Serikali imepiga ‘stop’ kuendelea kwa mradi wa uchimbaji chuma cha Liganga hadi uhakiki utakapofanyika pamoja na kukamilishwa mambo kadhaa, likiwemo la kurejewa kwa mkataba husika pamoja na kuangalia masilahi ya taifa yafikie kiwango cha juu.
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba kuna masuala yanafanyiwa mapitio, ikiwa ni pamoja na uhakiki wa fidia na muundo wa mkataba.
Mkataba huo wa sasa ambao kimsingi umepigwa marufuku na Rais Dk. John Magufuli, uliridhiwa na Baraza la Mawaziri, Machi 31, 2011, kupitia uamuzi wake namba 14/2010-11.
Baraza hilo la Mawaziri liliridhia kuwa asilimia 20 (zisizo fedha taslimu) ni kwa ajili ya NDC na asilimia hiyo nyingine 80 ni kwa ajili ya Sichuan Hongda (Group) Ltd, na kwamba, NDC iwe na fursa ya kuongeza hisa zake hadi asilimia 49 kwa njia ya malipo baada ya muda wa malipo ya mkopo.
Katika mapitio hayo, suala hilo linapaswa tena kupata baraka za Baraza la Mawaziri la sasa na kisha mradi husika kuweza kuendelea mbele kwa mujibu wa marekebisho yatakayoridhiwa na Baraza.
JAMHURI linafahamu kwamba maombi ya motisha kwa mwekezaji ni mambo yaliyozingatiwa katika mapitio mapya yaliyofanywa na timu maalumu inayoongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.
Moja ya mambo yanayoweza kutupwa katika orodha ya maombi ya mwekezaji huyo ni ombi la kuahirishwa ulipaji Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa muda wa miaka 10 ya mwanzo ya mradi.
Maombi mengine kwenye orodha hiyo ni pamoja msamaha wa kodi kwa vifaa vitakavyoingizwa nchini kwa ajili ya maandalizi ya mradi huo.
Fidia kwa wananchi
Watu takriban 1,145 watalipwa fidia kupisha mradi wa kuzalisha chuma wa Liganga katika kipindi cha kuanzia sasa hadi Juni, mwaka huu.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye alizuia kwa muda uendelezaji wa mradi huo hadi kwanza kufanyike upya uhakiki wa mkataba ili kulinda masilahi ya taifa.
Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Profesa Damian Gabagambi, anasema licha ya uhakiki huo kukamilika, mchakato wa malipo utafanyika kwa uangalifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na wahusika hao kuwapo kwenye maeneo yao, sambamba na utambulisho wao rasmi, na si kufanya malipo kwa kutazama tu majina.
“Uhakiki umefanyika upya na watu 1,145 wanastahili kulipwa fidia, ni matarajio yetu mchakato wa malipo utakamilika ndani ya mwaka huu wa fedha, kuna taratibu za kufuata. Hizi ni fedha za Serikali, ni lazima Hazina kwanza wapate idhini kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika suala hili,” anasema Gabagambi.
“Taratibu hizo zikikamilika, malipo yatafanyika kwa umakini ili kuepuka kulipa watu wasiostahili watakaokuwa wanajaribu kufanya ujanja. Kila mmoja tutamhakiki akiwa kwenye eneo lake na utambulisho wake rasmi,” alisema.
Profesa Gabagambi anaongeza: “Mradi huu ni wa miaka mingi, lakini wakati wote kulikuwa na nia ya kutaka kuchimba, sasa tunaimani Serikali ya Awamu ya Tano itafanikisha mradi huu kuanza. Serikali ya Awamu ya Tano itavunja ile laana ya muda mrefu ya kutokuanza kwa mradi huu kama ilivyokuwa kwa mradi wa kuhamia Dodoma.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dk. Samuel Nyantahe, katika mahojiano yake na Gazeti la JAMHURI anasema anaamini kuwa shughuli za kuendeleza mradi huo zitaanza ndani ya mwezi Machi.
