Mtandao wa Twitter umewataka watuamiaji wake zaidi ya milioni 330 kubadili nywila (password) zao baada ya kubaini tatizo lililosababaishwa nywila za baadhi ya watumiaji kuwa wazi (unmasked) tofauti na zilivyokuwa zinatakiwa kuwa zimefunikwa (masked) katika mfumo wa kompyuta.

Twitter imetoa taarifa hiyo kuanzia Alhamisi mchana kupitia blogu yake lakini pia imetuma ujumbe kwa kila mtumiaji ikimtaka kubadili nywila yake ili kujihakikishia usalama zaidi.

Katika taarifa hiyo, Twitter imeeleza uchunguzi umefanyika na tatizo hilo limetatuliwa, na hakuna dalili zozote zinazoonesha kwamba kuna nywila zimeibwa au akaunti ya mtu kutumiwa vibaya.

Katika taarifa hiyo hawakueleza ni akauti ngapi ziliathiriwa, lakini imeelezwa kwamba, nywila hizo zilikuwa wazi kwa muda mrefu kabla ya tatizo hilo kugundulika.

Kampuni hiyo imeeleza kwamba, unapoingiza nywila kwenye akaunti yako, huzibadili na kuwa namba ili mtu asiweze kutambua nywila yako, na kisha hizihifadhi katika mfumo wao. Hatua hiyo huwezesha mfumo wao kuthibitisha taarifa za akaunti yako bila kuonesha nywila yako.

Wameomba msamaha kufuatia hatua hiyi inayotishia usalama wa taarifa za watumiaji wake, na kuahidi kuwa tatizo hilo limekwisha na kuwataka watumiaji kuendelea kutumia mtandao huo.