Mahakama Kuu Kanda Mtwara imetoa zuio la muda dhidi ya matumizi ya Kanuni za Maudhui ya Kimtandao (Online Content Regulations) hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu maombi ya walalamikaji yaliyowasilishwa.
Maombi hayo yaliyowalishwa mahakamani na waombaji 6 wakiwemo Jamii Media, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) na Jukwaa la Wahahari Tanzania (TEF).
Mahakama imezuia kwa muda ukomo wa tarehe 5 Mei 2018 uliokuwa umetolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikitaka watoa huduma za habari kwa njia ya mtandao (Runinga, Redio, Blogs, Forums) wawe wamejisajili ifikapo tarehe tajwa hapo juu.
Zuio hilo limewekwa kusubiri kusikilizwa na kuhamuliwa kwa uamuzi wa maombi ya kibali cha ambacho kimeombwa ili wadai waruhusiwe kuomba kufuta uamuzi wa wadaiwa, kuwaagiza wadaiwa kutekeleza wajibu kwa mujibu wa sheria na kuomba kuwaamuru wadaiwa wasirudie tena hicho kitendo.
Katika kesi ya msingi ya mapatio ya kanuni hizo washitakiwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kesi ya msingi imepangwa kusikilizwa tarehe 10 Mei 2018.