Katika sehemu ya kwanza ya makala hii nilieleza aina mbalimbali za ubabe na kuonyesha madhara yake kwa jamii. Nilionyesha jinsi ambavyo ubabe wa wanyama unavyokuwa na jinsi ambavyo baadhi ya viongozi waliiga ubabe huo wa wanyama na tukaona mwisho wao ulikuwaje.
Katika mifano yote niliyotoa, hakukuwa na hata mfano mmoja ulioonyesha kuwa kiongozi mbabe alifanikiwa. Iwe katika siasa au uongozi wa nchi, hakuna sehemu yoyote ambapo watu walifanikisha mambo yao kwa kutumia ubabe. Unaweza kupata faida ya wakati mfupi tu lakini haitadumu. Ndiyo sababu ninasema ubabe hauleti tija yoyote katika madai.
Viongozi wetu wa vyama vya siasa kweli hawalijui hilo? Huu ubabe ni wa nini katika nchi hii ya amani na umoja?
Kuanzia pale Mwalimu Julius Nyerere aliposhauri kuacha ushindani na ubabe na kutaka zitumike njia za kistaarabu watu wanapodai kitu fulani, tukaona mkoloni ananywea na kusema Tanganyika itafanya uchaguzi mwaka 1958. Tangu uchaguzi huo wa kwanza wa mwaka 1958/59, mpaka leo hii mwaka wa 2020 tutakuwa tumeshafanya uchaguzi mara 14 hivi. Kati ya hizo, zipo zilizofanyika chini ya mfumo wa vyama vingi va siasa, kabla na baada ya Uhuru. Baadaye tukafanya uchaguzi mwingine mara kadhaa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa baada ya mfumo wa vyama vingi kufutwa.
Baada ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa katika miaka ya mwanzo ya 1990, Tanzaania ikarudi kwenye uchaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi ikiwa na uzoefu na mfumo huo kwani ulishawahi kutumika zamani.
Je, kwa kufanya uchaguzi mara 14 chini ya mifumo miwili tofauti ya siasa kweli tutakosa uzoefu wa kutosha? Baada ya kila uchaguzi kunajitokeza dosari/kasoro ambazo zinaboreshwa katika uchaguzi unaofuata. Kwa uzoefu huo sidhani kuwa bado hatuna ufundi wa kutosha kuendesha uchaguzi nchini.
Lakini kwa kampeni za ubabe hapo sina uhakika wa uzoefu. Ninasema hili wazi kwa maana niliona kwa mara ya kwanza hapa Dar es Salaam kampeni ya kupakana matope mwaka ule 1965 pale Wana Dar es Salaam wawili, aliyekuwa Mstahiki Meya wa jiji akiitwa mzee Ramadhani Kirundu na aliyekuwa Ofisa wa Polisi mzee Kitwana Kondo, wakirushiana madongo kwenye kampeni za kuwania ubunge wa Dar es Salaam. Mzee Kitwana Kondo alishinda.
Ninakumbuka wagombea hawa walipofika Chang’ombe kuomba kura eneo la Maduka Mawili, Mtaa wa Saranda katika viwanja vya Jamatini, mwisho wa mkutano wa kampeni, mzee Kirundu akihitimisha kujitangaza kwake alitamka kwa masikitiko akisema: “Laiti ningalijua kwamba kuomba kura kwenyewe kuko namna hii ya kukashifiana hadharani mimi nisingeliomba huo ubunge.”
Huko ni kukiri hadharani kuwa hapakuwa na kampeni za kistaarabu hata kidogo. Ulijaa ubabe, ukabila, u-mjini wa hapa Dar es Salaam na wala hakukuwa na kutangaza sera za TANU. Palikuwa na alama ya jembe na nyumba tu! Sasa wagombea wale walitakiwa watuelezee ubora wao kwa kutuelewesha uzuri au ubaya wa alama ile ya jembe au ya nyumba ndiyo sera yenyewe. Basi kwa kutumia ubabe wao wa mjini, walikashifiana tu pale. Ni ubabe usiokuwa na tija. Matokeo kampeni za ubabe baada ya kila uchaguzi zinatokea kesi za kupinga matokeo mahakamani. Hapo hakuna tija.
Siasa hizi za ubabe zimeibuka siku za hivi karibuni. Kwa wale Wana Dar es Salaam ninadhani bado wanakumbuka lugha ya chama kimoja walipojiita wao ni “ngangari” na hapo Jeshi la Polisi wakajitambulisha kama wao ni “ngunguri”. Matokeo ya ubabe ule risasi zilirushwa kule Mbagala Zakhem. Sioni tija yoyote katika mazingira kama hayo.
Kwa nini tufike mpaka pale serikali inalazimishwa kutumia silaha? Chama kimoja pale Mwembe Yanga kilijikita katika kuelezea ufisadi wa viongozi katika chama tawala. Pale hakuna sera ya chama iliyoelezwa. Ila ni kashfa za ufisadi.
