Na ATHUMANI KANJU
Hivi karibuni, Serikali kupitia Kamishna wa Elimu, Dk Edicome Shirima, ilitoa taarifa kwa umma ikizitaka shule binafsi kuwarejesha mara moja katika madarasa yao wanafunzi waliokaririshwa madarasa ama kuhamishiwa shule nyingine kwa kigezo cha kushindwa kufikia wastani uliowekwa na shule husika hadi kufikia tarehe 20 mwezi huu.
Taarifa hiyo inaeleza kwamba kitendo cha kuwakaririsha madarasa, kuwafukuza shule ama kuwahamisha wanafunzi ambao wamefaulu mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nne, Kidato cha Pili ama ule wa Kidato cha Nne, ni kwenda kinyume na Waraka wa Elimu Namba 7 wa mwaka 2004.
Kwa maoni yangu nasema hii inaweza kudhoofisha shule binafsi na huenda ukawa ni mkakati wa Serikali kutaka kujaribu kuleta uwiano baina ya shule binafsi na zile za umma, jambo ambalo litachukua miaka mingi sana kutokea.
Walianza na ada elekezi sasa hivi wamehamia kwenye kulazimisha wanafunzi wasikariri madarasa. Ingawa sikatai kwamba uendeshaji wa shule binafsi lazima uzingatie sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali, lakini naona kuna haja ya Serikali kuacha kuingilia baadhi ya mambo yanayofanywa na shule hizi binafsi.
Ni lazima ifahamike kwamba kusoma shule binafsi siyo haki ya kila Mtanzania isipokuwa tu shule hizi zipo kwa ajili ya wale ambao watakubaliana na vigezo pamoja na masharti ya kujiunga na shule hizi ikiwamo uwezo wa kulipa ada, ufaulu, n.k.
Naomba ninukuu kauli ya Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Suleiman Jaffo, aliyowahi kuitoa hivi karibuni kwamba; “Hatutaziua shule binafsi kwa kuzifungia, badala yake zitakufa zenyewe kwa kukosa wateja pale tutakapoboresha na kuimarisha mazingira ya shule zetu za umma.”
Kauli ya mheshimiwa waziri ni kauli nzuri sana kwamba hakuna haja ya kuzibana shule binafsi katika mambo mbali mbali, badala yake Serikali ielekeze nguvu katika kuboresha shule zake ili kusudi wananchi waamue wenyewe aidha kusomesha watoto wao katika shule binafsi au zile za umma.
Mimi naamini endapo mazingira ya shule zetu za umma yataboreshwa na ufaulu ukaongezeka, huu ndiyo utakaokuwa mwisho wa shule binafsi, kwani kile kinachofuatwa huko kwenye shule binafsi kitakuwa kinapatikana serikakini tena bila malipo.
Ikumbukwe kwamba kabla mwanafunzi hajadahiliwa katika shule hizi binafsi, huwa kuna fomu ya makubaliano anapatiwa mzazi wa mtoto juu ya vigezo na masharti ya shule husika ikiwamo wastani wa ufaulu unaohitajika kwa shule husika ili mwanafunzi aweze kuruhusiwa kuendelea na masomo.
Hakuna siku mzazi amelazimishwa kukubaliana na masharti haya isipokuwa ni mzazi mwenyewe ndiye anayetakiwa kuridhia kumwandikisha mtoto wake katika shule husika ama la.
Sasa kama mzazi amesoma na kuielewa fomu ya kujiunga ambayo kwa mfano inamtaka mwanafunzi apate wastani usiopungua alama 65 kwenye masomo yake ndipo aruhusiwe kuendelea na darasa jingine, dhambi iko wapi endapo mwanafunzi huyu atakaririshwa darasa kwa kushindwa kufikia wastani huo?
Aidha, Serikali imesahau pia kuwa zipo baadhi ya shule na vyuo vya umma hudahili wanafunzi waliofaulu kwa alama za juu zaidi kuliko shule/vyuo vingine.
Kwa mfano, zipo hizi shule zinazoitwa za vipaji maalumu kama Mzumbe, Kibaha, Ilboru, Kisimiri, Tabora (Wavulana), Tabora (Wasichana), Kilakala, Msalato na Loleza ni maalumu kwa wanafunzi waliofaulu kwa madaraja ya juu zaidi katika mitihani yao.