“Tunaamini, serikali imekwisha kujiridhisha na kufanya marekebisho yaliyohitajika kwa masilahi ya taifa. Mambo yataweza sasa kuendelea ingawa serikali itafanya uamuzi wa kubaki na mwekezaji mbia yule yule au itaamua vinginevyo, lakini mradi huu ni muhimu kwa taifa,” anasema Dk. Nyantahe.
Mbia wa sasa katika mradi huo wa uzalishaji chuma Liganga ni China kupitia Kampuni yake ya Sichuan Hongda (Group) Ltd, ambayo pamoja na Tanzania, zimeingia ubia kwa kuanzisha Kampuni inayoitwa Tanzania China International Minerals Resources Ltd (TCIMRL).
Katika ubia huo, Kampuni ya Sichuan ya China ilitakiwa kutoa dola za Marekani hadi milioni 600 kama mtaji (equity) na kisha, mwekezaji huyo pamoja na Tanzania kukopa kwa pamoja dola za Marekani bilioni 2.4 ili kukidhi mtaji wa dola za Marekani bilioni 3, unaohitajika na mradi huo wa uchenjuaji chuma kwa mujibu wa nyaraka.
Lakini pia mwekezaji anapaswa kutoa dola za Marekani “hadi” milioni 600, hiyo haimaanishi kwamba atatakiwa kutoa fedha hizo kwa wakati mmoja.
“Mwekezaji amekuwa na orodha yake yenye maombi kadhaa ya unafuu kwa serikali. Maombi hayo ni pamoja na msamaha wa kodi, kuna maombi ambayo anastahili na kuna mengine yanahitaji marekebisho,” anasema Dk. Nyantahe.
Mtikisiko kimataifa
Endapo mradi huu wa kuzalisha chuma cha pua utakamilika na kuanza shughuli zake, unaweza kusababisha mtikisiko utakaotokana na mgongano wa masilahi katika biashara ya chuma duniani, mtikisiko ambao utaigusa Tanzania dhidi ya mataifa mengine yanayofanya biashara hiyo duniani.
Safari ya mradi huu iliyoanza na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, mwaka wake wa kwanza tu Ikulu, ambaye kupitia Baraza la Mawaziri, iliridhiwa kuwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) liendeleze mradi huo, inatajwa na wachunguzi wa biashara za kimataifa kuwa utakuwa changamoto kwa Tanzania.
Wachunguzi hao wanaamini kuwa huu ni mradi utakaogusa masilahi ya nchi kubwa na zenye nguvu kiuchumi na kati ya nchi hizo ni pamoja na Marekani.
Kwa takwimu za Shirika la Kimataifa la Biashara (International Trade Organization – ITO) Marekani imekuwa ikiagiza chuma kutoka nje mara nne ya kiwango inachouza nje ya nchi hiyo, hali iliyowahi kumshitua Rais wa sasa wa taifa hilo, Donald Trump, kiasi cha kutishia kuweka vikwazo kwa chuma kinachoingizwa nchini humo ili kulinda ajira za ndani na viwanda vya taifa hilo linalotajwa kuongoza kwa nguvu za uchumi duniani.
Lakini vilevile ITO wanabainisha kuwa wakati Marekani inaagiza chuma kutoka nchi zaidi ya 100, robo tatu ya uagizaji huo hutoka katika nchi nane tu.
Muuzaji mkubwa wa chuma kwa Marekani, kwa mfano, kwa mwaka 2017 ni Canada, ikifuatiwa na Brazil, Afrika Kusini, Mexico na Urusi. Mataifa mengine kwenye orodha hiyo ni Uturuki, Japan na Taiwan.
China ambayo inaingia ubia na Tanzania kupitia Kampuni mpya ya kimataifa ya Tanzania China International Mineral Resources Limited (TCIMRL) haimo kwenye kumi bora za mauzo ya chuma kwa Marekani, ikishika nafasi ya 11 licha ya kutajwa kuzalisha nusu ya chuma duniani.
