Sehemu iliyopita, mwandishi wa makala hii, akinukuu maneno ya Kamara Kusupa, alisema hakuna chama hata kimoja, si CHADEMA wala si CUF wala si NCCR – Mageuzi hata hiyo CCM yenyewe vimewahi kushirikisha wanachama wake wote katika uamuzi mkubwa. Upo mfumo maalumu uliobuniwa ndiyo unatumika. ENDELEA na sehemu hii ya mwisho.
Kwa ajili hiyo kinachoendelea kwenye vyama vya siasa ni kuburuzana na kutimuana tu. Hakuna utamaduni wa kuheshimu demokrasia. Chama cha siasa kinaweza kuongoza umma kuwakataa watawala (chama tawala) kwa kutumia nguvu ya watu (kaulimbiu PEOPLE’S POWER au HAKI SAWA), lakini kuwakataa watawala haina maana kwamba chama husika kinaukataa mfumo.
Chama au mtu wa aina hiyo yaani anayetumia nguvu ya umma kuwafukuza watawala kwenye nafasi anayoitamani (urais) hata baada ya kufanikiwa kuwang’oa walioko madarakani, bado viongozi waandamizi wa chama hicho kilichohamasisha umma kuasi, huishia kutumia mfumo ule ule kuendeleza maovu mapya” (Mwinjilisti Kamara Kasupa: HII NDIYO TANZANIA TUNAYOITAKA uk. 284 soma hayo).
Hii imeonekana tangu huko nyuma pale TANU ilipohamasisha Watanganyika kumng’oa mkoloni, lakini walipoingia madarakani tu, maofisa waandamizi wa TANU wote wakawa ma-Regional Commisioner, ma-Area Commisioner, wenyeviti wa taasisi na wakaanza kuimba ‘Chama Kushika Hatamu’ na hapo hapo wengine wakageuza na kusema CHAMA kula UTAMU – kufaidi matunda ya Uhuru.
Kule Zambia, Movement for Democratic Change (MDC) ya Fredrick Chiluba, iliposhika madaraka Novemba, 1991 akina Kennedy Kaunda walionja joto la jiwe (alitiwa ndani – jela). Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamekiri kuwa Tanzania inaweza kujifunza kwa demokrasia kutokana na uchaguzi uliomalizika hivi karibuni nchini Zambia. Hilo mimi siliamini. Kumekuwa na ushindani mkali sana kati ya chama tawala cha Patriotic Front (PF) cha Edgar Lungu na chama cha upinzani cha United Party for National Development (UPND) cha Haikainde Hichilema. Baadhi ya viongozi wa Vyama vya Upinzani wametoa maoni yao, mathalani Twaha Taslima ambaye kawa Kaimu Mwenyekiti (CUF) amenukuliwa akisema “…umefika wakati nchi za Kiafrika kuacha kufanya vyama vya siasa kama vyama vya burudani ikiwemo mpira, kumbe lengo la vyama vya siasa kwa nchi maskini vinapaswa vitumike kuinua maendeleo ya wananchi.”
Katibu wa CHADEMA Dk. Vicent Mashinji amenukuliwa akisema: “Nchi zetu za Afrika kama zinataka kuwa na maendeleo ni lazima viongozi kuheshimu maamuzi ya (uamuzi wa) wananchi, na lazima wapeane nafasi katika uongozi, kwani kung’ang’ania madaraka siyo jambo jema kwa taifa linalotafuta misingi ya demokrasia ya vyama vingi.” Huku Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia, pamoja na mazuri mengi aliyosema juu ya uchaguzi wa huko Zambia, hakusahau kusema kwamba Mwalimu Julius Nyerere alisimamia kwa nguvu zake zote kwamba binadamu wote ni ndugu na Afrika yote ni moja, lakini kitu cha ajabu siasa za Bara la Afrika kumekuwa na siasa za uhasama (tazama Jamhuri toleo No. 257 la tar. 30 Agosti, 2005 uk. 14).
