Katika toleo lililopita, sehemu ya tatu tuliishia katika aya isemayo: “Hatupendi wafukuzwe au wafanyiwe ubaguzi wa namna yoyote, lakini Wahindi na Wazungu tuliowakubali ni wale ambao wamekwisha kukubali kukaa Tanganyika daima. Mhindi ambaye bado yuko India au Pakistan si Mtanganyika. Kadhalika Mzungu aliye Uingereza au Ugiriki si Mtanganyika.
“Hao hatuwataki. Hatutaki nchi yetu iwe mahali pa kupunguzia Wahindi, Wazungu au Waamerika waliozidi katika nchi zao. Tutakaribisha wageni wanaokuja kufanya biashara nasi au kuanzisha viwanda maalumu ambavyo ni vya faida kwa nchi nzima…Lakini hatutaki wageni wanaohamia nchini kwa ajili ya kuchukua ardhi walime, ambao mara nyingi ni Wazungu au wale wanaokuja kutafuta maskani ambao hutoka Bara la Hindi, wageni wa namna hiyo hatuoni faida yao katika nchi na kuwakaribisha ni kukaribisha ugomvi kati ya mataifa yaliyomo Tanganyika.” Sasa endelea…
Baada ya hotuba aliyoitoa Mwalimu J. K. Nyerere, wajumbe wa baraza hilo walimhoji. Hizi ni baadhi ya hoja na jinsi alivyozijibu Mwalimu Nyerere.
Reid (New Zealand): Ninafikiri kwamba ingesaidia baraza hili kama Nyerere labda baadaye angewapa
wajumbe orodha ya matawi katika majimbo mbalimbali na uanachama. Ingewezekana akatupa habari hiyo kesho.
Lakini ningependa Nyerere aeleze zaidi madhumuni ya TANU.
Nyerere: Nimekwisha kusema kwamba dhumuni letu kubwa kisiasa ni kuwatayarisha watu wa Tanganyika kujitawala na kuendelea kudai uhuru mpaka Tanganyika imejitawala. Hilo ndilo dhumuni letu la kisiasa. Tuna maana ya kudai uhuru kwa njia ya kikatiba.
Dhumuni jingine la TANU ni kujenga umoja wa kitaifa katika watu wa Tanganyika. Imesemekana, na hii ni kweli, kwamba Tanganyika ina ukabila, na tunafahamu kwamba tunahitaji kuuvunja ukabila huu na kujenga umoja wa kitaifa katika watu wetu. Na hii ni shabaha yetu mojawapo kubwa katika juhudi zetu za kudai uhuru.
Pia tumesema kwamba tutawekea mkazo uanzishaji wa uchaguzi katika masharika au sehemu zote zinazohusu watu, yaani mabaraza ya wenyeji, Baraza la Kutunga Sheria na mengine. Tunapenda mambo ya vyama vya wafanyakazi na vyama
vya ushirika na mpaka sasa tunaye mjumbe wa kamati aliyeko Dar es Salaam ambaye anajishughulisha na mambo ya wafanyakazi.
Tunayo shabaha nyingine ambayo ni kutaka elimu zaidi na bora, msingi bora wa uchumi kwa watu wetu, na kadhalika. Hayo ndiyo madhumuni makubwa ya chama chetu.
Jaipal (India): Ninafurahi kwamba Nyerere amefafanua zaidi jambo hili, lakini bado kuna mambo machache ambayo bado sijayaelewa.
Nyerere anasema kwamba watu wengi wa nchi yake hawana elimu, ningependa kujua namna kutokuwa na elimu huku kunavyohusika katika maisha yao ya kila siku.
Je, hawafuati sheria kwa sasa? Nyerere anasema kwamba watu wake ni washirikina, na mimi pia, lakini serikali yangu haisemi kwamba mimi ni mjinga.
Una maana gani unaposema “Ujinga”? Unayo maana kwamba chama chenu kinataka vifaa zaidi vya elimu kuliko ambavyo serikali inaweza kumudu kwa sasa?
Nyerere: Sidhani kwamba kwa kuwa watu wetu wengi hawakwenda shule kunawafanya wasifuate sheria, inaweza ikawa kinyume.
Kwa kweli ninafikiri kwamba jitihada ya kutaka elimu ni kubwa sana na kwamba kwa sasa serikali au shirika lolote
la kujitolea haliwezi kuimudu. Ujumbe wowote au mtu yeyote anayetembelea Tanganyika mara moja angetambua upungufu wa elimu tulio nao.
Hili ni jambo la kiasili. Sisemi kwamba ninafuata au sifuati sana sheria, lakini ninajisikia kwamba ni mtu bora au ninatakiwa niwe mtu bora, kwa sababu ya elimu niliyopata.
Kwa hiyo ningependa kuona watu wengi wakipata elimu zaidi, kuliko niliyo nayo, kama ikiwezekana. Hilo ndilo jambo tunalofikiria na kama elimu hii itawafanya wafuate sheria zaidi au hapana, siwezi kusema.
