Wiki iliyopita katika kitabu hiki cha ‘Uamuzi wa Busara’, tulisoma kuhusu uamuzi wa Mwalimu Nyerere kuacha kazi ya ualimu ili apate nafasi ya kuendesha siasa za kuikomboa nchi.

Katika maandiko hayo tuliishia sehemu ambayo wajumbe watatu waliotumwa na gavana wa kikoloni kwenda kwenye Baraza la Kutunga Sheria walipomuona Mwalimu Nyerere akitembea kwa miguu jijini Dar es Salaam katika Barabara ya Morogoro. Nini kilitokea? Endelea…

Akawapungia mkono wakasimamisha gari, akawaambia kwamba alikuwa njiani akienda huko huko kambini kwao, kwa sababu alihitaji kuwaona. Mmoja haraka akajibu: “Haya

vema utatukuta.”  Gari likapigwa moto, wakaendelea.

Mmoja wao akauliza: “Kwanini tusimchukue naye anasema anakuja kutuona?” Mwingine akajibu: “Hapana, yeye amezoea kutembea kwa miguu.” Lakini huyo mmoja akasisitiza kwamba wamchukue. Basi wale wenzake wawili wakasema haidhuru wamchukue, lakini wakasisitiza kwamba asiambiwe juu ya Azimio la Baraza la Kutunga Sheria la kupeleka New York kuhusu ujumbe wa kumpinga!

Hawa walikuwa ni wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria, waliochaguliwa na gavana. Pamoja na matatizo yote hayo Mwalimu Julius K. Nyerere, kiongozi wa TANU, aliondoka kwenda New York. 

Sh 12,000 za nauli zilichangwa, na katika muda wa siku chache tu zikapatikana, akaondoka.

Akafanya kazi yake aliyotumwa na TANU kufanya, akarudi salama Dar es Salaam. Aliporudi kutoka New York, Mwalimu Nyerere alikuta wakoloni wamekwisha kujiandaa kumuondoa katika uongozi wa TANU kwa njia ya hila sana.

Kwa baraka za Mwenyezi Mungu hawakufanikiwa, na ndiyo bahati yetu sisi Watanzania, tukaweza kuwa katika hali hii ya uhuru tulio nao leo. Ndiyo sababu TANU imeamua kuwa inafanya sherehe za kukumbuka siku hiyo.

Wakoloni walipanga mtego wao na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Pugu, kuwa Mwalimu Nyerere atakaporudi kutoka New York, mara moja apewe kuchagua mojawapo kati ya mawili; ama afanye kazi ya ualimu tu aache kabisa siasa; au afanye kazi ya siasa tu aache kabisa ualimu.

Matumaini yao makubwa yalikuwa ni kwamba atachagua kazi ya ualimu, yenye mshahara, kwa sababu walijua wazi kwamba TANU haikuwa na fedha za kumlipa mshahara.

Mwalimu Nyerere alirejea kutoka New York siku ya Jumamosi tarehe 21/3/1955, jioni. Akaenda nyumbani kwake Pugu. Asubuhi yake, Jumapili, tarehe 22/3/1955, Padri Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Pugu akamwita Mwalimu Julius Nyerere katika chumba cha shule hiyo, akamwambia kwamba kutokana na jinsi yeye Julius Nyerere alivyokuwa akijishughulisha sana na siasa, haingewezekana kumruhusu

aendelee na kazi ya ualimu; kwa hiyo alikuwa amemwita ili achague moja kati ya haya mawili: Kazi ya ualimu au kazi ya siasa.

Padri huyo akamshauri Mwalimu Nyerere hivi: “Mwanangu Julius, ualimu na siasa havipatani hata kidogo, fuata oni langu, uache kabisa mambo ya siasa na uzingatie kazi yako ya ualimu.”

Baada ya mkutano huo na Padri Mkuu wa Shule, Mwalimu Nyerere alitoka nje, fikra zimemjaa kichwani, akaenda nyumbani akiyafikiria maneno hayo na akijiuliza afanye nini

wakati huo. 

Swali lililokuwa mbele yake lilikuwa gumu, maana aliambiwa achague kati ya sifa na usalama wa kazi ya ualimu au kujitosa katika bahari ya siasa.

