Wiki iliyopita katika toleo hili la Uamuzi wa Busara tulisoma jinsi Rais wa Tanganyika alivyokuwa ameunda tume ya kuunda Katiba ya Chama cha TANU, lakini tume hiyo ilikuja pia na mapendekezo ya kuundwa Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano. Endelea…

Tanganyika na Unguja kukubali kuungana

Mwaka 1961, tarehe 9, Desemba Tanganyika ilijipatia Uhuru wake kutoka kwa utawala wa mkoloni – Mwingereza.

Mara tu baada ya miaka mitatu, Unguja nayo ikajinyakulia Uhuru wake kwa mapinduzi ya kuwatimua mabwanyenye

pamoja na sultani wao, ambao kwa siku nyingi walikuwa wakiwanyanyasa wananchi wa Visiwani.

Kwa upande wa Unguja, Chama cha Afro-Shiraz Party (ASP) kikiongozwa na Sheikh Abeid Aman Karume ndicho kilileta uhuru Unguja. Mapinduzi ya Unguja yalifanyika tarehe 12, Januari 1964 mara tu baada ya kupata uhuru wa wachache ambao ulidumu kwa mwezi mmoja tu.

Uhuru ulipatikana mwezi Desemba 1963, na mwezi uliofuata, yaani Januari 1964, mapinduzi yakafanyika. Kwa kweli historia ya Visiwani inasikitisha sana, hasa kuhusu maovu yote waliyotendewa ndugu zetu na dhuluma nyingi za Waarabu pamoja na ubeberu wa Waingereza.

Wananchi wa huko walitumika kama vyombo tu. Wananchi walinyimwa elimu, walinyimwa uhuru wa aina yoyote. Hii ndiyo sababu iliyowafanya wananchi wa huko Visiwani kuungana wote pamoja na kupigania haki na usawa kwa wote, hadi wakafaulu na kuutwaa uhuru wao wenyewe kwa njia ya silaha.

Walikuwa hawana njia yoyote ya kufanya, maana walikuwa wamejaribu chini juu kuupata uhuru wao kwa njia zote za amani lakini wapi!

Tarehe 25, Aprili, 1964, miezi mitatu tu baada ya mapinduzi, Rais wa TANU ambaye pia kwa wakati huo alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu J. K. Nyerere, aliitisha baraza la wabunge wote ili kujadiliana uwezekano wa kudumisha umoja wetu pamoja na ndugu zetu wa Visiwani kwa njia ya kuzifanya nchi mbili ziungane pamoja.

Ingawaje jambo hili lilijulikana mara baada ya mkutano huo, lakini viongozi wote wa pande zote mbili walikuwa wakilizungumzia jambo hili kwa muda mrefu. Baada ya majadiliano ambayo yalionekana dhahiri kuwa kulikuwa na umuhimu wa kuungana, ndipo wajumbe wote kwa pamoja, kwa furaha walikubali kupitishwa kwa suala hilo la Muungano.

Tarehe 26, Aprili 1964, muswada ukapitishwa na JAMHURI YA TANZANIA ikawa imezaliwa chini ya Katiba maalumu ambayo kwa wakati huo ilikuwa bado haijakamilika hadi mwaka 1965 ndipo hasa katiba ya muda iakawekwa kuhusu Muungano wenyewe utakavyoendeshwa.

Muungano wa Tanganyika na Unguja, ni kamilisho la historia ya nchi yetu. Kuna sababu nyingi zilizofanya tuungane kwa haraka na urahisi zaidi. Baadhi ya sababu hizo, ni pamoja na zile Mheshimiwa Rais Mwalimu J. K. Nyerere alizozisema wakati akiwahutubia wajumbe wa BUNGE walioketi kujadiliana kuhusu suala hili tarehe 25/4/1964.

Kwa kifupi ni kwamba, Unguja na Tanganyika ni majirani kwa kila njia. Kwanza, kihistoria, inasemekana kwamba hapo zamani Tanganyika na Unguja zilikuwa nchi moja, ambazo kwa miaka mingi, wananchi wao walikuwa wamoja. Wakati wa ukoloni, tulianza kutenganishwa.

Wenzetu wa Visiwani, waligawiwa Mwingereza pamoja na Kenya. Na sisi huku Tanganyika tukawa chini ya Mjerumani (Mdachi). Tuliendelea na hali hii hadi Mwingereza alipomshinda Mdachi na kuichukua Tanganyika; na Afrika ya Mashariki yote kwa ujumla.