Hata hivyo, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linatarajia kuwa Tanzania inaweza kushika nafasi ya nne barani Afrika katika uzalishaji wa chuma endapo mradi huu utaanza, ikiungana na mataifa mengine Afrika ambayo ni pamoja na Afrika Kusini, Misri, Libya na Algeria.
“Kwa Tanzania, huu ni moja ya miradi mikubwa sana. Utatoa ajira nyingi, zaidi ya 30,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Ni mradi unaokwenda kubadilisha kabisa eneo la mradi na kuligeuza kuwa kitovu cha uchumi na uzalishaji mali. Ni mradi utakaobadilisha taswira ya taifa katika biashara za kimataifa, kutakuwa na masilahi mengi ya kitaifa na kimataifa katika mradi huu,” anasema mhandisi Malesa.
Maelezo ya Malesa yanaungwa mkono na Dk. Nyantahe ambaye anasema, kwa vyovyote vile serikali imefanya uamuzi mzuri wa kufanya uhakiki kwa mara nyingine.
Aina ya mradi
Mradi huo wa ubia umelenga kuchenjua madini kutoka katika chuma – yaani madini aina ya Vanadium na Titanium.
Kiwanda hicho cha uchenjuaji kitahitaji megawati 250 za umeme ambao utapatikana kutoka mradi wa Mchuchuma, JAMHURI likielezwa kuwa mpango uliopo ni kuzalisha umeme takriban megawati 600 kwa kutumia makaa ya mawe.
Kati ya hizo megawati (MW600) zitakwenda kuzalisha katika mradi huo wa kuchenjua madini katika chuma – Liganga (unaohitaji megawati 250).
Njia ya kufikisha umeme huu wa megawati 250 inajengwa ikiwa na uwezo wa kupitisha msongo wa umeme KV 220.
Kati ya hizo megawati 600 za jumla – ukiondoa hizo 250, zinazobaki – 350 megawati zinajengewa njia ya kupitisha umeme wa msongo wa KV400 kutoka Mchuchuma hadi gridi ya taifa Makambako (megawati 350 zinasafirishwa kwenda Makambako). Katika mradi huu, uzalishaji wa chuma unatajwa kuwa utakuwa ni zaidi ya tani milioni moja kwa mwaka.
Mwenendo wa mradi
Mwaka 1996, serikali kupitia uamuzi wa Baraza la Mawaziri ilitoa jukumu kwa Shirika la Mandeleo la Taifa (NDC) kuendeleza mradi wa Liganga.
Mwaka 1997, NDC iliwasilisha maombi ya leseni ya utafiti wa madini (Prospecting License) katika Wizara ya Nishati na Madini (kwa wakati huo iliitwa hivyo) na hatimaye kupata leseni hiyo.
Mwaka 1999, NDC iliomba hati ya umiliki wa ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kupata ‘ofa’ (Letter of Offer) kwa ajili ya mradi huo.
Mwaka 2000, NDC iliipa majukumu mahususi Kampuni ya Mintek ya Afrika Kusini kufanya mapitio ya taarifa zote za kijiolojia, ikiwa ni pamoja na hazina ya mali iliyomo ardhini.
Mwezi Machi mwaka 2007, serikali kupitia waraka wa Baraza la Mawaziri namba 4/2007 iliridhia uendelezwaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma, katika programu ya kitaifa, vilevile programu ya kimataifa.
Machi 30, 2007, Wizara ya Viwanda na Biashara iliteua timu maalumu ya kiufundi ya viongozi waandamizi kusimamia mchakato wa ununuzi (procurement) unaofanywa na mwekezaji katika uendelezaji wa mradi huo kupitia programu ya kimataifa.
Kamati hiyo iliundwa na watu 12 chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Kamishna wa Madini, Dk. Peter Kafumu.