili kusitisha Waafrika kukimbia nchi zao.
Afrika ni bara la vijana. Maeneo yote mengine ya ulimwengu yana watu wanaozeeka. Jambo ambalo tunaambiwa linaathiri maendeleo ya watu – kuzaa holela – ni suala ambalo linaweza kuwa chanzo cha kuibuka kwa Afrika imara. Fikira mpya zinapaswa kuambatana na udhibiti wa kiwango fulani cha ongezeko la watu kuwiana na uzalishaji wa chakula unaotosheleza mahitaji. Ukiongeza uchumi imara, uimarishwaji wa demokrasia, na umoja, hakuna shaka kuwa Bara la Afrika litajitokeza kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza ulimwenguni.
Trump tunapaswa kumshutumu na kumshukuru. Tumshutumu kwa kupayuka hovyo bila kuheshimu hadhi yake kama kiongozi, lakini tumshukuru kwa kutukumbusha masuala tunayopaswa kutekeleza ili kuzima kabisa dharau na kejeli kwa Afrika na watu wake.