Ingawaje walitutenga, lakini haikutuzuia kushirikiana na wenzetu wa Visiwani kwa mambo yetu ya kawaida. Kwanza kisiasa, urafiki wetu ulizidishwa mara tu baada ya Mwingereza kuchukua mamlaka ya utawala wa nchi zote mbili hizi.

Mnamo mwaka 1927, Tanganyika African Association (TAA) ilianzishwa. Mwaka 1934, mkutano wa pamoja kati ya TAA na African Association (AA) ya Unguja ulifanyika mjini Dar es Salaam. Si hayo tu, bali hata katika miaka ya 1945 na hata 1947, mikutano iliendelea kufanyika Unguja na Dar es Salaam ili mradi kudumisha na kujenga uhusiano wetu imara zaidi.

Katika mwaka 1957, wakati Rais wa TANU Mwalimu J.K. Nyerere alipokuwa anakwenda New York kwenye Umoja wa Mataifa, alipitia Unguja na kuonana na viongozi wa Afro Shiraz Union, na kuwahimiza waendelee na kushika uzi ule ule wa kupigania haki yao, hasa katika kumwondoa sultani.

Si hayo tu, Unguja na Tanganyika ina wananchi wale wale. Wako Wazaramo, Wasukuma, Wanyamwezi, Wamatumbi na kila kabila la Tanganyika liko huko Unguja. Na hata lugha yetu ni moja, yaani Kiswahili. Sote tunaelewana kabisa. Mila zetu na tabia ni zile zile.

Uhusiano wa vyama viwili vya TANU na Afro Shiraz Party haukuanza jana kama mlivyosoma hapo mwanzoni.

Huu ni uhusiano wa tangu zamani sana wakati wa ukoloni. Viongozi wote wawili wa pande zote, wamekuwa wakielewana tangu zamani na shughuli zao zimekuwa zikiendeshwa pamoja kwa faida ya kuwakomboa wananchi wa Tanganyika na Unguja.

Tukiangalia kwa upande wa Bara letu la Afrika, tunaona wazi kuwa, tangu mwanzo kabisa wa PAFMECA na kabla ya OAU; viongozi wote wa nchi za Afrika, wamekuwa wakipigania kuwepo kwa umoja wa nchi zote za Afrika.

Hivyo mara tu waliposikia hatua hii ya kutangazwa kwa Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Unguja, wengi walipeleka pongezi na hongera kwa hatua hii kubwa na ya mwanzo katika kuimarisha Umoja wa nchi za Afrika, muungano huu haukuwa na maana ya kuishia hapo tu, bali uwe kama mfano kwa nchi nyingine katika Bara letu la Afrika.

Sisi tunaamini kuwa “Iwapo nchi mbili zinaweza kujiunga, basi nchi tatu zinaweza. Na iwapo nchi tatu zinaweza, basi nchi nne zinaweza hadi nchi 30 na kuendelea.”

Wakati Mheshimiwa Rais wa TANU, Mwalimu J.K. Nyerere alipokwenda kuzungumza na jamaa zetu wa ASP huko Unguja tarehe 22/4/1964, kabla ya kulipeleka wazo hilo kwa furaha na shangwe, na hii ikazidi kudhihirisha wazi kwamba kweli sote tulikuwa tunaingoja siku hiyo ya kuungana.

Kama tulivyoelezea kuwa, mwaka 1965, Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano ilitengenezwa, lakini ingefaa tuelewe pia kwa nini tunaiita Katiba ya muda. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu J.K. Nyerere, alipokuwa akilihutubia Bunge tarehe 6/6/1970 aliwaeleza wajumbe kuwa: “…..sababu peke yake inayofanya Katiba yetu ikaitwa ya muda, ni kwamba wakati wa muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, tuliharakisha muungano, kwa kutambua kwamba hatua hizo za haraka tu ndizo zingeweza kututimizia shabaha yetu ya kuungana.”

Mwalimu, aliendelea kusema kuwa: “Lakini tusiwe na wasiwasi wa bure kwa ajili ya jina hilo, maana halina sababu ya kuonyesha wasiwasi wowote juu ya utaratibu wetu wa uchaguzi au wa chama chetu.

Kama ilivyo katika vifungu vyote vya katiba hiyo, vifungu hivyo vinaweza kubadilika ikiwa zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge hili wakiamua kufanya hivyo.”