Hizo ni baadhi ya hoja na maswali aliyoyajibu Mwalimu Nyerere. Matokeo ya safari hiyo ya New York, kwa matumaini TANU iliyopata kutoka katika Baraza la Udhamini, ni kujiuzulu kwa Mwalimu Nyerere katika kazi ya ualimu na kuendesha Chama cha TANU. (Kujiuzulu huku kumeandikwa katika kitabu hiki).
Kujiuzulu kwa Mwalimu Nyerere katika Baraza la Kutunga Sheria
Serikali ilipomwomba Mwalimu Nyerere kuwa mjumbe wa Dar es Salaam katika Baraza la Kutunga Sheria, hakujua kama akubali au akatae. Wazo lake la kwanza lilikuwa kukataa.
Lakini baada ya kufikiri na kushauriana na wenzake alikubali kwa sababu moja kubwa. Alifikiri kwamba kumchagua kuwa katika Baraza la Kutunga Sheria huenda kukawa ni dalili ya nia njema kwa upande wa serikali.
Aliona ni wajibu wake kukubali ili huo uwe mwanzo wa maafikiano baina ya serikali na TANU. Katika muda wa miezi minne iliyokuwa imepita, Mwalimu Nyerere alikuwa ametoa mashauri mengi ambapo serikali ingeweza kukubali baadhi yake kama kweli serikali ilikuwa ina nia ya masikilizano.
Mara baada ya kurudi kutoka Amerika, Mwalimu Nyerere alishauri kwamba ingawa hatukupenda uchaguzi wa watu
watatu kutoka kila jimbo, tungeweza kukubali wajumbe watetezi 15 wachaguliwe kwa mpango huu, na wale 15 wengine wachaguliwe kwa mpango wa mjumbe mmoja kwa kila jimbo.
Baadaye alirudia kuomba mpango huu katika taarifa aliyoandikiwa Waziri wa Makoloni. Mpango huu alikataliwa.
Mwalimu Nyerere alipokuwa katika Baraza la Kutunga Sheria mwezi Septemba, 1957, alirudia shauri jingine alilokuwa ameliomba katika taarifa ya Waziri wa Makoloni.
Aliiambia serikali kuwa ikiwa haikuweza kubadili idadi ya wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kwa wakati huo, ingeweza kuchagua halmashauri ya kuchunguza jambo hilo, badala ya kusubiri mpaka baada ya uchaguzi wa mwaka 1959.
Kama serikali ingekubali shauri hili ni wazi kwamba baraza hilo lingedumu mpaka wakati mpango mpya ungetolewa na kukubaliwa. Ndiyo kusema kwamba baraza hilo lingeendelea zaidi ya muda wa miaka mitatu, mpango uliokuwa wa TANU mwanzoni.
Katika mkutano wa mwisho Mwalimu Nyerere alitoa azimio lililoomba mambo mawili:-
(a) Kura ya lazima iondolewe. (b) Uchaguzi ufanyike nchi nzima mwaka 1958. Kama serikali ingekubali azimio hilo ombi lake la kwanza lingekuwa limekufa. Uchaguzi ungefanyika nchi nzima; kwa hiari; na kila jimbo lingekuwa na wajumbe
watatu, kama ilivyotaka serikali, yaani Mzungu mmoja, Mhindi mmoja na Mwafrika mmoja.
Azimio la Mwalimu Nyerere lilibadilishwa kwa kuondoa ombi la pili; na kuacha ombi la kwanza tu, kwamba serikali ikubali kuondoa kura ya lazima.
Kama serikali ingekubali ombi hili, ombi lake la pili katika azimio hilo lingekufa. Uchaguzi ungefanyika katika majimbo yaliyochaguliwa na serikali tu, na majimbo mengine yangesubiri mpaka mwaka 1959.
Badiliko moja tu lingefanyika, kura ingekuwa ya hiari badala ya kuwa lazima kwa watu wote watatu. Ilijulikana kwamba serikali ilikuwa tayari kuondoa kura ya lazima; na kupinga azimio hilo ilionyesha desturi mbaya kabisa ya serikali ya kupinga jambo kwa ajili ya kupinga tu, ikiwa jambo lenyewe limetokana na raia.
Kama serikali ingelikubali azimio hilo lililobadilishwa, Dar es Salaam pasingekuwa na uchaguzi mwaka 1958.
Ndiyo kusema Mwalimu Nyerere angeendelea kukaa katika Baraza la Kutunga Sheria kwa kuteuliwa na gavana
ingawa baraza hilo mwaka 1958 lingekuwa na wajumbe 15 waliochaguliwa na raia.
Kwa upande wake hili lingekuwa jambo la fedheha kidogo; lakini alikuwa tayari kukubali fedheha hiyo ili kusaidia kuondoa kero ya kura ya lazima.
Itaendelea…