Hivi sasa nchi huru ya Tanzania imejaa UBINAFSI mtupu. Si kwenye vyama vya siasa na wala si serikalini. Watu wanakuwa waoga kuongea ukweli na hapo ndipo unafiki unatawala, majungu na hata ikazuka tabia ya kuunda mitandao. Chanzo chake ni huo woga wa kusema ukweli. Ndani ya vyama vya siasa ukisema ukweli tu, mathalani ukauliza matumizi ya fedha za ruzuku yakoje? Mkoani wanapata? Uongozi utakuita wewe unajidai kuwa mjuaji au kijogoo eti? Baraza Kuu au Kamati Kuu watakujadili na matokeo yake utafukuzwa kwenye chama. Imetokea Unguja hivi majuzi Baraza Kuu limeketi kule Vuga, Unguja katika kikao cha dharura – CUF ikaamua kuwa “purge” viongozi kadhaa akiwamo hata Mbunge wa Kaliua – Unyanyembe kule kwa watani zangu Wanyamwezi. Huo ndio udikteta katika vyama.
Lakini viongozi hao hao wanaukumbatia udikteta ndani ya vyama vyao vya siasa pamoja na kuhodhi madaraka ya utawala kwa muda mrefu mno. Hakuna maendeleo katika nchi, haki za binadamu zinakiukwa, Uhuru wa kukutana na kutoa mawazo hakuna! Hii si ndiyo tabia ya UKINYONGA ninayoisema? Kwa wengine, ukiukwaji wa haki za binadamu ndani ya vyama vyao usiulizwe wala hakuna nafasi mtu mwingine kugombea uongozi wa juu! Ni demokrasia gani hiyo ya ubabe?
Naomba Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA atuoneshe au atuelezee tofauti kati ya udikteta ndani ya CCM na ule wa ndani ya CHADEMA, CUF na NCCR – Mgeuzi. Kweli chama cha siasa chenye mbunge mmoja, huyo huyo Mwenyekiti wa Chama, huyo huyo mteuzi wa wagombea, huyo huyo ndiye msemaji mkuu, hiyo ni demokrasia ya wapi kama si ya ubabe na udikteka?
Viongozi wetu wa vyama vya siasa hebu tafakarini maneno haya juu ya demokrasia, udikteta na uvunjaji wa haki za binadamu. Kristo alisema hivi, “basi mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘ndugu yangu niache nikutoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako; nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako”. (Luka sura 6 mistari 41 – 42). Hili ni fundisho muhimu kwa viongozi wa vyama vya siasa. Wajisafishe kwanza wenyewe ndani ya vyama vyao ndipo waongelee udikteta wa CCM.
Viongozi wote wa vyama vya siasa andaeni kwanza mazingira ya kuendesha vyama kidemokrasia. Pawepo na uchaguzi huru, kila mwanachama aweze kuchagua au kuchaguliwa. Ondoeni ukiritimba wa kuchuja au kuwakata waombaji. Mwisho acheni mfumo wa udikteta ndani ya vyama na ule utaratibu wa kufukuzana. Hali hiyo ikirekebishwa, chama chochote kinaweza kutawala na kuleta demokrasia halisi katika nchi yetu. Hivi sasa kulilia kuing’oa CCM siyo “issue” mradi tuwe na demokrasia halisi ndani ya kila chama cha siasa. Ubabe ni udikteta tu. Na penye udikteta hakuna haki, hakuna uhuru wa kujieleza na hakuna uhuru wa kuchagua. Ni kuburuzwa tu na itifaki ya Baraza Kuu au Kamati Kuu ya chama.
Kule Uingereza, chama cha Conservative wakati wa Cameroon kiliposhindwa tu kura za maoni “kubaki” au “kutoka” katika Umoja wa Ulaya (EU), kiongozi wake, Cameroon akajiuzulu.