Haki kwa wote
Wakati wa kampeni za uchaguzi kila chama kinakuwa muwamba ngoma, hivyo lazima avutie ngozi upande wake ili ashinde, ashike dola na aongoze nchi. Je, ni lazima kutumia mneno y kashfa katika kujitangaza?
Ratiba za kampeni ziwe sawa, muda wa kampeni uwe sawa na mazingira wakati wa kampeni yawe sawa kwa vyama vyote. Haya ndiyo mambo yanayotakiwa.
Mkoloni alihujumu kampeni za TANU mwaka 1958/59 kwa kutumia ubabe, haikuwa sahihi. Mwalimu Nyerere aliwahi kutuasa kuwa ubaguzi wa aina yoyote ile ni ukaburu tu. Hivyo Watanzania tukiminya muda wa kampeni kwa wengine na kupendelea wengine hilo ni sawa na ubaguzi ule ule wa ukaburu.
Tume ya Uchaguzi imepata uzoefu wa kutosha kuandaa uchaguzi wa vyama vingi tangu mwaka 1995 mpaka sasa. Moja ya maboresho muhimu ni katika nyanja za wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo wawe makini na watende haki kwa vyama vyote.
Nchi yetu imepiga hatua kubwa sana katika masuala haya ya uchaguzi. Haitapendeza hata kidogo kusikia mazonge mazonge katika vituo vya kupigia kura wala kuona fujo za aina yoyote.
Mabaunsa wa vyama mbalimbali pale ni alama za ubabe. Hilo halikubaliki.
Kwa vile Katiba tunayotumia hivi sasa inasema wazi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa au kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi; Kila raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi. Hapa imewekwa wazi kuwa ushiriki wake huu unakuwa katika kuchagua (ndiko kupiga kura yake) au kuchaguliwa (ndiko kugombea uongozi).
Hapo basi ufikapo wakati muafaka wa uchaguzi, mtu awe huru kabisa kutumia huo utashi wake bila kubughudhiwa. Hilo ni moja ya mahitaji ya elimu ya uraia inayolenga kumwelimisha mpiga kura na mpigiwa kura. Sioni sababu za kutokea ubabe hapo, kwani sheria ziko wazi. Wasimamizi wanatambulika, mawakala wanatambulika, sasa ubabe utaanzia wapi?
Wasomaji wa makala hii, ninaamini wengi wetu tuliona historia imewekwa Machi 3, mwaka huu Rais na Mwenyekiti wa chama tawala akifungua mikono yake na kuwapokea viongozi wakuu wa vyama vya siasa vya upinzani pale Ikulu. Rais aliongea kwa faragha na kila kiongozi wa chama. Alianza na Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT – Wazalendo, akaja Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF na kisha alimpokea James Mbatia wa NCCR – Mageuzi.
Kwa wale tulioona kupitia runinga tunaamini maongezi yale yalikuwa kwa manufaa, kwa amani na umoja wa taifa letu. Kila kiongozi alipokuwa akitoka kwenye maongezi alionekana mwenye uso wa furaha na uliojaa matumaini. Hii ni hatua nzuri, na ni matayarisho ya huo uchaguzi ulio huru mwishoni mwa mwaka.
Lakini kuna swali katika vichwa vya wananchi; vipi, mbona uongozi wa chama kikuu cha upinzani bungeni haukujitokeza? Kulikoni? Au ndiyo ile ile tabia ya ubabe ninaouita hauna tija hapa nchini? Penye kutafuta maridhiano kuna kutoa na kupokea. Kwa msomi yeyote kama mimi, hii ni njia pekee ya kuelekea maridhiano.
Lakini kupokea tu ni unafsi, ni uchoyo na ndiyo chanzo cha tabia ya ubabe! Mbatia ametamka kuwa si tabia nzuri vyama vya siasa kukamiana. Huko kukamiana, mimi ninaita ubabe.
Nihitimishe kwa kuomba sote mwaka huu tuendeshe uchaguzi wetu kistaarabu. Kwanza, tumtangulize Mwenyezi Mungu katika yote hayo. Pili, tufuate taratibu zilizowekwa kwa uchaguzi huo. Nchi yetu sasa imekomaa kisiasa na viongozi wetu wa siasa wote ni watu wazima wa umri wa miaka 60 na zaidi na ni wazalendo na waliopikika katika kambi za JKT.
Mwalimu wangu wa Kiingereza pale St. Mary’s Tabora alipata kutuambia msemo lakini hatukuelewa, alisema: “Boys, set a thief to catch a thief”. Usemi ule kumbe ulikuwa na maana kuwa kila mwizi hamwamini mwizi mwenzake. Kwa hali hiyo ukiona mtu hakuamini, ujue wazi yeye mwenyewe si mwaminifu.
Na katika uchaguzi ukiona viongozi wa chama hawaamini mamlaka husika, basi ni wazi pia wao wenyewe hawaaminiki kitabia hata ndani ya chama chao.