Kama hujamsikia Aung San Suu Kyi, fungua macho upate somo la unafiki mkubwa unaotawala ulimwengu wetu enzi hizi.

Su Kyi ni kiongozi wa Myanmar mwenye wadhifa unaofanana na wa waziri mkuu ambaye ni maarufu kama mwanaharakati aliyepinga utawala wa kijeshi wa nchi yake kwa miongo kadhaa na kusababisha kutumikia kifungo cha nyumbani kwa karibia miaka 20 hadi kufikia mwaka 2010.

Ni ushindi wa asilimia 86wa chama chake cha siasa wa viti bungeni katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uliyompa wadhifa wake wa sasa.

Majenerali wa nchi hiyo aliyowapinga na waliyohodhi madaraka kwa zaidi ya miongo mitano walijiandaa vyema kushindwa kwenye uchaguzi, kama ilivyotokea mwaka 2015, lakini hawakuwa tayari kuachia uongozi. Kwa sababu hiyo, katikakati ya nchi hiyo, walitenga asilimia 25 nafasi za viti vya bunge kwa wanajeshi pekee. Kipengele kinachohitaji asilimia 75 ya wabunge kupitisha mabadiliko ya katiba kinawalinda dhidi ya hatua zozote za kuwaondolea nafasi yao ya upendeleo.

Isitoshe, wizara muhimu za ulinzi, mambo ya ndani, na mipaka zimetengwa mahususi kuongozwa na wanajeshi.

Nguvu hiyo ni chanzo cha nchi hiyo na serikali inayoongozwa na Suu Kyi kupakwa doa kubwa kutokana na kampeni za kijeshi za Agosti, 2017 dhidi ya kikundi kijulikanacho kama Arakan Rohingya Salvation Army (ARSA) kilichoshambulia vituo vya polisi na jeshi.

Kampeni ya kijeshi kujibu mapigo imelenga siyo wapiganaji wa ARSA pekee, bali malaki ya raia wa jamii ya Warohingya ambao sasa wamekimbia makazi yao, ikikadiriwa zaidi ya 700,000 kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh wakijinusuru kutokana na tuhuma dhidi ya jeshi la Myanmar za mauwaji, ubakaji, na kuteketezwa kwa vijiji vyao. Ni tuhuma ambazo Umoja wa Mataifa umebaini zina ukweli na ambazo zimeanza kuchunguzwa na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC).

Yote haya yakitokea wengi wa wale waliounga mkono jitihada za Suu Kyi kupigania haki na demokrasia nchini mwake dhidi ya utawala wa kijeshi walitarajia kusikia sauti yake angalau ikishutumu vitendo hivi.

Anapoongelea tatizo lililopo anasema tatizo si kubwa kama linavyosikika. Anakataa kushutumu vitendo vya ukiukwaji wa haki vinavyoripotiwa dhidi ya jeshi. Anaonekana kupata kigugumizi sehemu ambako sauti yake ingesikika ikishutumu vikali yanayotokea.

Tunamshangaa kwa sababu kama ambavyo tungeshangaa na kumlaani vikali Nelson Mandela iwapo, baada ya kuwa kielelezo cha dunia nzima cha harakati dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini, angetoka jela na kushika madaraka ya kuongoza nchi yake halafu afumbie macho na kuzibia masikio vitendo vya ubaguzi na ukandamizaji wa haki za raia nchini mwake.

Ni kweli kuwa washirika wenzake wanajeshi ndani ya serikali ya Myanmar wamejipa madaraka makubwa juu ya usimamizi wa jeshi na polisi, na ni kweli kuwa raia ndani ya serikali hiyo hawana nguvu ya kikatiba ya kutosha kuhoji vitendo vya ukiukwaji wa haki za raia.

Ni kweli pia kuwa upo ubaguzi mkubwa wa waumini wa dini ya Buddha na wa raia wa kawaida wa Myanmar dhidi ya Warohingya ambao, pamoja na kwamba wamo nchini humo kwa vizazi na vizazi, hawana haki ya kupiga kura na wananyimwa haki nyingi za msingi.

Kwa kifupi, Aung San Suu Kyi anaweza kuwa anasita kutetea watu ambao wanaweza kumharibia kisiasa.

Kama alijipatia umaarufu ulimwenguni kama kiongozi ambaye alitetea haki na demokrasia kwa sehemu kubwa ya maisha yake, sasa anadhihirisha kuwa alijijengea sifa ambayo hana. Huwezi kupigania haki na wakati huo huo ukanyamazia dhuluma.

Kiongozi wa kweli atatetea haki hata kama ni yeye peke yake amebaki akitetea haki kwa sababu suala la haki ni suala la msingi na linapaswa kulindwa katika mazingira yote, hata kama litamuumiza anayelitetea.

Uamuzi wa hivi karibuni wa Bunge la Canada wa kumnyang’anya uraia wa heshima aliyopewa na bunge hilo ni mwelekeo mzuri. Ni uamuzi unaotokana na uamuzi wa awali wa ICC wa kuchunguza uhalifu dhidi ya Warohingya.

Sauti za nje ya Myanmar dhidi ya ukimya wa Suu Kyi kuvumilia maovu ni chache, na hazisikiki sana kwa sababu wale vinara wa kufundisha walimwengu juu ya umuhimu wa kuheshimu demokrasia na haki za raia huwa wagumu sana kumsema mtu ambaye wao wenyewe walimuunga mkono na kumjengea sifa. Ni unafiki wa kisiasa ambao ni sehemu ya uhusiano kati ya nchi na nchi, kati ya viongozi na viongozi.

Bunge la Canada linaongeza idadi ya sauti hizo chache zinazokataa unafiki huu. Wengine hawana budi kufuata mfano.

 

…tamati….