Hata hizi shule nyingine za kawaida za bweni si kila mwanafunzi anayemaliza darasa la saba anaweza kujiunga na shule hizo. Mbali na kuchukua wanafunzi waliofaulu vizuri shule hizo, pia huendelea kuwasisitiza wanafunzi hao wasome kwa bidii vinginevyo watahamishiwa shule za kata.
Sasa kama hata katika shule za umma zinazoendeshwa na kodi ya kila Mtanzania kuna hiyo ‘categorization’ ya wanafunzi, iweje hili lionekane ni kosa linapofanywa na shule binafsi?
Si katika shule za sekondari pekee, hata tukija katika vyuo vikuu vya umma kama Muhimbili, UDSM na UDOM pia kuna tofauti ya vigezo vya udahili baina ya vyuo hivyo na vyuo vingine.
Mimi naona kuendelea kuzibana shule binafsi ni kuua kabisa elimu yetu hasa ukiangalia huko ndiko kulikokuwa tegemeo pekee baada ya shule nyingi za umma kushuka viwango siku za karibuni.
Tatizo letu Watanzania tumezoea kujifariji hata katika vitu ambavyo vinatutaka tujutie. Kwa mfano, tunafurahia kuona idadi kubwa ya wanafunzi wanamaliza shule ama hata vyuo vikuu pasipo kujiuliza wamevuna nini huko shuleni/vyuoni?
Kinachoenda kutokea endapo hili litaruhusiwa ni kwamba tutashuhudia wanafunzi wanaosomeshwa kwa gharama kubwa katika shule binafsi wanamaliza darasa la saba ama hata kidato cha nne hali ya kuwa hawajui hata kusoma na kuandika kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia kwa shule za umma.
Kimsingi kumkaririsha mtoto darasa ni kumsaidia mzazi asipoteze pesa nyingi kugharamia mtu ambaye hana anachokivuna. Waswahili wanasema “kawia ufike.” Ni heri wanafunzi akasoma darasa moja miaka miwili kuliko kukimbilia kumaliza shule ilhali hajapata maarifa ya kutosha.
Kibaya zaidi hawa wanafunzi wanaolazimishwa kuendelea mbele hata kama hawakidhi wastani wa ufaulu, pindi wamalizapo shule na kufeli huanza kuhangaika kurudia mtihani ili waweze kuufikia wastani unaotakiwa kuendelea na ngazi nyingine ya elimu.
Unakuta mtu anahangaika miaka mitatu ‘kuresit’ kidato cha nne ili apate credits za kumuwezesha kujiunga na kidato cha tano.
Sasa hapa mantiki iko wapi? Mmemruhusu mwanafunzi huyu kuendelea mbele matokeo yake amefeli anaanza kuhangaika kurudia mtihani tena akiwa na mzigo mkubwa maana atalazimika kusoma masomo ya madarasa yote kwa muda mfupi. Kipi bora?
Si vyema mwanafunzi ambaye anaonekana kutomudu masomo let say ya kidato cha pili akaendelea kubakia kidato cha kwanza ili ‘a-gain momentum’ kuliko kulazimisha aendelee mbele mwisho wake afeli?
Kitendo cha kuwakaririsha madarasa wanafunzi kinajenga hamasa ya wao kupenda kujisomea kwa kuhofia kuendelea kubakia darasa lile lile huku wenzake wakisonga mbele.
Chukulia mfano wa chuo kikuu jinsi watu wanavyojituma kusoma pasipo hata kushinikizwa kwa kuwa tu kuna utaratibu wa kuwafukuza chuo wale wanaofeli.
Fikiria ingekuwaje kama wote wanaofeli chuo wangeruhusiwa kuendelea na masomo yao nini kingetokea?
Mimi napenda tu kutoa mwito kwa Serikali yetu tukufu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuliangalia suala hili kwa jicho la tatu. Kuna msomi mmoja aliwahi kusema “Ukitaka kuliangamiza taifa hakuna haja ya kushika bunduki na marungu….cheza tu na elimu yake.” Mimi naipenda Tanzania sitaki iangamie….! tusicheze na elimu yetu.
Mwandishi wa Makala hii ni Mwalimu. Anapatikana kwa barua pepe;