Mwalimu Nyerere alitafuta kichwani mwake jibu la swali hili kwa makini sana. Lakini haikuchukua muda mrefu, akapiga moyo konde, akamwendea Padri Mkuu wa Shule AKAMPA BARUA YA KUJIUZULU.

Hivyo akawa amefanya uamuzi wa kuacha kazi ya heshima, yenye mapato na usalama, mambo ambayo angeyapata akiwa ni Mwafrika wa kwanza Tanganyika kupata digrii.

Badala ya kazi hii nzuri, Mwalimu akakubali kushika kazi ya uongozi wa siasa, kazi ambayo wakati huo ilikuwa na hatari ya kufungwa wakati wowote, kazi ambayo haikuwa hata na uhakika wa mafanikio, kazi ya unabii wa kuwaunganisha watu wote wa nchi ya Tanganyika kuwa taifa moja.

Hatuna budi tukumbuke uamuzi huo wa busara alioufanya kiongozi wetu siku hiyo ya Jumapili tarehe 22/3/1955. Kwa sababu kama angeamua vingine, yaani kuacha uongozi wa siasa na kuendelea na kazi ya ualimu, pengine historia ya Tanzania ingekuwa tofauti kabisa na vile ilivyo leo. Majira yetu haya yangekuwaje sasa…?

Watanzania na Wana TANU tukumbuke tulikotoka, tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa busara na hekima aliyompa Mwalimu Julius Nyerere siku hiyo, busara na hekima ambayo ilimuwezesha kufanya uamuzi mkubwa uliozishinda hila za wakoloni za kujaribu kumwondoa katika uongozi wa siasa ya nchi hii.

Tunapofurahia matunda ya uhuru wetu yatubidi kila mara tukumbuke jasho la mashujaa kama Mwalimu Julius Nyerere, jasho ambalo lilituletea matunda haya.

TANU katika Umoja wa Mataifa (UNO)

Mwaka 1947 ndipo Tanganyika iliwekwa chini ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, na mfalme wa Uingereza alikabidhiwa na baraza hilo madaraka ya kuisimamia

Tanganyika mpaka itakapoweza kujitawala.

Mwaka 1948 ulikuja nchini Tanganyika ujumbe wa kwanza kutoka Umoja wa Mataifa kukagua maendeleo ya nchi na mwaka 1951 ukaja ujumbe wa pili, na mwaka 1954 ukaja

ujumbe wa tatu kwa madhumuni hayo hayo.

Kama ilivyokuwa kawaida, wajumbe hao waliitembelea kila sehemu ya nchi waliyoweza kufika na huko walionana na watu mbalimbali. Chama cha TANU kiliwaeleza viongozi wa matawi yake kwamba wajumbe hao wangetembelea sehemu zao; na kila walipofika viongozi wa TANU walijitahidi kuonana nao na kuwaeleza shida za nchi kama walivyoziona.

Mjini Dar es Salaam, Halmashauri ya Ofisi Kuu ya TANU iliandika taarifa kwa niaba ya wanachama wote wa TANU na wenyeji wa Tanganyika. 

Wajumbe wa ukaguzi walipofika Dar es Salaam walipewa taarifa hiyo na viongozi wa TANU, pia ulifanywa mkutano baina ya wajumbe hao na viongozi wa TANU. Katika mkutano huo viongozi wa TANU waliendelea kutoa maoni yao juu ya maendeleo ya Waafrika.

Mambo makubwa yaliyotiliwa mkazo na viongozi wa TANU wa kila mahali yalikuwa haya:-

1. Umaskini na ujinga ndio ulikuwa mwingi sana katika nchi. Waafrika waliliomba Baraza la Udhamini liisaidie serikali iliyokuwa ikitusimamia kwa fedha na mambo

mengine ili umaskini upunguzwe na Waafrika wapate elimu zaidi.

2. Jambo la Wameru kunyang’anywa ardhi yao na kupewa Wazungu lilisikitisha Waafrika wote, na kuwatia shaka kwamba wao pia ingewezekana kunyang’anywa ardhi yao

wakapewa watu wengine. Kwa hiyo Waafrika wakaomba Wameru warudishiwe ardhi yao na kulipwa fidia ya haki.

3. Ardhi ambayo ilikwisha kuchukuliwa na serikali wakapewa wageni wasiokuwa Waafrika ilikuwa ni kubwa mno. Ikaombwa kwamba ardhi isichukuliwe tena kwa Waafrika na kupewa wageni.