Hapa Tanzania, pamoja na kilio cha demokrasia yetu inaminywa, viongozi wangapi walioshindwa katika kinyang’anyiro cha urais wa Jamhuri au wa Zanzibar wamejiuzulu uongozi ndani ya vyama vyao kupisha damu mpya? Ndiyo tafsiri ya demokrasia ya u-kinyonga hiyo- ni kujibadilisha tu alimradi upete, uendelee kuukata licha ya mawazo na uwezo wa kutawala na kuongoza sasa umekuwa butu. (“Obsolete” kwa kiingereza).
Mwisho wa tabia ya ung’ang’anizi katika vyama vya siasa ni hii ya kufukuzana kwa fedheha. Leo naona baadhi ya wanachama wanaulizama eti Profesa Lipumba anataka aendelee kuongoza, ataongoza CUF ipi? Hiyo kama siyo kejeli, wanasiasa mnaiitaje?
Hapa wananchi tunatofautiana sana katika kutafsiri neno hili demokrasia. Kule nchi za Magharibi, tulikoiga sisi, wenzetu, mara baada ya uchaguzi mkuu wanasiasa hawashughuliki na mihadhara tena. Pili, baada ya uchaguzi viongozi wa vyama wanajipanga kwa uchaguzi ujao. Sasa demokrasia maana yake kitafsiri yangu ni ile hali ya kusikiliza na kupokea mawazo ya wachache, uwepo uhuru wa kusema hata yale wengine (viongozi) hawapendi kuyasikia. Watawala wasiogopwe. Kamara Kusupa anasema demokrasia halisi ni kubadili mfumo wote kabisa na kuleta vitu vitatu muhimu:-
*Kuleta UHURU kamili katika nchi yoyote ile
*Kuwepo na DEMOKRASIA ya kweli siyo maneno maneno tu toka ndani ya vyama.
*Kuwepo na HAKI za binadamu wote katika nchi.
Matamko ya viongozi, maneno na vitendo viendane pamoja. U-kinyonga au upopo katika uongozi ni hatari kwa nchi yoyote ile. Matamshi ya viongozi yana uzito wake. Vitisho na malumbano si njia ya kuishi kwa amani. Uzalendo unaelekeza kwenye utaifa na hakuna taifa lisilo na tofauti za mawazo miongoni mwa watu wake.
Kuhitimisha makala yangu hii juu ya u-kinyonga na u-popo ni kwamba matamshi ya viongozi wa vyama vya siasa yawe na ukweli. Tabia ile ya kutangaza tamko zito leo, kesho tamko lile lile linayeyuka ni u-kinyonga.
Ninashukuru sana kuona lile TISHIO LA UKUTA kuandamana Septemba mosi halikutekelezeka. Aidha, lile tamko la UVCCM la kuandamana Agosti 31 nalo halikutekelezwa. Huo ni ukomavu wa viongozi wa vyama vya siasa. Laiti “confrontation” ile ingalitokea katika maandamano napwelea kusema maisha ya Watanzania wasio na hatia yangeweza kupotea bila sababu za msingi. Balaa limeepukika kutokana na maongozi ya Mungu Mwenyezi.
Tupongezane kushinda kishawishi cha ulimi uliowasha moto wa kiburi cha kudai demokrasia inaminywa na itadaiwa kwa njia yoyote ile hata kupambana na dola! (By hooks or crooks). Basi munkari utulizwe na upendo na amani vitawale.
Bado naona viongozi wa vyama vya siasa wanaona upande mmoja tu wa demokrasia – upande wa haki za binadamu tu. Je, wanaona na upande ule wa pili wa demokrasia? Upande wa wajibu unaombatana na demokrasia? Maana kuna HAKI na kuna WAJIBU – “RIGHTS” and fitting DUTIES”. Wajibu wa kuheshimu na wa kutii mamlaka halali mbona hawaufuati? Hata kodi ya majengo tu hawalipi ni kuwajibika gani huko?
MUNGU IBARIKI TANZANIA.