Serikali ya Khartoum imeufikisha Umoja wa Falme za Kiarabu mbele ya mahakama ya ICJ, ikiishtaki kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Masalit kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa RSF.
Sudan imeieleza Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu UAE ndio “nguvu inayoendesha” kile ilichokiita mauaji ya kimbari katika jimbo la Darfur, madai ambayo UAE imeyakanusha vikali na kusema hayana ukweli hata kidogo.
Serikali ya mjini Khartoum imeifikisha Umoja wa Falme za Kiarabu mbele ya mahakama ya ICJ, ikiishtaki kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Masalit kwa kuunga mkono wanamgambo wa RSF wanaopambana na jeshi la Sudan tangu mwaka 2023.
Hata hivyo UAE imekanusha kuwaunga mkono wanamgambo hao na imeitaja kesi ya Sudan kama “tamthilia ya kisiasa” na inayoyumbisha juhudi za kuvimaliza vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu.
Wakati mawakili wa pande zote mbili, Sudan na UAE wakitushiana misuli juu ya tafsiri za kisheria katika kesi hiyo, vilio na mateso yanayowakuta raia wa Sudan yanaendelea kuongezeka.
